MAAFA: WATU 23 WAFARIKI DUNIA KWA KUKOSA DAWA ZA MALARIA MULEBA





KUMETOKEA maafa makubwa ya vifo vya watu 23, wilayani Muleba mkoani Kagera kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa malaria. Kati ya vifo hivyo, watu 23 ambapo kati yao watoto 16 chini ya umri wa miaka mitano na watu wazima 7, wamefariki kati ya Mei 20 hadi Mei 31, mwaka huu.

Akizungumza na MTANZANIA Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kaloinisa Pathan alikiri kutokea kwa vifo hivyo na kusema Serikali inachukua hatua za kila aina kukabiliana na tatizo hilo. “Ni kweli tumepatwa na tatizo kubwa la mlipuko wa ugonjwa wa malaria, mpaka mwishoni mwa wiki watu 23 wamefariki dunia kati yao kuna watoto 16, waliochini ya miaka mitano. Serikali ya mkoa inafanya jitihada zote kupambana na tatizo hili,” alisema Pathan.

Alisema tatizo hilo, limepatiwa ufumbuzi kwa kiasi, baada ya kupokea dawa nyingi za kutibu ugonjwa huo ambao unaonekana kuzidi kushamiri kwa kasi kubwa wilayani humo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Lembres Kipuyo alisema vilitokea katika Hospitali Teule ya Rubya na kazi ya kudhibiti inaendelea.

Alisema vifo vingi, vilichangiwa na uhaba wa madawa na kasi ndogo ya wauguzi kutibu wagonjwa.

Alisema uongozi wa wilaya hiyo, kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa, umeweka mikakati madhubuti ya kudhibiti ugonjwa huo.

Alisema moja ya mkakati huo, ni pamoja na namna ya kupata dawa kwa ajili ya kudhibiti mlipuko huo ambao ni tishio kwa maisha ya watu.

Alisema hatua nyingine, ni uongozi wa Wilaya ya Muleba umeanza kazi ya kuwahamasisha wananchi wanaoishi kwenye maeneo yaliyoathirika.

Alisema maeneo ambayo yamekumbwa na mlipuko wa ugonjwa huo, ni yale ya vijiji vinavyozunguka mto Ngono ambao maji yake hutiririka hadi wilayani Missenyi.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili, waliutupia lawama uongozi wa wilaya kwa kushindwa kuchukua hatua haraka.

Walisema mara kwa mara, wananchi wamekuwa wepesi kutoa taarifa kwa uongozi wa hospitali, lakini uongozi hauonyeshi hatua zozote.

Walisema wananchi wengi ambao walipeleka wagonjwa, walijikuta katika wakati mgumu kutokana na wagonjwa wao kunyimwa msaada. 

"Ndugu waandishi msidanganywe, hata waliolazwa wodini mkiwaona afya zao sio nzuri upo uwezekano wa kutokea vifo vingine vingi zaidi, hali ni mbaya sana, muandike taarifa sahihi msipotoshwe na baadhi ya viongozi wanaotaka kufagilia unga wao," alisema mmoja wa wananchi.

"Hapa viongozi hasa wa halmashauri ya Wilaya ya Muleba, wanapaswa kuwajibika kwa suala hili, mimi binafsi naiomba Serikali ichukue suala hili kwa umakini zaidi, kwa kuwa wameonyesha uwajibikaji mdogo," alisema mwananchi mwingine bila kutaja jina lake.

Kufuatia kuzuka kwa mlipuko wa ugonjwa huo, Hospitali ya Rubya imefurika wagonjwa kiasi cha uongozi wa hospitali kulazimika kuwalaza wagonjwa zaidi ya watatu kwenye kitanda kimoja.

MBUNGE

Kutokana na hali hiyo, Mbunge wa Muleba Kusini ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ametoa msaada wa vyakula vyenye thamani ya Sh milioni 1.5.

Msaada huo, ulikabidhiwa kwa niaba yake na katibu wake wa jimbo hilo la Muleba Kusini, Denis Mutajwaha.

Hii ni mara ya pili, mlipuko wa ugonjwa wa malaria kutokea wilayani Muleba, karibu miaka mitano iliyopita na kusababisha vifo vya wengi.


CHANZO: Mtanzania
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment