KAMBI rasmi ya upinzani imeibua upya hoja ya tiba ya asili, maarufu kama Kikombe cha Babu wa Loliondo, ikihoji kwamba Serikali haijatoa kauli wala kuchukua hatua dhidi ya Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwaisapile aliyekuwa akitoa tiba hiyo.
Msemaji Mkuu wa kambi hiyo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Antony Mbassa alihoji jana bungeni katika hotuba yake kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2013/2014.
Alisema kwa mujibu wa aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda, watu 116 walifariki dunia kutokana na sababu mbalimbali wakiwa kijiji cha Samunge, ilikokuwa ikitolewa tiba hiyo na mchungaji Mwaisapile.
“Mpaka leo Serikali haijasema chochote kuhusu uchunguzi wa dawa ya babu. Mpaka leo Serikali haijatoa kauli yoyote wala kuchukua hatua yoyote dhidi ya Mzee Mwaisapile ambaye Februari hii alitoa kauli nyingine juu ya ugunduzi wa dawa nyingine,” alisema Mbassa.
Kwa mujibu wa Mbassa, timu ya uchunguzi iliyoundwa mpaka Machi 2011 ilikuwa imeandaa kukamilisha taratibu, ili kufuatilia maendeleo ya kiafya ya wagonjwa 200 ambao wamekubali kwa ridhaa yao kushiriki katika utafiti huo kuona maendeleo yao ya kiafya baada ya kunywa dawa hiyo.
Wakati huo huo, kambi hiyo ya upinzani imeishauri Serikali kutoa taarifa rasmi kwa wananchi juu ya dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi (ARVs) makopo 4,000, ambazo hazijakusanywa ili kuwaondolea mashaka na kuwajengea imani watumiaji.
Kambi hiyo imesema kuwa sakata la kuwepo ARVs bandia lililochukua miezi minane sasa, limekuwa na sura tofauti hususan juu ya nani anahusika moja kwa moja baada ya kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industry (TPI), kukanusha kuhusika wakati Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Bohari Kuu (MSD) wakisisitiza zimetoka kiwandani hapo.
“Wakati taratibu za kitaalamu na kisheria zikiendelea tunaishauri Serikali kutoa taarifa rasmi kwa wananchi juu ya dawa ambazo hazijakusanywa. Je, ziko vituoni au zilishatumiwa na wananchi? Kama zilishatumiwa, je, serikali ina taarifa zozote juu ya waliozitumia dawa hizo? Je, kuna madhara yoyote waliyoyapata kutokana na kuzitumie?” alisema.
Kulingana na taarifa ya kambi ya upinzani, jalada la kesi ya ARVs bandia limepokelewa na linashughulikiwa na Mkurugenzi wa Mshitaka (DPP) ili kupata mwelekeo wa nani ahusishwe na kwa kosa gani kabla ya kuachia mamlaka husika jukumu la uchunguzi wa kina.
Taarifa hiyo ya kambi inasema ofisi ya DPP ilitoa maelezo kwamba suala hilo limechukua muda mrefu zaidi ya miezi miwili tofauti na muda wa kawaida wa siku 14 unaotumiwa na ofisi hiyo kushughulikia kesi mbalimbali zinazofikishwa kutokana na uzito na unyeti wa suala hilo.
CHANZO: Habari Leo
0 comments:
Post a Comment