Pinda awaangukia viongozi wa dini

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda



  WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amewaomba viongozi wa dini kuisaidia Serikali    kuyaunganisha makundi yote ya kijamii pindi linapotokea jambo lolote linalotishia amani ya Taifa. Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana wakati wa kumweka wakfu, Askofu Lucas Mbedule wa Dayosisi mpya ya Kusini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT). Kauli ya Pinda imekuja siku chache baada ya kutokea vurugu zilizofanywa na baadhi ya wakazi wa Mtwara, wanaopinga ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.

Vurugu hizo zilitokea wiki iliyopita baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kumaliza kusoma mwelekeo wa bajeti ya mapato na matumizi ya wizara hiyo.

Aidha, vurugu hizo zilisababisha uharibifu mkubwa wa mali na uvunjifu wa amani, ambapo nyumba zilichomwa moto, miundombinu iliharibiwa na kusababisha majeruhi na vifo.

“Iwe dhehebu kwa dhehebu, dini kwa dini, wananchi na vyama vya siasa au wananchi na Serikali, lazima watu waunganishwe pindi linapojitokeza jambo lolote lisilo sawa.

“Nawaomba mkutane na makundi husika na kuyasuluhisha kwa ajili ya kuleta umoja wa kitaifa,” alisema Pinda.

Aidha, aliwaomba Watanzania wote wanaoishi maeneo ya Kusini mwa Tanzania, kutokubali kuharibu amani na umoja uliokuwapo miongoni mwetu.

“Napenda nitumie nafasi hii kuwaasa Watanzania wote wanaoishi maeneo haya ya Kusini kwamba chonde chonde, tusikubali kuharibu amani na umoja tuliojijengea tangu kuanzishwa kwa Taifa hili.

“Bila shaka wote ni binadamu, hatujakamilika na tunayo nafasi ya kukaa chini pamoja na kujadiliana nini cha kufanya pale tunapoona mambo hayaendi sawa na tunavyotarajia,” alisema Pinda.

Alisema matarajio yake ni kwamba, viongozi wa dini watakuwa mstari wa mbele katika kuiweka jamii yote pamoja bila kujali dini, kabila, itikadi na jinsia.

“Pamoja na furaha tuliyokuwa nayo leo (jana) ya kuwekwa wakfu Baba Askofu Lucas Mbedule, bado tuna changamoto nyingi zinazolikabili Taifa letu, zikiwamo za kijamii na kiuchumi.

“Nchi yetu pia kwa sasa inakabiliwa na ukosefu na uhaba wa ajira na ukosefu wa mikopo ya kufanya biashara hasa kwa vijana, lakini pia yapo matatizo, kwa mfano, suala zima la mmomonyoko wa maadili katika jamii hasa miongoni mwa vijana wetu,” alisema Pinda.

Alisema Serikali inatambua umuhimu wa viongozi wa dini katika kuijenga jamii yenye umoja na yenye utamaduni wa kupenda.

“Tuepuke kuotesha mbegu mbaya ya udini, ubaguzi na ukabila, tujenge umoja na mshikamano kwa manufaa ya wananchi wetu na Taifa letu,” alisema Pinda.

Aliwaambia wananchi wa Mtwara kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuwaletea maendeleo kwa ajili ya maisha bora.

“Napenda kuwaomba wananchi wote wa maeneo haya ya kusini mwa nchi yetu hususani Mtwara kwamba, Serikali inatambua umuhimu wa kuwaletea maendeleo kwa ajili ya kuwajengea maisha bora kwa kuwa tunalo jukumu la kuhakikisha wananchi wetu wanapata maendeleo kwa usawa bila ubaguzi wowote,” alisema Pinda.

Katika hatua nyingine, alisema kampuni 45 kutoka nchi mbalimbali zimeomba kuwekeza viwanda mkoani Mtwara, ikiwa ni pamoja na kiwanda kikubwa cha saruji baada ya ugunduzi wa kiasi kikubwa cha gesi asilia katika Bahari Kuu Kusini mwa Tanzania.

Alisema leo ataweka jiwe la msingi la Kiwanda cha Saruji cha Dangote, ambacho ni cha Kampuni ya Dangote Industries ya Alhaj Dangote wa Nigeria.

Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu za saruji kwa mwaka sawa na mifuko 150,000 na kitaajiri wafanyakazi 1,000 ndani ya kiwanda na wengine 9,000 wa nje watakaokuwa mawakala, wasafirishaji, wajenzi na wauzaji rejareja.

Kuna viwanda vinne vya saruji nchini hivi sasa vyenye uwezo wa kuzalisha tani 3,000 kwa mwaka.

Viwanda vingine vinavyotarajiwa kujengwa Mtwara ni pamoja na viwanda vya mbolea, bidhaa za plastiki na kusindika gesi asilia katika mitungi.

Bandari ya Mtwara nayo itapanuliwa na itajengwa reli kuunganishwa Mtwara na machimbo ya chuma ya mikoa ya jirani.

Alisema ofisi yake ndiyo inayoratibu Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na viwanda vitakavyoanzishwa Mtwara kutokana na ugunduzi wa gesi asilia, vitakuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi kwa wananchi wa Mtwara na Taifa kwa ujumla.

“Hadi sasa kituo cha uwekezaji cha TIC kina maombi takriban 45 ya uwekezaji mkoani Mtwara, ikiwamo kiwanda cha mbolea na bidhaa za plastiki.

“Vyote hivi, vitakuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi kwa wananchi wa Mtwara na Taifa kwa ujumla, hususan ajira,” alisema.

Kuhusu tatizo la maji mkoani Mtwara, alisema amemuagiza Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, kuleta wataalamu mkoani humo kuona uwezekano wa kupata maji kutoka Mto Ruvuma unaotenganisha Tanzania na Msumbiji.

Aidha, aliahidi kushughulikia maombi ya KKKT kupata eka 30 za ardhi kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha elimu katika Wilaya ya Masasi.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa KKKT, Alex Malasusa, aliwataka viongozi wa dini wasigombee waumini kama daladala bali wanatakiwa kuwa kitu kimoja.

“Nawaombeni viongozi wenzangu msigombanie waumini kama daladala, naombeni tuwe kitu kimoja na tushirikiane katika utendaji kazi wetu wa kuwaongoza waumini,” alisema Askofu Malasusa.
CHANZO:MTANZANIA
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment