Rais dhaifu CCM 2015

*Sitta, Mwakyembe, Magufuli na Membe katika mizani ya uadilifu
*Dk. Bana asema wanamvuruga Rais Kikwete, wamepwaya kiuongozi
*Prof. Safari awaita matapeli wa kisiasa, Dk. Slaa awapuuza

Samuel Sitta
Bernard Membe
SIKU moja baada ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta kutangaza timu inayoundwa na kundi lake kuwania ukuu wa dola mwaka 2015, maswali yameibuka kuhusu uadilifu wa timu hiyo.

Juzi wakati akizungumza katika kongamano la Mawasiliano katika Nyanja ya Digitali la wanafunzi wa idara ya uhusiano na Masoko wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) jijini Mwanza, Sitta aliitaja timu hiyo inayoundwa na watu wanne kuwa mmoja wao atawania urais katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.
Dk. Harrison Mwakyembe
Alisema wanaounda timu hiyo ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli na Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe.
Dk. John Magufuli
Kutajwa kwa vigogo hao kumeibua maswali toka kwa wachambuzi na wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa nchini, ambao wamechambua wasifu wa kila mmoja ikiwa ni pamoja na kupima utendaji na uadilifu wao kama wanafaa kupewa dhamana ya kuongoza nchi.

Sitta
Sitta ambaye kabla ya kuwa Waziri wa Afrika Mashariki, aliwahi kuwa Spika wa Bunge, baadhi ya wachambuzi wanamuelezea kuwa ni mwanasiasa mlafi wa madaraka, udhaifu ambao ulimsababishia afarakane na baadhi ya wanasiasa wenzake ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Watu wanaomfahamu Sitta, wanadai kuwa udhaifu wake huo ndio uliomtuma ashiriki siasa chafu ambazo kwa kiasi kikubwa zilisababisha kukiathiri chama.

Sitta kwa kushirikiana na Dk. Mwakyembe, wanadaiwa kushiriki kuiua CCM kutokana na kutajwa kuwa nyuma ya mpango wa kuanzisha chama kingine cha siasa, Chama cha Jamii (CCJ), wakiwa bado CCM.

Inadaiwa kuwa uroho wa madaraka ulimsukuma Sitta kushiriki kuuaminisha umma alikuwa akipambana kuibadili CCM kutoka kwenye makucha ya matajiri na mafisadi wachache, akijipambanua kuwa ni mpambanaji wa ufisadi.

Ni katika msingi huo huo Spika Sitta aliunda Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Mwakyembe kuchunguza uhalali wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond, ambayo ilimuondoa madarakani aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa.

Sitta akishirikiana na baadhi ya wanasiasa akiwemo Dk. Mwakyembe wanashutumiwa kwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha ukuaji wa uchumi nchini, kutokana na hatua ya kushinikiza kutonunuliwa mitambo ya Dowans iliyorithi mkataba wa kampuni ya Richmond kwa madai kuwa ni ya kifisadi.

Ni tabia hiyo ya usaliti ya Sitta ndiyo inayoelezwa kuchagiza harakati zilizoongozwa na Rais Jakaya Kikwete, kumuondoa katika wadhifa wa uspika na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa naibu wake Anne Makinda.

Wanaoamini hivyo, wanarejea taarifa zilizopata kuvuma pasipo yeye mwenyewe kuzitolea maelezo za kusudio lake la kutaka kujiunga na Chadema ili apate madaraka baada ya kufarakana na waliokuwa maswahiba wake wa kisiasa ndani ya CCM.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanadai kuwa baada ya kupima upepo wa kisiasa, Sitta alisitisha uamuzi huo wa kuhamia Chadema kabla chama chake hakijampooza na kumpa uwaziri, baada ya uchaguzi wa mwaka 2010.

Akiwa Spika, Sitta pia aliwahi kukumbwa na kashfa ya ujenzi wa chini ya kiwango wa ukumbi wa Bunge jipya, bunge hilo lililojengwa kwa mabilioni ya fedha lakini sasa linavuja na ukaguzi umeonyesha kuwa halikujengwa kwa kiwango stahiki na hakuna mitambo ya usalama iliyofungwa ukumbini humo na wakati huo huo kupoteza nyaraka za jengo hilo ya michoro yake.



Ofisi ya Mbunge
Wanaompima Sitta kama anaweza kuongoza nchi, pia wanaliangalia Jimbo lake la Urambo aliloliongoza kwa takribani miaka 35, ambalo hadi leo linadaiwa kuwa liko nyuma kimaendeleo.

Ni kwa muktadha huo, baadhi ya wachambuzi wanahoji kama alishindwa kuliongoza jimbo lenye watu wachache na kulivusha kwenye maendeleo, je ataweza kuongoza nchi yenye watu zaidi ya milioni 40?

Pamoja na hilo pia anadaiwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kujenga ofisi ndogo ya Spika, ambayo yeye aliita ya Mbunge jimboni humo.

Ingawa Serikali iliridhia ofisi za wabunge zijengwe kwa kiasi cha fedha kisichozidi Sh milioni 40 kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha, ofisi hiyo ya Sitta jimboni Urambo, ilijengwa kwa Sh Milioni 350.

Wakati huo huo alikuwa akidaiwa kujitibu kwa gharama ya shilingi milioni mbili kwa kununua dawa za mamilioni ya fedha ili kutibu mguu, alizonunua katika moja ya duka la dawa jijini Dar es Salaam.


Matumizi holela ya nyumba za Serikali
Sitta ni mmoja wa vigogo waliopatiwa nyumba za Serikali, wakati watumishi wengine wa Serikali wakikosa makazi na kuishi hotelini kwa gharama kubwa, zinazolipwa na Serikali, Sitta ameendelea kuitumia nyumba hiyo kiholela kwa kuweka biashara ya pombe.

Dk. Mwakyembe

Usaliti CCM

Kama ilivyo kwa Sitta, wafuatiliaji wa siasa za hapa nchini pia wanatilia shaka uadilifu wa Dk. Mwakyembe, kwa sababu ya uswahiba wake na Sitta na kubeba hoja zinazofanana.

Chanzo uchumi kudorora

Dk. Mwakyembe ambaye ni Msomi na Mwanasheria nguli, wakati akiwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge ya kuchunguza sakata la Richmond, anadaiwa kuwa alishiriki kuiaminisha uongo Serikali na umma wa Watanzania kuhusu kampuni ya Richmond.

Akiwa Mwenyekiti wa kamati hiyo teule, Dk. Mwakyembe na kamati yake walitoa maazimio 23 ambayo Bunge liliitaka Serikali iyatekeleze, hadi sasa ni maazimio 10 tu yameshafanyiwa kazi huku mengine 13 yakiwa bado hewani na yasiyozungumziwa hata na yeye mwenyewe.

Hata hivyo Dk. Mwakyembe anadaiwa kuipinga kampuni ya Dowans kwa sababu ya maslahi yake, kutokana na kile kinachodaiwa kuwa kampuni hiyo ilikuwa ni mshindani wa kampuni ambayo anadaiwa kuwa mmoja wa wamiliki wake ya kufua umeme.

Dk. Mwakyembe ilibainika kuwa ni miongoni mwa watu tisa wenye hisa katika kampuni binafsi ya kufua umeme wa kutumia nguvu za upepo ya Power Pool East Africa Ltd, ambapo yeye anamiliki hisa 1,485 katika kampuni hiyo.

Kampuni hiyo tayari imeshapata maeneo ya kuwekeza katika maeneo ya Makambako mkoani Iringa na Singida.

Maeneo hayo yanadaiwa kuwa na upepo mkali ambao ndiyo malighafi muhimu, hivyo ujasiri wa Dk. Mwakyembe katika kuishambulia kampuni ya Richmond na Dowans, unatokana na mgongano wa kimaslahi.

Ufisadi

Kashfa nyingine inayomkabili ni ya ujenzi wa bandari ya nchi kavu kwa kampuni inayomilikiwa na CCM, kinyume cha sheria za manunuzi.

Kampuni hiyo ya Jitegemee Trading Company, ilipewa zabuni ya ujenzi wa bandari katika Viwanja vya Sukita bila kuwa na mchakato wa kushindanisha kampuni nyingine.

Bernard Membe

Urais wa maadui

Wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa pia wameuchambua udhaifu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe wakisema kuwa hana uvumilivu baada ya kudhihirisha udhaifu wake kuwa anao maadui 11, kati yao wawili wakiwa ni waandishi wa habari ambao alidai pindi atakapokuwa Rais atawashughulikia.

Kupigiwa debe na familia ya JK

Membe pia anatajwa kuwa dhaifu kutokana na kushindwa kusimama yeye mwenyewe kisiasa na hivyo kutegemea msaada wa familia ya rais Kikwete.

Wanaouelezea udhaifu wa aina hiyo wa Membe wanakumbuka jinsi mwanasiasa huyo alivyopigiwa kampeni ya ujumbe wa NEC na mke na mtoto wa Rais, hali inayowalazimu watu kuamini kuwa Membe hana uwezo wa kujiamini.

Ikumbukwe kuwa Membe alishatangaza nia ya kugombea urais mwaka 2015 kwa kivuli cha kuombwa na wananchi kufanya hivyo.

Kashfa ya Ufisadi fedha za Libya

Ingawa Rais anapaswa kuwa mwadilifu na muwajibikaji, Membe anatajwa kuwa alipewa fedha za nchi huko Comoro, Morocco na Libya, lakini akazitia mfukoni.

Ilidaiwa kuwa Waziri huyo alizitumia fedha hizo kwa ujenzi wa hoteli kubwa katika makao makuu ya moja ya mikoa ya Kusini mwa Tanzania.

Fedha hizo za mkopo dola za Marekani milioni 20, zilitolewa na Serikali ya Libya wakati wa utawala wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Hayati Muamar Gaddafi.

Pamoja na kudai kuwa fedha hizo zilipaswa kupewa kampuni moja ya Meize, kwa ajili ya kujenga kiwanda cha saruji mkoani Lindi, Membe aliendelea kujikanganya na kudai kuwa kampuni ya Mohamed Enterprises ilikuwa inashirikiana na ofisa mmoja wa ubalozi wa Libya ili apate fedha hizo ambazo mpaka sasa zimeendelea kubaki kuwa kitendawili.

Dk. John Magufuli

Ufisadi

Kwa upande wake Dk. John Magufuli ambaye ni Waziri wa Ujenzi, naye uadilifu wake kama kiongozi unatiliwa shaka kutokana na kukumbwa na kashfa ya upotevu wa shilingi 252,975,000,000 zilizolipwa kwa mradi hewa, ambapo kiasi hicho cha fedha kinadaiwa kuwa kingeweza kujenga barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 316.218.

Uamuzi wa kukurupuka

Baadhi ya maamuzi mengine ya Dk. Magufuli yamelitumbukiza taifa katika hasara kubwa kama lile la kesi ya uvuvi haramu, ambapo taifa lililazimika kulipa mabilioni ya fedha kama gharama za kuhifadhi samaki hao wakati kesi hiyo ikiwa mahakamani.

Kama kiongozi ambaye anatakiwa kusikiliza ushauri na kufuatilia kero na malalamiko ya anaowaongoza, Dk. Magufuli amekuwa mzito ambapo watumishi wa wizara yake wanamtaja kama mtu asiyeshaurika.

Uamuzi mwingine wenye utata ambao uliligharimu taifa ni kuhusu suala la kuuza nyumba za Serikali, ambalo hadi leo taifa linaujutia, upo ukweli kuwa alihusika kugawa nyumba hizo hadi kwa ‘vimada’ wake, jambo ambalo linatiliwa shaka uadilifu wake kiuongozi.
CHANZO:MTANZANIA
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment