HOTUBA YA WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA, MATHIAS M. CHIKAWE (MB.)



HOTUBA YA WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA, MHESHIMIWA MATHIAS M. CHIKAWE (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI
YA FEDHA KWA MWAKA 2013/2014







A.      UTANGULIZI

1.      Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa yangu niliyoiwasilisha kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala tulipokutana kwa lengo la kujadili na hatimaye kupitisha maombi ya Mpango na Bajeti ya Wizara yangu, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha ya Wizara Katiba na Sheria, uliopitishwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kwa Mwaka wa fedha 2013/2014.

Muundo wa Wizara na Majukumu Yake

2.      Mheshimiwa Spika, kulingana na Muundo wa Wizara yangu, majukumu yanayotekelezwa yanajumuisha;- kuratibu mfumo wa utoaji haki nchini, kusimamia mambo ya katiba na utawala wa sheria, kuendesha mashtaka na kuitetea Serikali mahakamani ,na kusimamia utaratibu wa kutoa huduma ya msaada wa sheria kwa jamii. Majukumu hayo yanatekelezwa na Taasisi zifuatazo:-

i.          Mahakama ya Tanzania;
ii.         Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali;
iii.        Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora;
iv.       Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania;
v.        Tume ya Utumishi wa Mahakama;
vi.       Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA); na
vii.      Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (Law School of Tanzania)

B.      MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013

            Malengo ya Mwaka 2012/2013

3.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Wizara ilipanga kutekeleza malengo ya Muda wa Kati kwa kuzingatia maeneo ya kipaumbele kama ifuatavyo:-

i.          Uratibu wa Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba;
ii.         Usimamizi wa Usikilizaji na Uendeshaji wa Mashauri;
iii.      Uimarishaji wa Shughuli za Usajili, Ufilisi na Udhamini;
iv.      Uimarishaji na Uboreshaji wa Vyuo vya Mafunzo ya Sheria;
v.       Uimarishaji wa Utoaji wa Ushauri wa Kisheria Nchini;
vi.      Kufanya tafiti, mapitio, uandishi wa Sheria, Kanuni na Hati Mbalimbali; na
vii.     Usimamizi wa Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Uratibu wa Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba

4.      Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2012/2013 Wizara yangu imeendelea kuratibu Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba. Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeanza kazi rasmi tarehe 01 Mei, 2012. Madhumuni ya kuanzishwa kwa Tume ni kuratibu, kukusanya, kuchambua na kutathmini maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko ya Katiba. Kwa kuzingatia muda ambao Sheria imeelekeza, Tume imeweka malengo ya kuwezesha kupatikana kwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ifikapo Aprili 26, 2014.

5.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2012/2013, Tume ilitekeleza shughuli zake kama ifuatavyo:-

(i)         Kutoa elimu kwa umma na kuhamasisha wananchi kushiriki katika hatua zote za mchakato wa mabadiliko ya Katiba kupitia vyombo vya habari (Redio, Luninga, Magazeti, Tovuti) machapisho mbalimbali na katikamikutano;

(ii)        Kuandaa na kusambaza nakala 1,700,000 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, nakala 400,000 za Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83, Katiba ya Zanzibar nakala 19,000,Vipeperushi 800,000 vinavyoeleza majukumu ya Tume, Vipeperushi 670,000 vyenye maswali yanayoulizwa mara kwa mara na majibu yake nakala 588,600 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba sura ya 83 kwa lugha nyepesi;

(iii)       Kuandaa mifumo/njia mbalimbali ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi kama vile mikutano ya hadhara katika Wilaya zote nchini, mikutano ya Makundi Maalum, tovuti na mitandao ya kijamii, barua kwa njia ya posta, barua pepe, nukushi, ujumbe wa simu, makala, kujaza fomu maalum za Tume pamoja na magazeti;

(iv)      Kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Mabadiliko ya Katiba katika Wilaya zote nchini na kuyachambua maoni hayo;

(v)       Kuandaa, kuchapisha na kusambaza nakala 50,000 za Mwongozo kuhusu Muundo na Utaratibu wa kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya (Mamlaka ya Serikali za Mitaa);

(vi)      Kutoa elimu kwa umma kuhusu utaratibu wa uundwaji wa  Mabaraza ya Katiba, majukumu ya Mabaraza hayo na kuandaa ratiba ya uchaguzi wa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba (Mamlaka ya Serikali za Mitaa);

(vii)     Kuunda Mabaraza ya Katiba ya Wilaya (Mamlaka ya Serikali za Mitaa;

(viii)Kusimamia uchaguzi wa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya (Mamlaka ya Serikali za Mtaa);

(ix)      Kuandaa Mwongozo wa Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu; na

(x)       Kuandaa Ripoti ya Awali na Rasimu ya Katiba.

6.      Mheshimiwa Spika, Tume hii pia, inalo jukumu kubwa la kusimamia Mabaraza ya Katiba. Tume imeyagawa Mabaraza ya Katiba katika Makundi mawili; kundi la kwanza ni Mabaraza yatakayosimamiwa na Tume (Mabaraza ya Katiba ya Wilaya – Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa)na kundi la pili ni Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu wenye malengo yanayofanana.

Hadi sasa Tume imeweza kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba katika Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa kupitia chaguzi na taratibu mbalimbali ambapo jumla ya Wajumbe 10,932 wamepatikana katika Mikoa 17. Katika kufanikisha kupatikana kwa Wajumbe, Tume ilitumia Mfumo wa Serikali za Mitaa na taratibu za Mikutano katika ngazi za Serikali za Mitaa zilizopo sasa (Vijiji, Mitaa na Kata).Utaratibu huu ndio ulioainishwa kwenye Sheria zinazosimamia Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Aidha, kwa mujibu wa Ratiba ya shughuli za Tume, mikutano ya Mabaraza ya Katiba itaanza mwezi Juni, 2013 na itaendelea hadi mwezi Agosti, 2013.

7.      Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kifungu cha 10 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayo mamlaka na uhuru katika utekelezaji wa majukumu yake. Aidha, Tume imekuwa na utaratibu wa kutoa taarifa kuhusu jambo lolote linalopangwa kutekelezwa na kutoa taarifa baada ya utekelezaji wake kupitia mikutano na vyombo vya habari, magazeti, majadiliano katika redio, luninga na majarida ya kijamii.

Usikilizaji wa Mashauri nchini

8.      Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2012/2013 Mahakama ya Tanzania imesikiliza mashauri katika ngazi mbalimbali kama ifuatavyo:-
i.           Mahakama ya Rufani ilianza Mwaka wa Fedha wa 2012/2013 ikiwa na idadi ya mashauri 1,743yaliyosalia kutoka miaka ya nyuma. Aidha, Mahakama ya Rufani ilipokea mashauri mapya 450 na hivyo kuwa na jumla ya mashauri 2,193. Katika kipindi cha kuanzia Julai, 2012 hadi Machi, 2013 Mahakama imesikiliza na kuyatolea maamuzi jumla ya mashauri 275 sawa na asilimia 13 ya jumla ya mashauri yote na hivyo kubaki na jumla ya mashauri 1,918. Aidha, uwezo wa wastani wa uondoaji wa mashauri (Clearance Rate) katika Mahakama ya Rufani kwa tathmini ya kipindi cha miezi sita iliyopita ni asilimia 61. (Jedwali Na.1)

ii.          Mahakama Kuu ilianza Mwaka wa Fedha wa 2012/2013 ikiwa na idadi ya mashauri 9,737yaliyosalia kutoka miaka ya nyuma. Aidha, Mahakama Kuu ilipokea mashauri mapya 7,547 na hivyo kuwa na jumla ya mashauri 17,284. Katika kipindi cha kuanzia Julai 2012 hadi Machi 2013 Mahakama Kuu imesikiliza na kuyatolea maamuzi jumla ya mashauri 5,191 sawa na asilimia 30 ya jumla ya mashauri yote na hivyo kubaki na jumla ya mashauri 12,093. Aidha, uwezo wa wastani wa uondoaji wa mashauri (Clearance Rate) katika Mahakama ya Kuu kwa tathmini ya kipindi cha miezi sita iliyopita ni asilimia 70. (Jedwali Na.2)

iii.         Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, ilianza Mwaka wa Fedha  wa 2012/2013 ikiwa na idadi ya mashauri 285 yaliyosalia kutoka miaka ya nyuma. Aidha, Mahakama ilipokea mashauri mapya 118 na hivyo kuwa na jumla ya mashauri 403. Katika kipindi cha kuanzia Julai, 2012 hadi Machi 2013 Mahakama ya Biashara imesikiliza na kuyatolea maamuzi jumla ya mashauri 74 sawa na asilimia 18ya jumla ya mashauri yote na hivyo kubaki na jumla ya mashauri 329.Aidha, uwezo wa wastani wa uondoaji wa mashauri (Clearance Rate) katika Mahakama ya Biashara kwa tathmini ya kipindi cha miezi sita iliyopita ni asilimia 64.(Jedwali Na.3)

iv.        Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, ilianza Mwaka wa Fedha wa 2012/2013 ikiwa na idadiya mashauri 1,597 yaliyosalia kutoka miaka ya nyuma. Aidha, Mahakama ilipokea mashauri mapya 674 na hivyo kuwa na jumla ya mashauri 2,271. Katika kipindi cha kuanzia Julai 2012 hadi Machi 2013 Mahakama ya Kazi imesikiliza na kuyatolea maamuzi jumla ya mashauri 491 sawa na asilimia 22 ya jumla ya mashauri yote na hivyo kubaki na jumla ya mashauri 1,780. Aidha, uwezo wastani wa uondoaji wa mashauri (Clearance Rate) katika Mahakama ya Kazi kwa tathmini ya kipindi cha miezi sita iliyopita ni asilimia 73. (Jedwali Na.4)

v.         Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, ilianza Mwaka wa Fedha wa 2012/2013 ikiwa na idadi ya mashauri 5,393 yaliyosalia kutoka miaka ya nyuma. Aidha, Mahakama ya Ardhi ilipokea mashauri mapya 427 na hivyo kuwa na jumla ya mashauri 5,820. Katika kipindi cha kuanzia Julai 2012 hadi Machi, 2013 Mahakama ya Ardhi imesikiliza na kuyatolea maamuzi jumla ya mashauri 427 sawa na asilimia 7ya jumla ya mashauri yote na hivyo kubaki na jumla ya mashauri 5,393.Aidha, uwezo wa wastani uondoaji wa mashauri (Clearance Rate) katika Mahakama ya Ardhi kwa tathmini ya kipindi cha miezi sita iliyopita ni asilimia 100.(Jedwali Na.5)

vi.        Mahakama za Hakimu Mkazi, ilianza Mwaka wa Fedha wa 2012/2013 ikiwa na idadi ya mashauri 25,002 yaliyosalia kutoka miaka ya nyuma. Aidha, Mahakama ilipokea mashauri mapya 980 na hivyo kuwa na jumla ya mashauri 25,982. Katika kipindi cha kuanzia Julai, 2012 hadi Machi 2013 Mahakama imesikiliza na kuyatolea maamuzi jumla ya mashauri 612 sawa na asilimia 2 ya jumla ya mashauri yote na hivyo kubaki na jumla ya mashauri 25,370.Aidha, uwezo wa wastani wa uondoaji wa mashauri (Clearance Rate) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kwa tathmini ya kipindi cha miezi sita iliyopita ni asilimia 73. (Jedwali Na.6)

vii.       Mahakama za Wilaya, zilianza Mwaka wa Fedha wa 2012/2013 ikiwa na idadi ya mashauri 31,025 yaliyosalia kutoka miaka ya nyuma. Aidha, Mahakama za Wilaya ilipokea mashauri mapya 94,872 na hivyo kuwa na jumla ya mashauri 125,897. Katika kipindi cha kuanzia Julai 2012 hadi Machi 2013 Mahakama za Wilaya imesikiliza na kuyatolea maamuzi jumla ya mashauri 104,359 sawa na asilimia 83 ya jumla ya mashauri yote na hivyo kubaki na jumla ya mashauri 21,538. Aidha, uwezo wa wastani wa uondoaji wa mashauri (Clearance Rate) katika Mahakama za Wilaya kwa tathmini ya kipindi cha miezi sita iliyopita ni asilimia 110.(Jedwali Na.7)


viii.  Mahakama za Mwanzo, zilianza Mwaka wa Fedha wa 2012/2013 zikiwa na idadi ya mashauri 124,959 yaliyosalia kutoka miaka ya nyuma. Aidha, Mahakama za Mwanzo zilipokea mashauri mapya 650,181 na hivyo kuwa na jumla ya mashauri 775,140. Katika kipindi cha kuanzia Julai, 2012 hadi Machi 2013 Mahakama imesikiliza na kuyatolea maamuzi jumla ya mashauri 577,425 sawa na asilimia 74 ya jumla ya mashauri yote na hivyo kubaki na jumla ya mashauri 197,715. Aidha, uwezo wa wastani wa uondoaji wa mashauri (Clearance Rate) katika Mahakama za Mwanzo kwa tathmini ya kipindi cha miezi sita iliyopita ni asilimia 89.(Jedwali Na.8)

Uendeshaji wa Mashauri nchini

9.      Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu la kuiwakilisha Serikali katika mashauri mbalimbali ndani na nje ya nchi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, imeendesha mashauri ya Jinai, Madai na Katiba katika Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu na Mahakama zilizo chini ya Mahakama Kuu isipokuwa Mahakama za Mwanzo. Aidha, Ofisi pia imeendelea kuratibu mashauri ya usuluhishi (arbitration) ambapo manne (4) ya Mahakama Kuu na 11 ya Tume ya Usuluhushi (CMA). Hadi Machi, 2013 kulikuwa na jumla ya mashauri ya madai 682yakijumuisha mashauri mapya 132.Mashauri haya yote yalifunguliwa dhidi ya Serikali na Kesi moja (1) ya Madai ilifunguliwa na Serikali.  Mashauri hayo yako katika hatua mbalimbali za kusikilizwa na kutolewa maamuzi na Mahakama (Jedwali Na.11). Mashauri ya madai yaliyohitimishwa hadi mwezi Machi, 2013 ni 40 na kubaki mashauri 642.

Aidha, kulikuwa na jumla ya Maombi ya madai 285yaliyofunguliwa yakiwemo mapya 89yaliyopokelewa katika kipindi cha Julai 2012 hadi Machi 2013. Maombi haya ya madai yalifunguliwa dhidi ya Serikali. Hadi Machi, 2013 maombi ya madai 63 yalihitimishwa na maombi 222 yanaendelea kusikilizwa. Vilevile, palikuwepo na Rufani za madai 46zikijumuisha mpya saba (7). Kati ya hizi rufani mbili (2) zilihitimishwa na kubaki na rufani 44 ambazo zinazoendelea kusikilizwa. Vilevile, kuhusu masuala ya upatanishi (arbitration) mgogoro mmoja (1) unaohusu Serikali ulishughulikiwa kati ya Mashauri yaliyobakia.

Hali kadhalika, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendelea kuendesha mashauri ya rufani za uchaguzi yatokanayo na uchaguzi Mkuu wa 2010 ambayo ni kutoka Kigoma (3), Tabora (2), Mara (1), Sumbawanga (1), Dar es Salaam (1), Mtwara (3), Kagera (1) na Arusha (2). Kati ya mashauri hayo, mashauri matano (5)yamehitimishwa na mashauri tisa (9)yanaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Rufani.

10.      Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Kurugenzi ya Mashtaka iliendelea kutekeleza jukumu lake la kuendesha mashauri ya jinai katika Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu na Mahakama zilizo chini ya Mahakama Kuu na pia iliendelea kuratibu kazi za upelelezi unaofanywa na vyombo vya upelelezi isipokuwa Mahakama za Mwanzo. Jumla ya mashauri 14,453yaliyokuwepo na mengine mapya 13,487ya Mwaka 2012/2013 yaliendelea kuendeshwa Mahakamani. Mashauri haya yanahusu kesi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mashauri yaliyohusisha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, udanganyifu na utakatishaji wa fedha haramu. Hadi mwezi Machi 2013 mashauri 5,257 yalihitimishwa na kubaki mashauri 22,683yatakayoendelea kuendeshwa katika ngazi mbalimbali za Mahakama pamoja na Mashauri mapya yatakayopokelewa (Jedwali Na. 12).

Katika uendeshaji wa mashauri yanayohusu watu wenye ulemavu wa ngozi, jumla ya matukio 60 yaliripotiwa na polisi nchi nzima. Mashauri 12 yanaendelea kusikilizwa, mashauri 14yameondolewa mahakamani na mashauri 10yameamuliwa ambapo Jamhuri imeshinda mashauri yote. Mashauri 24 yanaendelea kufanyiwa kazi.

11.      Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya upelelezi vya TAKUKURU na Jeshi la Polisi ni mshiriki mkubwa katika mapambano dhidi ya rushwa. Hadi kufikia Mwaka 2012/2013 Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imepokea jumla ya majalada 317 yaliyohusu rushwa kubwa na ubadhirifu kutoka vyombo vya upelelezi vya TAKUKURU na Jeshi la Polisi. Kati ya Majalada hayo, 95yaliandaliwa hati za Mashtaka na kupewa kibali cha kushtaki, jalada moja (1) lilifungwa na majalada 65 yalirudishwa kwa vyombo husika kwa ajili ya kufanyiwa upelelezi zaidi na majalada 156 yanaendelea kufanyiwa kazi na Divisheni ya Mashtaka.

Vilevile, katika kuhakikisha kwamba mali zilizopatikana kwa njia zisizo halali zinarejeshwa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inasimamia urejeshwaji wa mali na fedha (Asset Recovery and Forfeiture) katika mashauri mbalimbali. Katika kipindi hiki mali zilizotaifishwa ni pamoja na magari manne (4) katika mikoa ya Morogoro (1), Dar es Salaam (1) na Tanga (2) na nyumba tatu (3)pamoja na fedha Shilingi bilioni saba (7) zinazotakiwa kurejeshwa baada ya watuhumiwa watano kutiwa hatiani katika shauri la madawa ya kulevya. Watuhumiwa hao wamekata rufaa.

12.      Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2012/2013 Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendelea kuendesha mashauri 14 yanayohusu makosa ya wizi, kugushi na kutakatisha fedha ambayo yaliyobaki katika kipindi cha mwaka 2011/2012 katika Mahakama mbalimbali nchini zikiwemo Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Arusha na Nzega. Mashauri haya yanahusu takribani kiasi cha Shilingi Bilioni 48. Hadi Machi, 2013 kulikuwa na jumla ya kesi tatu (3) zilizotolewa hukumu. Kesi moja (1) yenye kuhusisha kiasi cha takriban Shilingi Bilioni moja washtakiwa waliachiwa huru lakini Jamhuri imekata rufaa na kesi mbili (2) washtakiwa wametiwa hatiani na wanatakiwa kurudisha fedha zipatazo Shilingi Milioni 960. Vilevile, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendesha mashauri yanayohusu madawa ya kulevya ambapo katika kipindi cha Julai 2012 hadi Machi 2013 kesi moja (1) ya madawa ya kulevya ilihitimishwa kwa Mahakama kuwatia hatiani watu watano kwa kila mmoja kuhukumiwa kifungo cha miaka 25.


Utenganishaji wa jukumu la Upelelezi na Mashtaka (Civilianisation of Prosecutions Service)

13.      Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2012/2013, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliendelea na utekelezaji wa Mpango wa Kutenganisha Jukumu la Upelelezi na Mashtaka (Civilianisation of Prosecutions Service) ili kuondoa tatizo la haki kuchelewa kutendeka, kesi kuchukua muda mrefu Mahakamani kwa sababu ya muda mrefu unaotumika katika upelelezi. Hatua mbalimbali ziliendelea kuchukuliwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji, uelimishaji na uenezaji wa utaratibu huu katika Mikoa na Wilaya zote za Tanzania Bara. Hatua hizi ni pamoja na kuajiri Mawakili wa Serikali na kufungua ofisi katika Mikoa mitano (5) ya Morogoro, Manyara, Kigoma, Njombe na Pwani pamoja na Wilaya za Monduli na Temeke. Hadi sasa zipo Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mikoa 22ya Tanzania Bara. Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Iringa, Singida, Dodoma, Mtwara, Lindi, Mara, Kagera, Ruvuma, Rukwa, Mwanza, Kilimanjaro, Tanga, Tabora,  Shinyanga, Morogoro, Pwani, Kigoma, Manyara na Njombe.  Aidha, lengo la kuwa na Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mikoa mitatu iliyosalia ya Geita, Simiyu na Katavi litakamilishwa katika Mwaka wa Fedha wa 2013/2014.

Hadi Machi, 2013, Divisheni ya Mashtaka ilikuwa inaendesha kesi katika Mahakama za Wilaya 22 za Makao Makuu ya Mikoa na Wilaya zilizotajwa hapo juu. Lengo ni kufikisha huduma za mashtaka karibu zaidi na wananchi. Aidha, Mpango huu wa kutenganishwa kwa shughuli za upelelezi na mashtaka umesaidia sana kupunguza idadi ya kesi zinazofunguliwa Mahakamani na msongamano wa mahabusu na wafungwa magerezani. Idadi ya Mahabusu imepungua kutoka 17,932 kwa mwezi Julai, 2012 hadi kufikia mahabusu 16,973 mwezi Machi 2013. Vilevile, idadi ya wafungwa imepungua kutoka 17,868 kwa mwezi Julai 2012 hadi kufikia wafungwa 17,497mwezi Machi, 2013.

Lakini la msingi zaidi ni kuwa, utenganishaji huu unafanywa kwa misingi ya utawala bora. Si vyema kukipa chombo kimoja cha dola madaraka ya kuhisia, kutuhumu, kukamata, kupeleleza na kushitaki bila udhibiti wa chombo kingine. Wataalam wa utawala wanasema “Regulation is the hallmark of Government” ndiyo maana kuna EWURA, TICRA, SSRA nk. Na ndani ya Serikali nako ni muhimu kuwa na utaratibu huu wa “checks and balances”. Nchi nyingi ambazo mifumo yao ya Sheria na Utawala inafanana na sisi wana utaratibu huu. Marekani mashtaka huendeshwa na Mwanasheria Mkuu kupitia “District Attorneys”. Uingereza kuna “Crown Prosecution Agency” nk. Na hapa kwetu ndiyo tuna Mwanasheria Mkuu kupitia Ofisi ya DPP.

Uimarishaji wa Utoaji wa ushauri wa Kisheria nchini

14.      Mheshimiwa Spika,  katika Mwaka wa Fedha wa 2012/2013, Wizara yangu kwa kushirikiana na Asasi zisizo za Kiserikali, iliunda kikosi kazi kwa ajili ya kufanya utafiti na kuwasilisha mapendekezo yatakayoisaidia Serikali kubuni utaratibu wa utoaji wa  huduma za msaada wa kisheria kwa watu wasio na uwezo wa kulipia  gharama za kisheria. Kikosi kazi hicho kimefanya utafiti na tayari mapendekezo ya kutunga sheria itakayoratibu utoaji wa huduma za msaada wa  kisheria kwa umma na kuwatambua watoa huduma za msaada wa kisheria kwa umma ikiwa ni pamoja na wasaidizi wa kisheria (Paralegals) yameshawasilishwa Serikalini. Taratibu za kupata Sheria hiyo zinaendelea vizuri na ni matumaini yetu kwamba Rasimu ya Sheria hii itawasilishwa katika Bunge hili tukufu katika kipindi cha Mwaka wa Fedha wa 2013/2014.

15.         Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha wa 2011/2012 Wizara yangu ilianzisha Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari.  Kamati hii imeanzishwa kutokana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Nchi Zinazozunguka/za Ukanda wa Maziwa Makuu (The International Conference on the Great Lakes Region-ICGLR).  Nchi husika zilifikia makubaliano katika Mkataba uliosainiwa na Nchi zote wanachama ya kuweka utaratibu wa kubaini viashiria vya uvunjifu wa amani na kusababisha vita katika eneo la maziwa makuu.  Tanzania imesaini “protocol for the prevention and punishment of the crimes of Genocide, war crimes, crimes against humanity and all forms of discrimination” ambayo pia yanaitaka Nchi wanachama kuanzisha Kamati za Kitaifa za Kuzuia Mauaji ya Kimbari.  Nchini Tanzania Kamati hiyo ilianzishwa mwezi Februari 2012 na Kamati hii inajukumu la kubaini dalili/viashiria vya uvunjifu wa amani ya Nchi yetu,  kuishauri Serikali pamoja na kujenga uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kuzuia uvunjifu wa Amani na mauaji na uhalifu dhidi ya binadamu nchini.  Kamati hii ya kitaifa  ina wajumbe wafuatao:-


i.           Ofisi ya Rais-Ikulu
ii.          Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
iii.         Ofisi ya Waziri Mkuu
iv.        Wizara ya Ulinzi na Jeshi laKujenga Taifa
v.         Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
vi.        Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
vii.       Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki
viii.      Wizara ya Vijana, Habari, Utamaduni na Michezo
ix.         Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
x.          Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
xi.         Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
xii.        Chuo Kikuu cha Dar es salaam
xiii.       Taasisi ya Wakfu ya Mwalimu Nyerere

Aidha, mapema mwezi Disemba, 2012, Wizara kupitia Kamati hii imefanya Mkutano na viongozi wa dini zote ambapo viongozi wa kidini walijadili nafasi yao katika kulinda na kudumisha amani nchini.  Mikutano ya Kamati hii ni endelevu na ili iwe na tija hutumika kuishauri Serikali na pia kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuzuia mauaji na uhalifu dhidi ya binadamu nchini.

16.      Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2012/2013 Wizara yangu imeratibu na kuandaa Mkutano wa Kimataifa wa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Ugaidi uliofanyika Dar es salaam kuanzia tarehe 26-28 Februari, 2013 na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka Nchi 36 duniani. Ujumbe na mada kuu katika Mkutano huo ulikuwa ni “Bringing Terrorists to Justice; Policy challenges in the Prosecution and Prevention of Terrorism”.

17.         Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha wa 2012/2013 Wizara yangu imekamilisha  tafiti kuhusu hali ya watoto wanaokinzana na Sheria na pia kuhusu upatikanaji wa haki sheria kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 kwa kushirikiana na UNICEF. Kutokana na utafiti huo, Wizara imeandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Haki Sheria kwa watoto. Mpango Mkakati huu utaboresha mfumo mzima wa upatikanaji wa ulinzi na haki kwa watoto nchini. Vilevile, Mpango Mkakati huu utasaidia kuweka pamoja mikakati ya namna bora ya kushughulikia masuala ya haki sheria kwa watoto nchini. Mpango Mkakati huu unaandaliwa Waraka wa Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kujadili na kupitisha Mpango Mkakati huu ili uweze kutumika.

18.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha wa 2012/2013 Wizara yangu imeendelea kupokea malalamiko ya aina mbalimbali toka kwa wananchi na yameshughulikiwa. Malalamiko mengi yalielekezwa kwenye Taasisi na vyombo vya Serikali vinavyojishughulisha na utoaji haki na usimamizi wa Sheria.  Malalamiko hayo yalishughulikiwa kwa kuwasiliana na vyombo/Taasisi husika kama njia ya kuyatafutia utatuzi.

19.      Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendelea kutekeleza jukumu la kuimarisha utoaji wa ushauri wa kisheria kuhusu masuala ya mikataba ya kibiashara, Kimataifa, Katiba na Haki za Binadamu. Aidha, Ofisi pia imeshiriki katika mikutano mbalimbali ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa Mataifa, Nchi wanachama wa Kusini mwa Afrika (SADC) na Nchi za Umoja wa Afrika kwa ajili ya kufanya majadiliano na kutoa ushauri wa kisheria. Majadiliano ambayo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeshiriki ni ubia wa kibiashara kati ya Umoja wa Nchi za Ulaya na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EPA); kuanzishwa kwa  Itifaki ya Umoja wa Fedha; Itifaki ya Mahakama ya Nchi  wanachama wa Kusini mwa Afrika; kuanzisha Soko Huru baina ya Nchi Wanachama wa Afrika Mashariki, SADC na COMESA; kurekebisha Mkataba wa kuanzisha Mahakama ya Umoja wa Afrika; kurekebisha Mkataba ulioanzisha Bunge la Afrika; Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kuzuia kusambaa kwa silaha ndogo; kurekebisha Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; na majadiliano ya mgogoro wa mpaka baina ya Tanzania na Malawi. Vilevile, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha wa 2012/2013 Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeshughulikia na kutoa ushauri wa kisheria katika mikataba (Contracts) 330. Kati ya Mikataba hii, mikataba 295ilihusu manunuzi ya umma na Mikataba 35ilihusu masuala ya uwekezaji. Vile vile, Mikataba ya Makubaliano (MOU) 58 ilishughulikiwa na makubaliano baina ya Nchi na Nchi (Bilateral Agreement) 21; mahudhurio ya vikao 185vilivyohusu Majadiliano ya Mikataba na Mahusiano ya Kimataifa.

Mpango wa Serikali Wazi

20.      Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza mwaka jana katika Bunge lako Tukufu, Serikali imeendelea kutelekeza Mpango wa Uendeshaji Shughuli za Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership-OGP)ambao ulianzishwa tarehe 21 Septemba, 2011. Mpango huu unasimamiwa na Wizara yangu na kuratibiwa na Kamati ya Kitaifa chini ya uenyekiti wa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu. Katika mwaka wa fedha 2012/2013 Mpango huu umeendelea kutekelezwa na Sekta tatu za kipaumbele za huduma za jamii ambazo ni Afya, Maji na Elimu. Mpango wa Serikali wazi unajikita katika maeneo ya kuweka uwazi zaidi katika uendeshaji wa shughuli za Serikali, Ushirikishwaji wa wananchi katika mpango wa utekelezaji, Uwajibikaji na Uadilifu, Utawala Bora, kupambana na Rushwa na matumizi ya teknolojia na ubunifu. Malengo ya Mpango huu ni kuimarisha usimamizi wa matumizi ya rasilimali za umma kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza usalama wa nchi na kuongezeka kwa uwajibikaji wa kitaasisi.

21.      Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Mpango huu yafuatayo yamefanyika:-

i.        Mpango Kamili wa OGP Tanzania umeandaliwa na kuwasilishwa Makao Makuu ya OGP katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa viongozi wa nchi wanachama wa OGP uliofanyika Brasilia Brazili tarehe 17-18 Aprili, 2012;
ii.       “Road Map” na Bango kitita ya “Commitments” ya shughuli zitakazotekelezwa hadi kufikia Juni, 2013 imeandaliwa na kusambazwa kwenye sekta husika;
iii.      Wizara nane (8) zimeandaa Mipango Kazi yao na kuiwasilisha kwenye Kamati. Wizara hizi ni Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais Tume ya Mipango, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Maji, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Fedha
Aidha, kwa hivi sasa Kamati imeandaa Mkakati wa Mawasiliano kuhusu utekelezaji wa Mpango wa OGP Tanzania (Open Government Partnership Communication Strategy) na vile vile Kamati inashirikiana  kwa karibu na Wakala wa Serikali Mtandao (e-Government Agency) kuhakikisha Tovuti ya wananchi (Citizen Portal) inaanza kazi mapema iwezekanavyo ili iweze kuhudumia wananchi. Aidha, Waraka wa Mapendekezo ya Kutunga Sheria ya Uhuru wa Habari (Freedom of Information Law) unaandaliwa na Wizara husika ambayo ndiyo yenye dhamana ya masuala ya habari nchini, na utawasilishwa kwenye ngazi za maamuzi na hatimaye sheria kutungwa na  kuletwa katika Bunge lako Tukufu.
iv.      Kuhudhuria kikao cha Mawaziri wa Nchi zinazotekeleza Mpango wa Serikali Wazi (OGP) kilichofanyika Mjini London kuanzia tarehe 22-25/04/2013.
22.      Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2013/2014 Wizara yangu itaendelea kusimamia Mipango Kazi ya Sekta za kipaumbele zinatekelezwa kwa kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoendelea kujitokeza katika utekelezaji wa Mpango wa Serikali Wazi.

Utafiti na Mapitio ya Sheria

23.      Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imekamilisha Taarifa ya Mfumo wa Haki za Madai (Civil Justice System Review) na Taarifa ya Mapitio ya Tamko la Sheria za Mila zinazofuata mkondo wa ukoo wa mama (Matrilineal Societies). Taarifa hizi zimewasilishwa kwangu ili ziweze kufanyiwa kazi zaidi na Mwanashera Mkuu wa Serikali na kutolewa kauli Bungeni ya hatua zitazochukuliwa. Tume iko katika hatua za mwisho za kukamilisha Taarifa ya Mapitio ya Sheria zinazosimamia Usuluhishi na Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi. Aidha, Rasimu ya Awali ya Mapitio ya Mfumo wa Sheria zinazosimamia Huduma za Jamii kwa Wazee imeandaliwa ili kuwezesha kufanya utafiti katika Mikoa 12 ya Tanzania ambayo ni Kagera, Shinyanga, Mara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Dodoma, Mbeya, Rukwa Ruvuma na Pwani. Kwa upande wa Mapitio ya Mfumo wa Sheria unaosimamia Haki za Walaji (Consumer Protection), taratibu za kumpata Mshauri Mwelekezi zimeanza.

24.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2012 hadi Machi 2013 Tume imefanya uchambuzi wa hukumu za kesi za Mahakama ya Rufani ya Tanzania zipatazo 100 ili kuainisha misingi ya Kisheria (Legal Principles) na kuweka misingi hiyo katika tovuti yake ili kuwarahisishia wadau kuelewa tafsiri ya maamuzi ya Mahakama ya Rufani kuhusu vipengele vya kisheria vilivyotumika. Vilevile Tume imewasilisha kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Rasimu tano (5) za tafsiri za Sheria katika lugha ya Kiswahili (Kiambatisho ‘E’).  Pia Tume imeendelea kutoa elimu ya Sheria kwa umma kupitia vipindi vya Redio na runinga kwa lengo la kuelimisha jamii kuhusu haki, wajibu na masuala mbalimbali ya Kisheria.

Uandishi wa Sheria na Hati Mbalimbali

25.      Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2012/2013 Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, iliendelea kutekeleza jukumu la kuandaa Miswada ya Sheria na kuiwasilisha mbele ya Bunge kwa ajili ya kujadiliwa na hatimaye kupitishwa na kuwa Sheria za Nchi. Hadi mwezi Machi, 2013 jumla ya Miswada sita(6) iliandaliwa kati ya hiyo, Miswada minne (4) ilipitishwa na kuwa Sheria, miswada miwili (2) bado haijapitishwa. Aidha, kazi ya kuzifanyia urekebu Sheria zilizopitishwa na Bunge iliendelea kufanyika ambapo Sheria 14 zilifanyiwa urekebu, jumla ya Sheria Ndogo 260 zilitayarishwa na kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali na Maazimio 11 yaliwasilishwa Bungeni. (Jedwali Na.13).

Vilevile, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilitekeleza jukumu la kutafsiri Sheria kwa lugha ya kiswahili na kiingereza. Kwa mwaka wa Fedha wa 2012/2013 Ofisi imetafsiri jumla ya Sheria saba (7)katika lugha ya Kiswahili. (Kiambatisho ‘B’).

Usimamiaji wa Haki za Binadamu, Utawala Bora na Masuala ya Katiba

26.       Mheshimiwa Spika, kwa upande wa masuala ya Katiba na Haki za Binadamu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilipokea maombi ya mashauri ya Kikatiba na Haki za Binadamu 73 na kuhitimishwa 17. Hivyo kubaki mashauri 56yanayoendelea kusikilizwa. (Jedwali Na.14)Aidha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliweza kushiriki vikao mbalimbali kuhusiana na masuala ya haki za binadamu kama vile, Kikao cha Kamati ya Haki za Binadamu inayosimamia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni ambapo Taarifa ya Nchi ya Mkataba huo ilijadiliwa Novemba, 2012 huko Geneva, Uswisi; Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Marekani; na Kikao cha Tume ya Haki za Binadamu na Watu (African Commission on Human and People’s Rights) kilichofanyika Gambia April, 2013.

Vilevile, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeshiriki kwenye wiki ya Maadhimisho ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ambayo hufikia kilele chake tarehe 10 Desemba kila mwaka kwa kushirikiana na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Wizara ya Katiba na Sheria. Katika maadhimisho hayo taarifa mbalimbali za Nchi kuhusu Haki za Binadamu na mapendekezo yanayotolewa na Kamati au Tume zinazosimamia Mikataba husika ya Kimataifa ya Haki za Binadamu kuhusu Tanzania zilitolewa kwa wananchi. Madhumuni ya maadhimisho hayo yalikuwa ni kuwawezesha wananchi kufahamu hali halisi ya Kitaifa katika masuala ya Haki za Binadamu na jinsi Tanzania inavyotekeleza shughuli za kulinda na kukuza Haki za Binadamu.

27.      Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa fedha wa 2012/2013, Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ilipanga kudumisha Utawala Bora nchini kwa kusimamia Utekelezaji wa Haki za Binadamu kama zilivyoelezwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Tamko la Umoja wa Mataifa na Tamko la Afrika la Haki za Binadamu. Katika kutekeleza hili Tume imekamilisha kuandaa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu ambao umewasilishwa Serikalini kwa ajili ya Kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri. Aidha, Tume iliendelea kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa kupokea na kufuatilia malalamiko, kutoa ushauri wa kisheria, kufanya uchunguzi na utafiti juu ya masuala yanayohusu haki za binadamu na utawala bora.

28.      Mheshimiwa Spika, Tume iliendelea kupokea na kushughulikia malalamiko mapya na ya zamani kulingana na uwezo uliokuwepo. Hadi kufikia mwezi Machi, 2013 Tume ilikuwa imeshughulikia jumla ya malalamiko 8,350. Kati ya malalamiko hayo 7,165 ni ya miaka ya nyuma na 1,185 ni mapya. Kati ya Malalamiko hayo 688 yalihitimishwa baada ya kupatiwa ufumbuzi na kubakia na malalamiko 7,662 yanayoendelea kushughulikiwa. (Jedwali Na.9)

29.      Mheshimiwa Spika, Tume iliongeza juhudi za kuleta ufumbuzi wa malalamiko ya wananchi na migogoro ya ardhi. Vilevile, Tume ilikamilisha uchunguzi na kutoa mapendekezo kwa mamlaka husika kuhusu ukiukwaji wa haki za watumishi wa mamlaka ya Maji Safi na Taka (DAWASCO), Mgogoro kati ya wafugaji na wakulima wa Wilaya ya Rufiji, na Mgogoro wa Ardhi Mabwepande, Wilaya ya  Kinondoni. Aidha, Tume iliitisha na kuendesha vikao vya kujadili taarifa za uchunguzi wa hadharani kuhusu migogoro ya ardhi na uhamishwaji wa watu katika ardhi yao ulioshirikisha wadau mbalimbali kutoka Taasisi za     Serikali na Binafsi. Vile vile Tume ilifanya kaguzi katika vituo 100vya vizuizi (detention facilities) katika Wilaya 21 ili kupima na kutathimini hali na haki za watoto waliozuiwa katika vituo hivyo.

30.      Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imetoa elimu kwa umma kuhusu haki za bindamu na utawala bora kupitia vipindi vya redio, luninga na machapisho mbalimbali. Jumla ya machapisho 38,250yalisambazwa na wananchi 1,594 walipatiwa ushauri wa kisheria. Aidha, tume ilitoa mafunzo kwa waandishi wa habari 112 katika Mikoa sita (6) ya Tanzania bara ya Iringa, Dodoma, Lindi, Morogoro, Mwanza, Tanga na Mjini Magharibi kwa upande wa Zanzibar.

Uimarishaji wa Shughuli za Usajili, Ufilisi na Udhamini

31.      Mheshimiwa Spika, Wakala wa Usajili,Ufilisi na Udhamini umeanza mazungumzo na wadau wa usajili wa watoto ambao ni Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI juu ya namna ya kuboresha shughuli za Usajili wa Watoto. Rasimu ya Mkataba wa Makubaliano kati ya RITA,  Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuhusu namna ya kusogeza huduma za  usajili wa vizazi na vifo kufikia ngazi ya kata imekamilika,  na rasimu hiyo inatarajiwa  kujadiliwa katika kikao cha Wadau kitakachofanyika tarehe 3 Mei, 2013.

Utekelezaji wa mpango wa kusajili watoto chini ya umri wa miaka Mitano unaojulikana kama “U5BRI – Under 5 Birth Registration Initiative” ulianza kwa majaribio kwa kipindi cha wiki sita yaliyofanyika kuanzia tarehe 4 Juni, 2012 katika Manispaa ya Temeke. Jumla ya watoto 15,513 walio na umri wa chini ya miaka mitano walisajiliwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa.  Wakala unaendelea kutekeleza Mpango  huo ambao ni mkakati wa kupunguza mlundikano wa vizazi ambavyo havijasajiliwa. Maandalizi ya kueneza mpango/mkakati huu yamefanyika katika Wilaya zote za Mkoa wa Mbeya kwa kufanya utafiti wa awali (Baseline Survey) na kutoa hamasa kwa makundi mbalimbali ya viongozi kama vile kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya, vikao vya Madiwani na Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya. Utekelezaji wa Mkakati  huu unatarajiwa kuanza mwezi Juni, 2013.

Sanjari na Mkakati huo wa kusajili watoto walio na umri chini ya miaka mitano, Wakala pia unatekeleza Mkakati wa kusajili watoto wa umri kati ya miaka 6 hadi 18 (6-18 Birth Registration Initiative) waliopo mashuleni ambao umefanyiwa majaribio katika Wilaya ya Igunga. Katika majaribio hayo jumla ya watoto 1,499 walisajiliwa katika kipindi cha miezi miwili kuanzia tarehe 18 Februari, 2013 na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa.

32.      Mheshimiwa Spika, Wakala wa RITA umeendelea kusogeza huduma za usajili kwa wananchi, kwa kuendesha kampeni za uhamasishaji ambazo zilipelekea kusajili vizazi 331,272, vifo 59,099, ndoa 6,094, talaka 42, uasili wa Watoto 23 na kufunga mirathi mmoja, kuandika na kuhifadhi wosia 37.

33.      Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu ya Ufilisi Wakala pia uliteuliwa na Mahakama kuwa mfilisi wa muda ili kusimamia mali za kampuni ya mitambo ya kufua Umeme ya IPTL. Katika shauri namba 49 la mwaka 2003 lillilohusu IPTL. Mahakama ya Rufani ilitoa maamuzi ya kufuta amri ya kuifilisi IPTL iliyotolewa tarehe 17 Disemba, 2012, hivyo Wakala kubaki na jukumu la kuwa Mfilisi wa muda (Provisional Liquidator) wa Kampuni hiyo hadi shauri hilo litakapomalizika.

34.      Mheshimiwa Spika, katika masuala ya Udhamini, Wakala unajukumu la kusimamia mali zisizokuwa na uangalizi maalumu, mali zisizokuwa na mwenyewe na zile zinazopaswa kumilikiwa na watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ambao hawana waangalizi maalum (Guardians) kwa mujibu wa Sheria ya Mdhamini wa Serikali ambapo Wakala (Administrator General) huteuliwa na Mahakama kama Mdhamini wa Serikali (Public Trustee).

Pia, Wakala husimamia mirathi baada ya kuombwa na ndugu wa marehemu au kuteuliwa na Mahakama. Shughuli nyingine inayofanyika ni kusajili Miunganisho ya Wadhamini ili kuwapatia nguvu ya kisheria ya kumiliki mali kwa niaba ya Taasisi zao. Wadhamini wa Taasisi za kijamii, kidini, mifuko ya maendeleo ya kijamii, vilabu vya michezo pamoja na vyama vya siasa husajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Muunganisho wa Wadhamini, Sura ya 318 toleo la 2002. Hadi kufikia Machi, 2013, Wakala umesajili Miunganisho ya Udhamini 204 na kutoa elimu kwa madhehebu ya dini mbalimbali na kutoa hati za usajili kwa Wadhamini wa Vyama vya Siasa, Vikundi, Makanisa, Misikiti na Mali zipatazo151. (Jedwali na 10). Pia, Wakala imetembelea vikundi vya Udhamini katika Wilaya ya Morogoro, Iringa na Arusha.

35.      Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuboresha mazingira ya kazi Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini unaendelea na ujenzi wa Jengo la Makao Makuu ya Ofisi za Wakala lililopo katika Mtaa wa Makunganya mjini Dar es Salaam ambao unatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha wa 2013/2014.


Uimarishaji wa Vyuo vya Mafunzo ya Sheria

36.      Mheshimiwa Spika, katika kuiimarisha Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (Law School of Tanzania), Wizara yangu kupitia Programu ya Maboresho ya Sekta ya Sheria (Legal Sector Reform Programme) imekamilisha ujenzi wa majengo ya kudumu ya Taasisi hii katika kiwanja Na. 2005/2/1 Sam Nujoma/Mpakani, Sinza, Dar Es Salaam.  Jumla ya Shilingi bilioni 16.1zilitumika katika ujenzi huo.  Kwa sasa Taasisi hii inaendesha mafunzo katika majengo hayo baada ya kuhamia hapo Agosti 2012.  Kukamilika kwa majengo hayo kutaiwezesha Taasisi hii kuongeza udahili wa wanafunzi kufikia 1,500 kwa mwaka.

37.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2012 – Februari 2013 Taasisi hii ilidahili wanafunzi wapya 736. Aidha, Taasisi hii imetoa mafunzo ya Uanasheria Kwa Vitendo kwa wanafunzi 585waliosajiliwa katika Mwaka wa Fedha wa 2011/12 ambao walikuwa wanaendelea na mafunzo.  Katika kipindi hicho jumla ya wanafunzi 1,136 walifanya mitihani ya mwisho na wanafunzi 409 walifaulu mitihani hiyo na kupata sifa ya kusajiliwa kuwa Mawakili wa Kujitegemea. Wanafunzi 861 walitakiwa kurudia mitihani mbalimbali (supplementary examinations) ya kukamilisha mafunzo yao wakati wanafunzi 43 walishindwa mitihani.

38.      Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa fedha kupitia Wizara yangu kwa ajili ya kuwapa ruzuku wanafunzi wahitaji wa Taasisi hii kwa ajili ya kugharamia mafunzo. Tangu Julai 2012 hadi sasa, jumla ya Shilingi 2,232,558,500.00 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya ruzuku kwa wanafunzi hao. Aidha mchakato wa kurejea Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Mwaka 2004 umeanza ambapo suala la Mikopo kwa Wanafunzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo yamezingatiwa.

39.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2012 hadi Februari 2013, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (Institute of Judicial Administration) kilidahili wanafunzi 551 wa Mwaka wa Kwanza wa Stashahada ya Sheria na wanafunzi 634 wa Cheti cha Sheria. Kulikuwa na wanafunzi 273 wa Mwaka wa Pili wa Stashahada ya Sheria waliokuwa wanaendelea na mafunzo. Jumla ya wanafunzi 706 walihitimu mafunzo ambapo 223 walitunukiwa Stashahada ya Sheria na 483 walitunukiwa Cheti cha Sheria. Aidha, Chuo kiliendesha mafunzo ya awali (Induction Course) kwa ajili ya Mahakimu Wakazi wapya 290 waliokuwa wameajiriwa kufanya kazi katika Mahakama za Mwanzo sehemu mbalimbali hapa nchini. Mafunzo hayo ni sehemu ya Mpango Mkakati wa Chuo ya kuanzisha na kuendesha mafunzo mahsusi na endelevu kwa Majaji, Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama ya Tanzania. Vile vile, Chuo kimefikia asilimia 50 ya ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kiume 300linalotarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2013.

Habari, Elimu na Mawasiliano kwa Jamii

40.         Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inahakikisha uboreshaji wa mfumo wa teknolojia ya habari, elimu na mawasiliano unapewa umuhimu wa kutosha. Katika kutekeleza azma hiyo, hatua ya kuunganisha kwenye Mfumo mmoja wa mawasiliano (WAN) Makao makuu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Divisheni ya Mashtaka na Kanda ya Dar es Salaam imeanza. Katika kutekeleza hili usimikaji wa LAN (Local Area Network) ambayo ni ya kisasa yenye uwezo wa kusafirisha na kupokea sauti, picha na takwimu imeanza kufungwa Makao Makuu.   Lengo ni kurahisisha, kuboresha mawasiliano na kuongeza ufanisi wa kazi. Aidha, Tovuti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (www.agctz.go.tz ) imeendelea kufanya kazi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa mbalimbali kwa jamii. Pia, “Software” ya kutunza kumbukumbu za vitabu vya maktaba imekamilika na imeanza kutumika.
Vilevile, Ofisi imeendelea kutoa elimu kwa umma kwa njia mbalimbali ikiwemo kushiriki katika vipindi vya redio na luninga juu ya masuala ya Katiba na Haki za Binadamu, mikataba, uandishi wa sheria, uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi, masuala ya haki jinai pamoja na majukumu ya Ofisi kwa ujumla.

41.      Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaendelea kuandaa mtandao wa kompyuta ujulikanao kama “Case Docket Management System” utakaowezesha utunzaji wa nyaraka mbalimbali za mashauri nchini. Mfumo huu utakapokamilika utaimarisha upatikanaji wa takwimu za kesi na masuala mengine ya uendeshaji mashauri. Ofisi pia ipo katika hatua za usimikaji wa mfumo wa eletroniki kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu za uendeshaji mashauri katika ofisi zote za mikoa baada ya kazi ya kufunga mfumo kukamilika katika makao makuu na mkoa wa Dar es Salaam.

42.      Mheshimiwa Spika, Wizara pia imekamilisha usimikaji wa mfumo wa kuhifadhi kumbukumbu (Data Center) ambao lengo lake ni kuunganisha mifumo ya utunzaji kumbukumbu za Taasisi zilizo chini ya Wizara. Sambamba na uimarishaji wa mifumo ya teknolojia, Wizara iliendelea na jukumu la kutoa elimu kwa umma kwa njia ya vipindi vya redio na luninga kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu utoaji na usimamizi wa haki. Vilevile, Wizara imeingia Mkataba wa makubaliano na Kampuni Tanzu ya Serikali ya China ya ZTE Corporation ili kufanya upembuzi yakinifu wa kusimika mfumo wa “e-justice”katika Mahakama na Magereza ili kurahisisha usikilizaji wa Kesi. Upembuzi huo yakinifu umekwishaanza na unaendelea kufanyika. Mpango huu wa kusikiliza kesi kwa kutumia mfumo maalum wa “e-justice” ilikuwa ni ahadi yangu wakati nikiwasilisha bajeti ya mwaka 2012/2013 bungeni. Utaratibu wa kutekeleza Mradi huu unaendelea kwa kuratibiwa na Wizara yangu.
                        
Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo

43.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka 2012/2013 Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa Ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UNDP) iliwajengea uwezo wa kitaalamu Mawakili kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wanasheria na wataalam wengine walio katika Wizara mbalimbalina Idara za Serikali. Mafunzo haya yalihusu nyanja za kujadili, kuandika na kuhakiki mikataba kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa hatua zote za majadiliano ya mikataba ili kuweza kubaini matatizo kabla ya mikataba kusainiwa na hatimaye kuwa na mikataba yenye maslahi kwa Taifa. Vilevile, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inatekeleza Mradi wa Kujenga Uwezo katika mapambano dhidi ya rushwa (STACA). Kazi zilizofanyika kwa Mwaka 2012/2013 kutokana na mradi huu ni kufanya mapitio ya Sheria mbalimbali zinazokinzana, kufanya mapitio ya mafaili ya kesi za rushwa kwa kuzitolea ushauri, maandalizi ya Hadidu za Rejea kwa ajili ya kupata mtaalam mwelekezi wa kutengeneza mwongozo wa maadili kwa waendesha mashtaka na kuandaa majarida (journals) mbalimbali ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

44.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea na jukumu la kuratibu na kutekeleza Programu ya Maboresho ya Sekta ya Sheria kwa Taasisi zilizo chini ya Sekta ya Sheria ambazo ni Mahakama ya Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo, Tume ya Haki za binadamu na Utawala Bora na Sekretarieti inayoratibu huduma ya msaada wa Kisheria (Legal Aid Secretariet).

45.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai hadi Februari 2013 Programu imetekeleza kazi zifuatazo; Kukamilisha ujenzi wa majengo ya kudumu ya Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (Law School of Tanzania); Kuendesha mafunzo ya Jinsia kwa Watumishi toka Taasisi zinazotekeleza Programu kwa lengo la kupata wakufunzi watakaoendelea kutoa mafunzo haya ndani ya Taasisi husika; na kutayarisha andiko la mchakato wa kuandaa Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria. Aidha, wahisani wamekubali kuongeza kipindi cha utekelezaji wa Programu hii kwa mwaka mmoja zaidi hadi Juni, 2014 ili kukamilisha malengo yaliyochelewa kufikiwa. Programu ya Maboresho ya Sekta ya Sheria ilipaswa kuisha Juni, 2013.

Uboreshaji wa Mazingira ya Kazi na Ujenzi wa Majengo

46.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Mahakama ya Tanzania imekarabati na kujenga Mahakama kama ifuatavyo;-

i.        Ukarabati wa jengo la Mahakama Kuu Dar es salaam na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu unaendelea;
ii.       Ujenzi wa mabweni ya chuo cha Mahakama Lushoto unaendelea;
iii.      Ujenzi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi uko katika hatua ya mwisho ambapo inategemewa kukamilika mwezi juni, 2013;
iv.     Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Kisarawe umekamilika;
v.      Ujenzi wa Mahakama Kuu Bukoba umekamilika na awamu ya pili ya ujenzi wa jengo la Mahakama Kuu Shinyanga unaendelea;
vi.     Magari 33yamenunuliwa yakiwemo magari 32 ya Waheshimiwa Majaji na basi moja (1)kwa ajili ya watumishi wa Wizara.        

Maendeleo na Ustawi Wa Watumishi

47.      Mheshimiwa Spika, katika kuleta ufanisi na tija kazini jumla ya watumishi 579wa Wizara na Taasisi zake wamepatiwa mafunzo ya muda mrefu na mfupi katika fani mbalimbali, nje na ndani ya nchi ikiwa ni pamoja na mafunzo kazini (on job training). Watumishi 13 wamepandishwa vyeo na watumishi 15 walihudhuria  mikutano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kuiwakilisha Wizara katika masuala mbalimbali. Aidha, Tume ya Utumishi wa Mahakama hadi kufikia mwezi Februari, 2013 imefanya vikao viwili (2) vya kawaida na vikao viwili (2) vya dharura ambapo watumishi 17 waliajiriwa  katika masharti ya kudumu na malipo ya pensheni; Mahakimu 98 walithibitishwa katika cheo pamoja na kuthibitisha kazini Hakimu mmoja (1). Tume kupitia vikao hivyo ilishughulikia masuala saba (7) ya kinidhamu ambapo sita walirejeshwa kazini na mmoja (1)alifukuzwa kazi.

48.      Mheshimiwa Spika, Tume ya Utumishi wa Mahakama ilikamilisha mchakato wa kumpata Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Msajili Mkuu wa Mahakama, Msajili wa Mahakama ya Rufani na Msajili wa Mahakama Kuu. Tume pia ilifanya ziara Katika Mikoa ya Mwanza, Mara, na Kagera kwa lengo la kutoa elimu kwa watumishi wa Mahakama na Kamati za Maadili za Mikoa na za Wilaya kuhusu utendaji wake. Aidha, Tume imekagua Kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya katika Mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Manyara, Dodoma, Morogoro na Pwani. Lengo la ukaguzi huu ni kufuatilia uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa.

C.         CHANGAMOTO

49.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kutekeleza Majukumu yake ya msingi na kupata mafanikio mbalimbali. Hata hivyo Wizara pia imeendelea kukabiliwa na changamoto. Baadhi ya Changamoto hizi ni kama ifuatavyo:-
(i)       Baadhi ya Taasisi kukosa Ofisi zake za kudumu na hivyo kutumia gharama kubwa kwa ajili ya kulipia pango;
(ii)      Bajeti inayotengwa kwenye Wizara na Taasisi zake imeendelea kuwa pungufu ikilinganishwa na mahitaji halisi ya kutekeleza        majukumu ya           Wizara ambayo yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka;
(iii)     Wizara inakabiliwa na upungufu wa rasilimali watu katika Taasisi zake, hali ambayo inaathiri ufanisi wa utoaji haki kwa wananchi; 
(iv)     Baadhi ya wananchi kukosa imani na vyombo vya utoaji haki kutokana na baadhi ya watumishi wasio waadilifu kuendelea kulalamikiwa kwa kujihusisha na Vitendo vya Rushwa;
(v)      Suala la Mikopo kwa wanafunzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo limekuwa tatizo kubwa kwa Wizara na kwa wanafunzi husika ambao ni wahitimu  wa Shahada ya Kwanza. Hali hii inatokana na Sheria ya Bodi ya Mikopo inayowaruhusu wanafunzi wa Shahada ya Kwanza “undergraduate” peke yake kupata mikopo hiyo;
(vi)     Uwezo na uelewa mdogo wa wananchi walio wengi kutumia vyombo vya kutoa haki na huduma za Kisheria kuhusu mfumo uliopo wa Sheria; na
(vii)    Mazingira ya kazi yasiyoridhisha kwa watumishi walio wengi yanayotokana na maslahi duni na uhaba wa vitendea kazi ikiwa ni pamoja na vyombo vya usafiri.


D.   MIKAKATI YA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO

50.      Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuzipatia ufumbuzi changamoto nilizozielezea, Wizara pamoja na Taasisi inaendelea kuchukua hatua zifuatazo:-

(i)         Kuendelea kuomba na kufuatilia vibali ili kujaza nafasi zilizo wazi katika Muundo na kurejea Miundo ili itosheleze mahitaji ya Taasisi kwa kushirikiana  na Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma;
(ii)        Kuboresha mazingira ya kazi kwa kujenga na kukarabati Majengo ya Mahakama na ofisi za Wizara na Taasisi;
(iii)       Kuendelea kuainisha vipaumbele vya Wizara na Taasisi zake na kujenga hoja ya kuongezewa Bajeti kulingana na uwezo wa Serikali;
(iv)       Kuwajengea watumishi uwezo na ujuzi wa taaluma zao;
(v)        Kuimarisha uwajibikaji na uadilifu kwa kusimamia vyema Sheria, Kanuni , Taratibu na Miongozo ya utekelezaji wa majukumu;
(vi)       Kufanya mawasiliano na Uongozi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na kupendekeza Marekebisho ya Sheria iliyoanzisha Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo ya Mwaka 2007 kufanyika ili kulipatia ufumbuzi tatizo la Mikopo kwa Wanafunzi wenye Shahada ya Kwanza ya Sheria;
(vii)      Kuendelea kutoa elimu ya Sheria na kusogeza huduma za Kisheria kwa wananchi; na
(viii)     Kuongeza idadi ya Mawakili wa Serikali, Majaji, Mahakimu na watumishi wa kada nyingine ili kuongeza kasi ya uendeshaji wa mashauri mbalimbali nchini.Lengo ni kulipatia ufumbuzi suala la mlundikano wa mashauri mahakamani na msongamano wa Mahabusu na Wafungwa Magerezani.

E.          MPANGO NA MALENGO YA MWAKA 2013/2014

51.      Mheshimiwa Spika, baada ya kuelezea utekelezaji wa majukumu ya Wizara yangu kwa Mwaka wa Fedha wa 2012/2013, sasa napenda  kulielezea Bunge lako Tukufu Mpango na Malengo ya Wizara yangu kwa Mwaka 2013/2014 kama ifuatavyo:

              i.  Kutoa elimu na habari kuhusu utoaji wa haki kwa jamii;
             ii.  Kuimarisha utoaji wa huduma za Kisheria;
            iii.  Kuhakiki na kushiriki majadiliano ya mikataba mbalimbali;
           iv.  Kuboresha miundombinu ya utoaji haki;
            v.  Kusikiliza na kuendesha Mashauri nchini;
           vi.  Kufanya tafiti na tafasiri za Sheria;
          vii.  Uandishi wa Sheria na Hati za Serikali;
         viii.  Kuimarisha Taasisi za Mafunzo ya Sheria;
           ix.  Kuimarisha shughuli za Usajili, Ufilisi na Udhamini;
            x.  Kuimarisha Haki za Binadamu na Utawala Bora;
           xi.  Kuratibu mchakato wa Mabadiliko ya Katiba;
          xii.  Uratibu na utekelezaji wa Programu ya Maboresho ya Sekta ya Sheria na miradi ya maendeleo; na
         xiii.  Kuimarisha Usimamizi na Uwajibikaji katika rasilimali.

52.      Mheshimiwa Spika, katika  Mwaka 2013/2014 Wizara itatekeleza Mpango na Malengo yake ambayo yamezingatia maelekezo yaliyotolewa na Serikali katika Mwongozo wake wa Utayarishaji Mpango na Bajeti kwa kuzingatia Vipaumbele  vya Taifa na Kisekta vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa  Miaka Mitano na Mpango wa Pili wa Mwaka Mmoja mmoja, MKUKUTA II na Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2010 – 2015).  Wizara ya Katiba na Sheria ikiwa moja ya Wizara zilizo chini ya Nguzo ya Tatu ya MKUKUTA II ya Utawala Bora na Uwajibikaji, mkazo na msukumo utawekwa katika kuhakikisha kunakuwa na rasilimali za kutosha na mikakati ya utekelezaji wa mpango vinawekwa ili kuimarisha utawala bora, utawala wa sheria na uwajibikaji katika kusimamia matumizi ya rasilimali na upatikanaji wa haki kwa wakati ikiwa ni pamoja na kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba kwa ufanisi.

Aidha, Mpango na Malengo ya Wizara yangu yamelenga kutoa kipaumbele cha kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi kwa kuendelea kuimarisha na kujenga miundombinu muhimu ya utoaji haki, kujenga uwezo wa watumishi na kuongeza vitendea kazi katika Sekta ya Sheria. Malengo yafuatayo yatatekelezwa:-

Kutoa elimu, habari na mawasiliano ya utoaji haki kwa jamii

53.         Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itaendelea Kuboresha Mfumo wa matumizi ya TEHAMA katika usikilizaji wa mashauri na utunzaji kumbukumbu pamoja na Takwimu mbalimbali. Hivyo, kwa Mwaka wa Fedha wa 2013/2014 Wizara itatekeleza yafuatayo:-

i.        Kuendelea kupanua mtandao wa kielektroniki kwa ajili ya kusikiliza/kuendesha Mashauri na shughuli mbalimbali za kiofisi;
ii.       Kuandaa Sera na Mkakati wa TEHAMA kwa Wizara na Mahakama;
iii.      Kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu kwa kutumia mtandao wa kompyuta;
iv.      Kuongeza matumizi ya kompyuta katika shughuli mbalimbali za kiofisi;
v.       Kuimarisha mafunzo yaujuzi wa TEHAMA; na
vi.      Kutayarisha programu mbalimbali zitakazojadiliwa kwenye vyombo vya habari kwa ajili ya kuelimisha umma kuhusu masuala ya Sheria, haki za binadamu na utawala bora na majukumu ya Wizara pamoja na Taasisi zake kwa ujumla.

Kuimarisha utoaji wa huduma za Kisheria

54.      Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea na mchakato wa kutunga Sheria itakayoratibu Utoaji wa Huduma za Kisheria kwa Umma na  kutambua watoa huduma za msaada wa Kisheria kwa umma ikiwa ni pamoja na wasaidizi wa kisheria (Paralegals). Aidha, Wizara itendelea kupokea na kushughulikia malalamiko mbalimbali toka kwa wananchi yanayohusu upatikanaji wa haki zao.


Kuhakiki na kushiriki majadiliano ya mikataba mbalimbali

55.      Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itahakikisha kuwa maslahi ya taifa yanapewa kipaumble katika mashirikiano ya kitaifa, kikanda na kimataifa. Aidha, mashirikiano haya yanakuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya wananchi kwa ujumla. Katika kutekeleza lengo hili, ofisi imepanga kutekeleza shughuli zifuatazo:-

(i)       Kushiriki katika masuala ya Mtangamano wa Kikanda kwa maslahi ya taifa;

(ii)        Kutoa ushauri wa kisheria na kufanya majadiliano ya mikataba ya kibiashara na mikataba ya mahusiano ya kikanda na kimataifa (Contracts & Treaties);

(iii)       Kuimarisha uwezo wa kutayarisha taarifa mbalimbali zinazojadiliwa katika mikutano ya kikanda na kimataifa;

(iv)       Kushiriki katika mikutano ya Kamati mbalimbali za uanachama wa vyombo mbalimbali vinavyohusika na uendeshaji wa mashauri ya jinai, madai, kikatiba na haki za binadamu.



Kuboresha Miundombinu ya Utoaji Haki

56.      Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka 2013/2014 Wizara yangu kupitia Mahakama imepanga kuendelea na ujenzi wa Mahakama Kuu ya Shinyanga na kuanza ujenzi wa Mahakama kuu katika mikoa ya Kigoma, Mara, Lindi na Morogoro. Aidha, Kanda maalum ya Mahakama Kuu Ilala na baadaye Temeke na Kinondoni zitaanzishwa ili kuweza kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

57.         Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mazingira ya kazi Mahakama itaanza ujenzi wa nyumba za Majaji katika Mkoa wa Dar es Salaam na pia kuboresha masjala za Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo kwa kuanzia na zile zilizoko mijini.
Aidha, Mahakama pia itafanya upanuzi wa jengo la Mahakama Kuu Dodoma na kuanza ujenzi wa Mahakama za Mwanzo za Bunda, Ludewa, Bariadi, Kawe, Mkomazi, Mailimoja, Lukuledi, Gairo, Mangaka na Nyamikoma.

58.      Mheshimiwa Spika, Mahakama pia ipo katika hatua za awali za kuanzisha Programu maalum ya ujenzi wa Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI, Mikoa, Wilaya na Halmashauri husika. Ni matumaini yangu makubwa kuwa Programu hiyo itasaidia katika kufanikisha lengo kuu la Wizara la kusogeza huduma karibu na wananchi.

59.      Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kuimarisha Ofisi mpya zilizoanzishwa katika Mikoa na Wilaya kwa kuzijengea uwezo wa kuendesha mashauri mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika utoaji haki kwa ujumla. Aidha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itafungua Ofisi mpya katika Mikoa ya Geita, Simiyu, Katavi na Ofisi moja (1) katika Wilaya ya Tarime. Vilevile, Wizara itafanya ukarabati wa jengo la Ofisi za Wizara (Makao Makuu) na kukamilisha ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya RITA. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora itaendelea kuimarisha Ofisi zake za kanda na itaanzisha Ofisi nyingine za kanda za Kilimanjaro, Mbeya na Dodoma.



Kusikiliza na kuendesha Mashauri nchini

60.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itaendelea kusikiliza na kuyatolea maamuzi mashauri katika ngazi mbalimbali za Mahakama, kupitia Programu maalum ya kumaliza mlundikano wa mashauri ya nyuma 1,918 yaliyoko Mahakama ya Rufani, 12,093 Mahakama Kuu, 329 yaliyoko Mahakama Kuu – Divisheni ya Biashara, 1,780yaliyoko Mahakama Kuu- Divisheni ya Kazi, 5,393yaliyoko Mahakama Kuu – Divisheni ya Ardhi, 25,370 yaliyoko Mahakama za Hakimu Mkazi, 21,538 yaliyoko Mahakama za Wilaya na 197,715 yaliyoko Mahakama za Mwanzo.

Aidha, Mahakama pia itaongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri katika ngazi za Mahakama za Mikoa (RMs na Wilaya) kwa kutenganisha shughuli za Kimahakama na za Kiutawala. Vilevile, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendesha mashauri ya Madai, Katiba na Jinai na kushughulikia mashauri ya zamani na mengine mapya yatakayopokelewa.

Kufanya Utafiti na Tafasiri ya Sheria

61.      Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka 2013/2014 Wizara yangu itaendelea kufanya mapitio ya Mfumo wa Sheria zinazosimamia huduma za jamii kwa wazee, Sheria zinazomlinda Mlaji na Sheria za makosa ya jinai. Kutafsiri Sheria kutoka lugha ya kingereza kwenda Kiswahili, kufanya uchambuzi wa hukumu za kesi za Mahakama ya Rufani ili kuainisha misingi ya kisheria na kuziweka kwenye tovuti ya Tume ya Kurekebisha Sheria.
Aidha, Wizara yangu itafanya mapitio ya Sheria mbalimbali ili kuhakikisha kuwa hazikinzani na Katiba ya Nchi na Misingi ya Haki za Binadamu.


Uandishi wa Sheria na Hati za Serikali

62.      Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa kuwa na Mfumo wa Sheria nchini unaokidhi mahitaji ya jamii katika kujiletea maendeleo kiuchumi, kijamii na kiteknolojia, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itatekeleza yafuatayo:-

(i)       kusimamia uandishi, tafsiri na urekebu wa Sheria mbalimbali za Nchi;
(ii)      kutayarisha maazimio mbalimbali ya kimataifa ambayo Nchi imeweka saini ili yaridhiwe na Bunge; na
(iii)    kuwezesha upatikanaji wa Sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge.

Kuimarisha Taasisi za Mafunzo ya Sheria

63.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itaendelea kuimarisha Taasisi za Mafunzo ya Sheria kwa kuanzisha ushirikiano maalum wa maendeleo ya watumishi kati ya Mahakama, Chuo cha Uongozi wa Mahakama na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania.

Kuimarisha shughuli za Usajili, Ufilisi na Udhamini

64.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kuimarisha shughuli za wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ili kuhakikisha kwamba lengo la Taasisi hii la kuwa Wakala linafikiwa kwa ufanisi. Katika Mwaka wa Fedha 2013/2014 Wakala unatarajia kuupeleka Mfumo wa Usajili wa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano (Under 5 Births Registration Initiative - U5BRI) hadi ngazi ya Serikali za Mitaa, ili kupunguza mlundikano wa vizazi ambavyo havijasajiliwa na kumwezesha mtoto kupata cheti cha kuzaliwa ambacho ni haki yake ya msingi. Mpango huu unatarajiwa kuanza rasmi katika Mkoa wa Mbeya na kuendelea kuutekeleza katika Mikoa ya Simiyu, Geita, Shinyanga na Mwanza. Katika Mfumo huu, utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa mara ya kwanza hutolewa bila tozo kwa watoto wote walio na umri wa chini ya miaka mitano. Aidha, Wakala pia utatekeleza Mkakati wa kusajili watoto wa umri kati ya miaka 6 hadi 18 (6-18 Birth Registration Initiative) waliopo mashuleni kwa kutumia Bajeti ya Serikali.

Vilevile Wakala unatarajia kuanzisha mazungumzo kati yake na NIDA - pamoja na Uhamiaji ili kuona namna ya kupunguza gharama za usajili kwa kutumia Mifumo ambayo tayari ipo kwa ajili ya uandikishaji na uchapishaji wa vyeti.

Kuimarisha Haki za Binadamu na Utawala Bora

65.      Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa Sheria na taratibu zilizowekwa na mamlaka mbalimbali kuhusu haki za binadamu zinafuatwa wakati wote wa utekelezaji wa majukumu mbalimbali. Kwa kuzingatia hilo, Ofisi imedhamiria kufanya yafuatayo:-

(i)       kutoa ushauri wa kisheria ulio bora katika masuala ya Katiba na Haki za Binadamu;
(ii)      kuandaa taarifa za utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu nchini kwenye mikataba ya kikanda na kimataifa ya Haki za Binadamu ambayo Nchi imeridhia na kuziwasilisha kwenye vyombo husika kwa ajili ya majadiliano; na
(iii)     kufanya ukaguzi katika maeneo yanayohifadhi mahabusu na wafungwa ili kutoa ushauri wa namna ya kuboresha.

66.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora itaendelea kulinda, kukuza na kuhifadhi haki za binadamu na utawala bora. Katika Mwaka 2013/2014 Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora itaendelea kukamilisha uchunguzi wa mashauri ya uvunjwaji wa haki za binadamu ambao haukukamilika, kufanya tafiti kuhusu haki za binadamu na utawala bora; kupitia miswada na Sheria ili kuangalia kama zinakidhi vigezo vya kimataifa na vya kikanda ili kulinda haki za binadamu na utawala bora; na kukagua Magereza na Vituo vya Polisi na Sehemu nyinginezo wanamozuiliwa watu.
Aidha, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora itaendelea kushughulikia malalamiko yaliyosalia na yatakayopokelewa yanayohusu uvunjwaji wa haki za binadamu.

67.      Mheshimiwa Spika, katika kusimamia maadili ya Mahakimu, Wizara yangu kupitia Tume ya Utumishi wa Mahakama itaendelea kuzijengea uwezo Kamati za maadili za Mikoa na Wilaya kwa Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara Tanga, Dodoma na Singida kwa kuzipatia mafunzo ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Aidha, Tume itaendelea na kazi ya kukagua Kamati za Maadili za Mkoa na Wilaya kwa Mikoa ya Mtwara, Lindi, Mbeya, Rukwa na Katavi. Lengo likiwa ni kuona kama zinatekeleza majukumu yake kwa misingi ya sheria na taratibu. Tume itaitisha vikao vinne vya kawaida kwa ajili ya kujadili na kuamua masuala mbalimbali ya watumishi.

Kuratibu mchakato wa Mabadiliko ya Katiba

68.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itaendelea kuratibu jambo kubwa na la kihistoria nchini mwetu ambalo ni mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Awamu ya kwanza ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi na makundi mbalimbali imekamilika. Hivi sasa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaendelea na uchambuzi wa maoni hayo ili kuandaa Rasimu ya Katiba itakayowasilishwa kwenye Mabaraza ya Katiba. Aidha, katika Mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara yangu kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba inategemea kufanya mambo yafuatayo ili kukamilisha Mchakato huu wa mabadiliko ya Katiba:-

(i)       Kusimamia Mikutano ya Mabaraza ya Katiba;
(ii)      Kuchambua maoni yatakayo tolewa na wajumbe wa Mabaraza ya Katiba;
(iii)   Kuchapisha Ripoti na Rasimu ya Katiba;
(iv)   Kuwasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalum la Katiba; na
(v)    Kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kushiriki katika Kura ya Maoni.

69.      Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa mchakato huu wa mabadiliko ya Katiba, kupitia kwenu Waheshimiwa Wabunge, ninaomba muwahamasishe wananchi wa majimbo yenu ili waweze kujitokeza kwa wingi katika kutoa mawazo kuhusu Rasimu ya Katiba kupitia kwa wajumbe wanaounda Mabaraza ya Katiba. Nawahamasisha na kuziomba Taasisi, Asasi za kiraia, jumuia za kidini, vyama vya siasa na makundi mengine yote kuunda Mabaraza ya Katiba. Aidha, ninawaomba wajumbe wa mabaraza kutoa mawazo yao kwa uwazi, uhuru na bila ya hofu yoyote. Pia nipende kuwahakikishia wananchi kuwa Tume inafanya kazi zake kwa uhuru na uwazi, na kwamba maoni yote yaliyotolewa na yatakayotolewa na wananchi, Taasisi, Asasi za Kiraia na makundi mengine yanaheshimiwa na kufanyiwa kazi ipasavyo.

Uratibu na utekelezaji wa Programu ya Maboresho ya Sekta ya Sheria na Miradi ya maendeleo

70.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itaendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Muda wa Kati (Medium Term Strategy) wa Programu hii, kwa kuendelea kuziwezesha Taasisi zinazotekeleza Programu hii kuboresha Mfumo wa Sheria na kuimarisha mazingira ya kisheria yanayoongeza fursa ya wananchi ya kupata haki kwa wakati ili kuwezesha jamii kutumia muda wao mwingi katikakujihusisha na kazi za maendeleo ya kiuchumi na kijamii, badala ya kupoteza muda huo, wakitafuta haki. Aidha, napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa, Wizara imekwisha anza kujiandaa kukamilisha na hatimaye kufunga programu kwa kuanza kutekeleza kazi ya kufanya tathimini ya hali ya sasa ya Sekta hii (Legal Sector Assessment) ili kujua kiwango cha maendeleo kilichofikiwa, kubaini changamoto zinazoikabili Sekta hii na kutambua fursa zilizopo na ambazo zinaweza kutumika kikamilifu katika mipango hiyo ya kuboresha sekta hii muhimu.

71.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kubuni mbinu na kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ya kuboresha huduma zitolewazo na Taasisi mbalimbali za Sheria, ili kuweza kufikia dira yetu ya haki sawa kwa wote na kwa wakati. Kama ambavyo nililiarifu Bunge lako Tukufu mwaka uliopita kwamba, Wizara yangu imebuni na itaanzisha Mradi wa “e-justice”, ninafurahi kulialifu Bunge lako Tukufukwamba, tayari hatua za awali za Mradi huu zimekwishaanza na Serikali ya China imeridhia kufadhili mradi huu. Tayari kazi ya upembuzi yakinifu wa Mradi huo inafanywa na Kampuni ya ZTE Corporation, iliyokasimiwa kazi hiyo na Serikali ya China. Kutegemea na taarifa ya upembuzi yakinifu wa Mradi huu itakayo andaliwa, Wizara yangu itatekeleza Mradi huu kwa awamu tatu. Awamu ya kwanza ikiwa ni majaribio (Pilot Study) kwa Mkoa wa Dar es Salaam, kisha kuhusisha Mikoa yote yenye Kanda za Mahakama Kuu kwa awamu ya pili na awamu ya tatu  kukamilisha Mradi kwa kufikia Mikoa yote Tanzania Bara.

72.         Mheshimiwa Spika, katika kuzingatia umuhimu wa kuwepo na Mikataba mizuri yenye maslahi kwa taifa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, itaendelea kuwajengea uwezo wa kitaalam Mawakili wa Serikali katika nyanja za kujadili, kuandika na kuhakiki mikataba kupitia Mradi wa UNDP- unaofadhiliwa  na Shirika la Umoja wa Mataifa – UNDP.  Katika uendeshaji wa mashauri ya  rushwa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kutekeleza Mradi wa Uimarishaji wa Mapambano Dhidi ya Rushwa Tanzania (STACA) kwa kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali katika uendeshaji wa mashauri  ya rushwa, ununuzi wa vitendea kazi, uimarishaji wa  mfumo wa utunzaji na usimamizi wa kumbukumbu za mashauri kielektroniki (Case Docket Management System).

Kuimarisha Usimamizi na Uwajibikaji katika rasilimali

73.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imezingatia lengo hili katika mipango yake ili kuhakikisha kwamba kunakuwa na usimamizi madhubuti wa rasilimali mbalimbali za Serikali. Katika kufanikisha lengo hili mambo yafuatayo yatafanyika:-

(i)     Kufanya ukaguzi wa matumizi ya fedha katika Ofisi za Makao Makuu na Mikoa kwa Taasisi zote za Wizara;
(ii)    Kufanya ukaguzi wa vifaa mbalimbali vilivyopo na vinavyonunuliwa katika Ofisi zote;
(iii)   Kutayarisha ratiba ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa malengo yaliyopangwa na Wizara na Taasisi zake ili kuwezesha utekelezaji na utoaji wa taarifa;
(iv)   Kuimarisha uratibu, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mipango ya Wizara;
(v)    Kuimarisha uwajibikaji na uadilifu katika utendaji wa kazi katika ngazi mbalimbali;
(vi)   Kuwaongezea watumishi maarifa na ujuzi katika maeneo yao ya kitaalam ili wawe na tija wakati wa kutekeleza majukumu yao hasa katika maeneo ambayo yameonekana kuwa na changamoto nyingi katika kuleta ufanisi wa utendaji; na
(vii)  Kuandaa Mpango thabiti wa rasilimali watu kwa Wizara na Taasisi na kuchambua mahitaji ya ujuzi kwa kila eneo la utekelezaji.


F.    SHUKRANI
74.      Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru sana wadau wetu wa maendeleo kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha Sekta yetu ya Sheria. Kwa namna ya pekee napenda kushukuru nchi za CANADA na Denmark ambazo kupitia Mashirika yao ya Kimataifa ya Maendeleo ya CIDA na DANIDA wameisaidia sana Wizara yangu katika kushawishi Mashirika na nchi nyingine wahisani kuelekeza misaada yao katika kuboresha Sekta ya Sheria. Nayashukuru pia Mashirika na Taasisisi za Kimataifa zifuatazo: - Benki ya Dunia (WB), Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Watoto (UNICEF), Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) na Taasisi ya Maendeleo ya Kimataifa ya Serikali ya Uingereza (DFID).

75.      Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani za pekee kwa wadau mbalimbali wa Sekta ya Sheria kwa ushirikiano na ushauri uliowezesha kutekelezwa kwa majukumu ya Wizara kwa mwaka 2012/2013 kama yalivyobainishwa katika Hotuba hii. Ninapenda kumshukuru Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Angela Kairuki (Mbunge), Jaji Mkuu Mheshimiwa Othmani Chande, Mwanasheria Mkuu wa Serikali , Mheshimiwa Frederick Mwita Werema, Jaji Kiongozi  Mheshimiwa Fakih A.R Jundu, Katibu Mkuu  wa Wizara ya Katiba na Sheria ndugu Fanuel E.Mbonde, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ndugu Hussein Kattanga, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndugu George Masaju, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, ndugu Ignas Paul Kitusi, Mkurugenzi wa Mashtaka Dr. Eliezer M. Feleshi, Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Bi. Winifrida Korroso, Katibu Mtendaji Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Bi.Mary Massey, Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Mheshimiwa Dr. Gerald Ndika, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa RITA, nduguPhilip Saliboko, Wakurugenzi wa Idara na Taasisi zilizo chini ya Wizara na Watumishi wote kwa ushirikiano na kazi kubwa waliyoifanya katika kuandaa Mpango na Bajeti hii kwa wakati. Ni matarajio yangu kwamba Wizara itaendelea kupata ushirikiano wao katika mwaka 2013/2014 kama walivyofanya nitekeleze majukumu yangu na wajibu wangu kwa ufanisi hadi sasa. Mwisho nitoe shukrani kwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kufanikisha uchapishaji wa Hotuba hii.

G.      MAJUMUISHO

76.      Mheshimiwa Spika, tukitambua kwamba Sekta ya Sheria ndio jiwe la msingi katika utawala wa Serikali na kwa kuzingatia umuhimu wa Sekta ya Sheria katika kuchochea maendeleo ya Nchi kiuchumi, kisiasa, kijamii, kisayansi na kiteknolojia, Wizara ya Katiba na Sheria inao wajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba inakuza, inaimarisha na inalinda amani na utulivu na kudumisha haki za binadamu na utawala wa Sheria nchini.

Napenda kutoa wito kwa wananchi wote na Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha kuwa azma ya Serikali ya kulinda Amani, Utulivu na Haki za Binadamu inazingatiwa, inaendelezwa na kupewa kipaumbele kwa manufaa ya Taifa letu na kizazi kijacho.

H.      MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2013/2014

77.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa fedha 2012/2013 Wizara ya Katiba na Sheria ilitetengewa jumla ya Sh. 186,323,718,000. Hadi kufikia tarehe 28 Februari, 2013 jumla ya Sh.86,005,210,966.19. Ili kutekeleza majukumu yaliyopangwa kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014, Wizara yangu inaomba kuidhinishiwa kiasi cha Sh.230,687,333,000 kwa ajili ya Taasisi, Idara na Vitengo vya Wizara. Matumizi ya Kawaida yanayoombewa jumla ya Sh.195,427,547,000. Kati ya fedha hizo, Sh.152,890,448,000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Sh.42,537,099,000 ni kwa ajili ya Mishahara. Miradi ya Maendeleo inaombewa jumla ya Sh.35,259,786,000. Kati ya fedha hizi Sh.24,000,000,000 ni za ndani na Sh.11,259,786,000ni fedha za nje. Mchanganuo wa matumizi ya bajeti kwa mafungu ya Wizara ni kama ifuatavyo:

MATUMIZI:

Fungu 8: Tume ya Mabadiliko ya  Katiba.

Matumizi Mengineyo       Sh.33,944,588,000/=
                                 
               Jumla              Sh. 33,944,588,000/=

Fungu 12: Tume ya Utumishi wa Mahakama

Matumizi ya Mishahara    Sh. 161,882,000/=
Matumizi Mengineyo        Sh.2,871,716,000/=

Jumla                Sh. 3,033,598,000/=

Fungu 16: Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Matumizi ya Mishahara      Sh. 2,174,186,000/=
Matumizi Mengineyo         Sh.8,332,865,000/=
Matumizi ya Maendeleo (nje)   Sh.826,000,000/=

Jumla               Sh.11,333,051,000/=

Fungu 35: Mkurugenzi wa Mashtaka

Matumizi ya Mishahara      Sh. 4,383,211,000/=
Matumizi  Mengineyo          Sh. 6,460,826,000/= 
Matumizi ya Maendeleo(nje)Sh.2,167,759,000/=           
Jumla      Sh.13,011,796,000/=

Fungu 40: Mahakama

Matumizi ya Mishahara    Sh. 30,980,157,000/=
Matumizi Mengineyo        Sh. 86,600,000,000/=
Matumizi ya Maendeleo(ndani)
     Sh. 20,000,000,000/=
Matumizi ya Maendeleo(nje)Sh.2,716,668,000 /=

              Jumla                         Sh.140,296,825,000/= 

Fungu 41: Wizara ya Katiba na Sheria

Matumizi ya Mishahara     Sh. 2,447,110,000 /=
Matumizi  Mengineyo         Sh. 8,028,651,000 /=
Matumizi ya Maendeleo (ndani)
                   Sh.4,000,000,000/=           
Matumizi ya Maendeleo.(nje)       
       Sh. 3,898,840,000/=

              Jumla                Sh.18,374,601,000/=

Fungu 55: Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora

Matumizi ya Mishahara       Sh.1,814,993,000/=
Matumizi  Mengineyo                    Sh.3,795,802,000/=
Matumizi ya Maendeleo (nje)  Sh.1,034,169,000/=

Jumla  Sh.  6,644,964,000 /=
Fungu 59: Tume ya Kurekebisha Sheria

Matumizi ya Mishahara      Sh.   575,560,000/=
Matumizi  Mengineyo          Sh. 2,856,000,000/=
Matumizi ya Maendeleo(nje)  Sh.   616,350,000 /=        
                        Jumla            Sh. 4,047,910,000/=


I.    MAKUSANYO YA MADUHULI

78.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kwa Mwaka 2013/2014 inatarajia kukusanya jumla ya kiasi cha Sh.5,250,454,700/= kama maduhuli ya Serikali. Mchanganuo wa makusanyo kwa mafungu husika ni kama ifuatavyo:

Fungu 16:     Sh.                3,002,000/=   
Fungu 40:     Sh.         2,261,303,900/=
Fungu 41:     Sh.         2,983,648,800/=
Fungu 55:     Sh.                2,500,000/=         
Jumla      Sh. 5,250,454,700/=
                     
79.      Mheshimiwa Spika,mchanganuo wa maombi ya fedha kwa kila Fungu umeainishwa kwenye Randama zilizoandaliwa kwa kila Fungu na kuwasilishwa hapa Bungeni rasmi.

80.      Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Kiambatisho ‘A’
MGAWANYO WA FEDHA ZA MATUMIZI YA KAWAIDA NA MAENDELEO KITAASISI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
FUNGU
MAELEZO
MISHAHARA
MATUMIZI MENGINEYO
MAENDELEO NDANI
MAENDELEO NJE
JUMLA
8
Tume ya Mabadiliko ya Katiba
                          -  
        33,944,588,000
                         -  
                         -  
      33,944,588,000
12
Tume ya Utumishi wa Mahakama
           161,882,000
          2,871,716,000
                         -  
                         -  
        3,033,598,000
16
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
        2,174,186,000
          8,332,865,000
                         -  
          826,000,000
      11,333,051,000
35
Mkurugenzi wa Mashtaka
        4,383,211,000
          6,460,826,000
                         -  
       2,167,759,000
      13,011,796,000
40
Mahakama
30,980,157,000
86,600,000,000
20,000,000,000
2,716,668,000
140,296,825,000
41
Wizara ya Katiba na Sheria
        2,447,110,000
          8,028,651,000
       4,000,000,000
       3,898,840,000
      18,374,601,000
55
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
        1,814,993,080
          3,795,802,000
                         -  
       1,034,169,000
        6,644,964,000
59
Tume ya Kurekebisha Sheria
           575,560,000
          2,856,000,000
                         -  
          616,350,000
        4,047,910,000
JUMLA

42,537,099,080
152,890,448,000
24,000,000,000
11,259,786,000
230,687,333,000

MAHAKAMA YA TANZANIA

IDADI YA MASHAURI YALIYOFUNGULIWA, YALIYOAMULIWA NA YALIYOBAKIA KATIKA MAHAKAMA MBALIMBALI ZA TANZANIA

JEDWALI Na.1 : Mwenendo wa Mashauri – Mahakama ya Rufani

Mwaka
Masha-uri yaliyo-kuwepo
Masha-
uri yaliyofu-nguliwa
Jumla
 ya Masha-uri
Masha-
uri yaliyosi-kilizwa
Mashauri yaliyo-baki
2008/09
1,798
824
2,622
552
2,070
2009/10
2,070
753
2,823
651
2,172
2010/11
2,172
615
2,787
637
2,059
2011/2012
2,059
727
2,786
1,043
1,743
2013/2014
1,743
450
2,193
275
1,918


JEDWALI Na.2 : Mwenendo wa Mashauri – Mahakama ya Kuu

Mwaka
Mashauri yaliyoku-wepo
Mashauri yaliyofu-nguliwa
Jumla ya Mash-auri
Mashauri yaliyosi-kilizwa
Masha-uri yaliyo-baki
2008/09
11,531
7,594
19,125
7,419
11,706
2009/10
11,706
7,743
19,449
8,517
10,932
2010/11
10,932
9,453
20,385
9,669
10,718
2011/2012
10,718
4,217
14,935
5,198
9,737
2012/2013
9,737
7,547
17,284
5,191
12,093




Jedwali Na.3: Mwenendo wa Mashauri Mahakama Kuu Divisheni Biashara

Mwaka
Mashauri yaliyo-kuwepo
Masha-uri yaliyofu-nguliwa
Jumla ya Masha-uri
Mashauri yaliyosi-kilizwa
Mashauri yaliyo-baki
2008/9/
105
12
117
109
8
2009/10
8
310
318
144
174
2010/11
174
268
442
174
268
2011/2012
268
189
457
172
285
2012/2013
285
118
403
74
329


Jedwali Na.4: Mwenendo wa Mashauri Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi

Mwaka
Mashauri yaliyo-kuwepo
Masha-uri yaliyofu-nguliwa
Jumla ya Masha-uri
Masha-uri yaliyosi-kilizwa
Masha-uri yaliyo-baki
2008/9/
572
903
1,475
412
1,063
2009/10
1,063
939
2,002
585
1,417
2010/11
1,417
1,403
2,400
893
1,507
2011/2012
1,507
986
2,493
896
1,597
2012/2013
1,597
674
2,271
491
1,780


Jedwali Na.5: Mwenendo wa Mashauri Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi

Mwaka
Masha-uri yaliyo-kuwepo
Masha-uri yaliyo-fungu-liwa
Jumla ya Masha-uri
Masha-uri yaliyosi-kilizwa
Masha-uri yaliyo-baki
2008/9/
4,859


1,548
3,311
2009/10
3,311
1,939
5,250
1,109
4,141
2010/11
4,141
2,313
6,454
1,371
5,083
2011/2012
5,083
1,417
6,500
1,107
5,393
2012/2013
5,393
427
5,820
427
3,393





Jedwali NA.6 : Mwenendo wa Mashauri – Mahakama za Hakimu Mkazi

Mwaka
Mashauri yaliyokuwepo
Mashauri yaliyofunguliwa
Jumla ya Mashauri
Mashauri yaliyosikilizwa
Mashauri yaliyobaki
2008/09
16,698
19,001
35,699
14,361
21,338
2009/10
21,338
17,582
38,920
18,664
20,256
2010/11
20,256
28,096
48,352
19,760
28,592
2011/12
28,592
14,191
42,783
17,781
25,002
2012/13
25,002
980
25,982
612
25,370



Jedwali  Na.7: Mwenendo wa Mashauri – Mahakama za Wilaya

Mwaka
Mashauri yaliyokuwepo
Mashauri yaliyofunguliwa
Jumla ya Mashauri
Mashauri yaliyosikilizwa
Mashauri yaliyobaki
2008/09
19,793
30,181
49,974
26,232
23,742
2009/10
23,742
31,370
55,112
28,050
27,062
2010/11
27,062
57,227
84,289
47,677
36,612
2011/12
36,612
77,495
114,107
83,082
31,025
2012/13
31,025
94,872
125,897
104,359
21,538

Jedwali  Na.8 : Mwenendo wa Mashauri – Mahakama za Mwanzo
Mwaka
Mashauri yaliyokuwepo
Mashauri yaliyofunguliwa
Jumla ya Mashauri
Mashauri yaliyosikilizwa
Mashauri yaliyobaki
2008/09
50,764
128,183
178,947
132,956
45,991
2009/10
45,991
140,095
186,086
145,770
40,316
2010/11
40,316
303,032
343,340
219,693
123,647
2011/12
123,647
512,308
635,955
510,996
124,959
2012/13
124,959
650,181
775,140
577,425
197,715

Jedwali Na.9: Malalamiko-Tume Ya Haki Za Binadamu na Utawala Bora

Mwaka
Idadi ya Malalamiko
Ya Zamani
Mapya
Jumla
Yaliyohitimishwa
Yaliyobaki
2008/09
2,285
2,073
4,358
789
3,569
2009/10
941
481
1,422
941
481
2010/11
7,542
1,333
8,875
1,042
7,833
2011/12
7,833
886
8,719
1,554
7,165
2012/13
7,165
1,185
8,350
688
7,662




Jedwali Na.10: Usajili wa Matukio-RITA

Mwaka/ Shughuli
Vizazi
Vifo
Ndoa
Talaka
Udhamini
Wosia
Mirathi
Kuasili
2008/09
938,775
105,482
15,345
73
247
-
-
39
2009/10
469,274
47,118
17,106
85
277
83
13
46
2010/11
625,670
73,810
23,108
69
203
36
14
33
2011/12
519,511
66,463
13,631
51
204
33
2
18
2012/13
331,272
59,099
6,094
42
151
37
1
23

         
                                                                

Jedwali Na. 11: Mwenendo wa Mashauri ya Madai kuanzia Mahakama ya Rufani hadi Mahakama za Wilaya

Mahakama
Mashauri yaliyokuwepo Juni 2012
Mashauri yaliyofunguliwa Julai hadi Machi, 2013
Jumla
Mashauri yaliyohitimishwa
Mashauri yaliyobaki
Mahakama ya Rufani
39
7
46
2
44
Mahakama Kuu
550
132
682
40
642
Maombi ya Madai
196
89
285
63
222
Jumla
785
228
1013
105
908

Jedwali Na.12: Mwenendo wa Mashauri ya Jinai kuanzia Mahakama ya Rufani hadi Mahakama za Wilaya

Mahakama
Mashauri yaliyokuwepo Juni 2012
Mashauri yaliyofunguliwa Julai hadi Machi, 2013
Jumla
Mashauri yaliyohitimishwa
Mashauri yaliyobaki
Mahakama ya Rufani
26
161
187
122
65
Mahakama Kuu
359
445
804
316
488
Mahakama za chini
14,068
12,881
26,949
4,819
22,130
JUMLA
14,453
13,487
27,940
5,257
22,683

Jedwali Na. 13 MISWADA

Mwaka
Idadi ya Miswada
Iliyoandaliwa
Iliyopitishwa na Bunge na Kusainiwa na Mhe. Rais
Inayofanyiwa Kazi
2008/2009
29
22
7
2009/2010
37
18
19
2010/2011
12
4
8
2011/2012
18
6
12
2012/2013
6
4
2

Jedwali Na. 14: Mwenendo wa Mashauri ya Katiba na Haki za Binadamu

Mahakama
Mashauri yaliyokuwepo Juni 2012
Mashauri yaliyofunguliwa Julai hadi Machi, 2013
Jumla
Mashauri yaliyohitimishwa
Mashauri yaliyobaki
Mahakama ya Rufani
5
4
9
0
9
Mahakama Kuu
32
29
61
17
44
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu
1
2
3
0
3
Jumla
38
35
73
17
56



Kiambatisho “B”

Orodha Ya Sheria Zilizotafsiriwa Katika Lugha Ya Kiswahili

Tafsiri ya Sheria za Tawala za Mikoa: Sura ya 97;
(i)    Tafsiri ya Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura 287; na
(ii)   Tafsiri ya Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura 288;
(iii)  Tafsiri rasmi ya Sheria ya Tozo za Mamlaka za Miji, Sura ya 289;
(iv) Tafsiri ya Sheria ya Fedha za Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Sura ya 290;
(v)   Tafsiri ya Sheria ya Serikali za Mitaa (Upambaji wa Majengo) sura ya 293;
(vi) Sheria ya Mipango Miji, Sura ya 335


Kiambatisho “C”

Orodha Ya Sheria Zilizofanyiwa Marekebisho

VAT Act, cap148
(i)          The Export Tax Act,
(ii)         The Protection of New Plant Varieties (Plant Breeders Rights)
(iii)        Tanzania Investment Act, Cap 38
(iv)       Gaming Act, cap 41
(v)        Motor Vehicle (Tax on Registration and Transfer) Act, Cap 124
(vi)       The Excise (Management and Tariff) Act, cap 147
(vii)      The Law Reform Commission Act, cap 171
(viii)     The East African Development Bank Act cap 231
(ix)       Local Government Finance Act, cap 290
(x)        The Local Government (Elections) Act cap 292
(xi)       The Public Service Act, cap. 298
(xii)      Income Tax Act , cap 332
(xiii)     The Airport Service Charge Act cap 365.

Kiambatisho “D”

Orodha ya Miswada Iliyopitishwa Na Bunge Na Kuwa Sheria

Muswada wa Sheria ya Fedha
(i)    Muswada wa Matumizi  ya Serikali;
(ii)   Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali; na
(iii)  Muswada wa Sheria ya kulinda Haki za Wagunduzi wa aina mpya za Mbegu za Mimea. 



Kiambatisho “E”

Orodha ya Rasimu za Sheria Zilizotafsiriwa na Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania na Kuwasilishwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Serikali

i.  Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya Mwaka 2002;
ii. Sheria ya Utakatishaji wa fedha Haramu ya Mwaka 2006;
iii.  Sheria ya Kuzuia usafirishaji Haramu wa Binadamu ya Mwaka 2008;
iv. Sheria ya Uthibitisho wa Wosia na Usimamizi wa Mirathi ya Mwaka 2002; na
v.  Sheria ya Madawa na Kuzuia usafirishaji Haramu wa Madawa ya Mwaka 1991.
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment