Vurugu zatikisa Arusha, Lindi

*Wananchi wapinga kuendelea kukopwa korosho zao
*Nyumba ya mbunge, ofisi, magari vyachomwa moto
*Lema achafua hali ya hewa, mkuu wa mkoa apigwa mawe

VURUGU kubwa zimetokea katika mikoa ya Arusha na Lindi na hivyo kuzusha tafrani na hali ya wasiwasi kwa wananchi wa maeneo hayo. Vurugu zilizotokea Wilaya ya Liwale mkoani Lindi, zimesababisha uharibifu mkubwa wa mali za watu, ikiwamo magari kadhaa na nyumba tano kuteketezwa kwa moto.

Nyumba ya Mbunge wa Liwale, Faith Mitambo (CCM) ni miongoni mwa nyumba zilizochomwa na kuteketezwa kwa moto, kutokana na vurugu hizo zilizoibuka usiku wa kuamkia jana.

Katika vurugu hizo, nyumba za viongozi mbalimbali wakiwamo madiwani, viongozi wa CCM, maofisa wa vyama vya ushirika ziliathiriwa pamoja na maduka kuporwa.

Habari kutoka Liwale, zimeeleza kuwa vurugu hizo zimeibuka kutokana na hasira za wananchi kupinga mfumo wa stakabadhi ghalani, unaowakandamiza wakulima wa zao la korosho.

Kwa muda mrefu sasa wananchi wa mikoa ya kusini, wamekuwa wakipinga mfumo wa stakabadhi ghalani, wakidai kuwa wamekuwa wakikopwa mazao yao bila ridhaa yao.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, Mwenyekiti wa Umoja wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Liwale, Amiri Mkalipa, alisema tatizo kubwa ni mfumo wa stakabadhi ghalani unaopingwa na wananchi.

“Hizi vurugu ni kubwa, kumetokea uharibifu wa mali mbalimbali. Nyumba takriban tano zimeteketezwa kwa moto, ipo nyumba ya mbunge wa Liwale na nyumba nyingine za madiwani.

“Katika watu walioathirika ni pamoja na mjumbe wetu wa halmashauri kuu Wilaya ya Liwale, ambaye maduka yake mawili yameporwa mali kabla ya nyumba yake kuchomwa moto,” alisema.

Mkalipa alipoulizwa sababu za kutokea kwa vurugu hizo alisema: “Hapa tatizo ni mfumo huu wa stakabadhi ghalani, ambao wananchi wengi wanaupinga.

“Tatizo limeanzia kwenye malipo ya awamu ya pili. Bei elekezi ya kilo moja ya korosho ni Sh 1, 200 awamu ya kwanza walilipwa Sh 600 sasa awamu ya pili imechelewa.

“Licha ya kuchelewa lakini fedha zenyewe zimekuja pungufu, jambo hili limewatia hasira wananchi kwa hivyo wakaamua kufanya hizo fujo,” alisema.

Taarifa zaidi kutoka Liwale zinasema kuwa, tafrani ilianza kutokea katika Kijiji cha Liwale B, ambako wakulima wa Chama cha Msingi kiitwacho Minali walikataa malipo ya Sh 200 kama malipo ya awamu ya pili, badala ya Sh 600 kama walivyoahidiwa.

Mwenyekiti wa chama hicho, Mohamed Limbwilindi alienda kijijini hapo akiwa na Sh milioni 61 ambazo wakulima hao wangelipwa Sh 200 kwa kilo moja.

“Wengine ambao hawakupewa malipo ya awali walielezwa kuwa watalipwa Sh 800, jambo ambalo lilizua mtafaruku miongoni mwao na ndipo fedha zikarudishwa.

Alisema, kutokana na hali hiyo wananchi wenye hasira wakateketeza moto ofisi ya chama hicho na nyumba ya mwenyekiti wa Minali, kabla hawajaishambulia pia nyumba ya katibu mkuu wake, Juma Majivuno.

“Niliona kundi kubwa la watu wanakuja nyumbani kwangu majira ya saa 3 usiku, wakiwa wamebeba nondo, mawe pamoja na madumu ambayo nadhani kulikuwa na petrol.

“Watu hao walinieleza kuwa wanataka fedha zao za korosho. Hali hii ilinitisha nikalazimika kukimbia ili kujisalimisha,” alisema Mohamed.

Baada ya vurugu hizo huko Liwale B, jana alasiri vurugu zilihamia mjini Liwale ambako uharibifu mkubwa wa mali ulifanywa.

Wengine waliochomewa nyumba zao ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Liwale, Mohamed Ngomambo ambaye alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema:

“Mimi namwachia Mungu, kama nimepoteza wazazi ambao wana thamani kubwa maishani mwangu, nyumba ni kitu gani kwangu,” alisema kwa huzuni.

VURUGU ARUSHA

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mullongo, jana alijikuta akishushiwa mvua ya mawe na kunusurika kipigo kutoka kwa wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu mkoani humo.

Vurugu hizo ziliibuka baada ya mwanafunzi mwenzao, Henry Kago (22) wa mwaka wa pili, kudaiwa kuuawa katika mazingira yenye utata.

Kutokana na hali hiyo, Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walioandamana na mkuu huyo wa mkoa walilazimika kutumia mabomu ya machozi ili kuwatawanya wanafunzi hao.

Kunusurika kwa Magesa kumekuja wakati Mulongo akiwa chuoni hapo na wajumbe wa kamati yake ya ulinzi na usalama ya mkoa, ili kuzungumza na wanafunzi kusikiliza kilio chao.

Mwanafunzi huyo alikutwa akiwa amekufa katikati ya eneo la makao makuu ya Kanisa la Sabato na chuo cha ESAMI eneo la Njiro jijini hapa.

Wakati Magesa akiwasili chuoni hapo, tayari Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alifika eneo hilo na kuanza kuzungumza na wanafunzi hao akiwa juu ghorofani, kwa lengo la kutuliza hasira za wananchi hao.

Katika mazungumzo hayo, Lema alikuwa akiwasihi wanafunzi hao kuacha jazba na badala yake wafuate njia sahihi za kutatua tatizo lililokuwa mbele yao, badala ya kuanza kufanya maandamano kama walivyokuwa wamepanga.

Katika mazungumzo yake, Lema alimvaa Mulongo na kudai kuwa kiongozi huyo alikwenda katika eneo hilo la tukio akiwa ki “sharobaro” hatua iliyowafanya wanafunzi kulipuka kwa kumzomea mkuu wa mkoa.

Akiwa amepanda juu ya ngazi za moja ya bweni chuoni hapo, Lema aliendelea kuzungumza na wanafunzi kwa kuwasisitiza wasome kwa bidii na waachane na anasa.

“Washikaji nakwenda zangu kwenye msiba, mkuu wa mkoa amekuja ila msikubali kushindwa lazima msonge mbele.

“Nawaomba muache tabia zenu za kupenda starehe na kwenda kwenye klabu, someni na nyinyi wasichana msipende kuingia kwenye klabu kwa kulipiwa fedha someni kwanza,” alisema Lema.

Hata hivyo Mulongo aliamuru Lema ateremke chini kwa ajili ya kwenda kwenye bwalo la chakula lililokuwa limeandaliwa kwa ajili ya mazungumzo ya wanafunzi na viongozi wa Serikali.

Mara baada ya kushawishi wanafunzi hao kuelekea kwenye ukumbi wa mazungunzo, huku wengine wakiendelea kupinga kitendo hicho, hali ya hewa ndipo ilipochafuka.

Wanafunzi walianza kurusha mawe kuelekea alipokuwa amesimama mkuu huyo wa mkoa, huku polisi nao wakifyatua mabomu ya machozi hali iliyozua tafrani.

Hata hivyo polisi waliweza kumuokoa kwa kumuingiza katika gari mkuu huyo wa mkoa, kisha kuondolewa katika eneo la tukio kwa kasi.

RC MULONGO

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Mulongo alisikitishwa na kitencho cha Lema kuingia ndani ya eneo la chuo hicho na kufanya siasa kupitia tukio la kifo cha mwanafunzi.

Mulongo alisema tukio la kifo hicho bado linachunguzwa, kutokana na kuwapo madai kuwa mwanafunzi huyo alikuwa akitoka klabu ya starehe, huku taarifa nyingine zikidai alikuwa akitoka kujisomea.

Kutokana na tukio hilo Mulongo ameliagiza Jeshi la Polisi kumkamata Lema na wanafunzi wote walioshiriki kurusha mawe, ili watoe maelezo zaidi.

Kutokana na vurugu hizo, mkuu wa chuo hicho, Faraj Kasidi alitangaza kufunga chuo hicho chenye wanafunzi 3,300 kwa muda usiojulikana.
chanzo:Mtanzania

Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment