Prof Ibrahim H Lipumba - Mwenyekiti Wa CUF Taifa |
Majibu yasiyoridhisha kutoka kwa serikali yamekuwa ni chanzo kingine cha sintofahamu inayoendelea bungeni.
Mawaziri na manaibu mawaziri wamekuwa hawatoi majibu yaliyojitosheleza ama kutotoa majibu ambayo hayaendani na maswali yaliyoulizwa.
Spika amekuwa muoga kuwalazimisha mawaziri kujibu maswali ya wabunge kwa ufasaha na umakini mkubwa.
Hii imepelekea wabunge wengi kuleta vurugu bungeni wakilazimisha maswali yao yajibiwe kwa ufasaha na usahihi.
Lifuatalo Ndio Tamko Halisi
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
25/04/2013
1:KUHUSU HALI YA BUNGE LA SASA
Kutokana na mwenendo wa bunge kumekuwa na mkanganyiko mkubwa wa Wananchi juu ya nini hatma ya bunge na mustakabali wake kwani Bunge halionekani kujikita katika kutetea maslahi ya Wananchi kwa sababu ya matukio yafuatayo.
SPIKA KUPOTEZA UWEZO WA KUONGOZA
Bunge la hivi sasa limekuwa na vurugu za hapa na pale hasa wabunge kutotii kanuni za bunge. Mfano wabunge kuzomea ovyo, tabia za kutovumiliana, kutotii amri ya Spika, wabunge kutohudhuria bungeni nk. Hii yote inatokana na meza ya spika kupoteza sifa za kuliongoza bunge. Hasa pale spika wa bunge anakuwa anafanya maamuzi yanaoubeba upande wa CCM na kupuuza upande wa upinzani ama kutupilia mbali hoja za upinzani kwa sabau zisizo za msingi.
Halikadhalika kuyumba kwa kuruhusu kujadili jambo ambalo lipo chini wa muhimili mwengine wa dola yaani Mahakama, na bado hukumu ya jambo hilo haijatolewa.
Mfano baada ya Spika Anna Makinda kutangaza kwamba mbunge atakayetukana atachukuliwa hatua za kisheria kesho yake Mbunge wa CCM alitukana kwa Kiingereza bila kuchukuliwa hatua zozote na baadae Wabunge wa Chadema walitolewa nje kwa kosa la kumtetea mbunge mwenzao asitolewe nje.
Spika wa Bunge anaonesha maamuzi yaliyolalia upande mmoja na kutoa adhabu kwa baadhi ya wabunge na kuwaacha wengine inawafanya wabunge wengi kudharau ofisi ya spika na kutofuata taratibu na kanuni za bunge ili kupigania kile wanachokitaka kifanyike.
SERIKALI
Majibu yasiyoridhisha kutoka kwa serikali yamekuwa chanzo kingine cha sintofahamu inayoendelea bungeni. Mawaziri na manaibu mawaziri wamekuwa hawatoi majibu yaliyojitosheleza ama kutotoa majibu ambayo hayaendani na maswali yaliyoulizwa. Spika amekuwa muoga kuwalazimisha mawaziri kujibu maswali ya wabunge kwa ufasaha na umakini mkubwa. Hii imepelekea wabunge wengi kuleta vurugu bungeni wakilazimisha maswali yao yajibiwe kwa ufasaha na usahihi.
KAMBI RASMI YA UPINZANI KUYUMBA
Kambi rasmi ya upinzani imepoteza uwezo wa kujenga hoja za mashiko na mbinu madhubuti za kuwabana wabunge wa CCM bungeni. Kumekuwa na tabia mbaya ya wabunge wa Chadema kufuata mfumo wa CCM wa kwenda bungeni na hoja zinazobeba chama chao na si watanzania wote kama jinsi CCM wanavyo fanya. Kambi rasmi ya upinzani pia imeshindwa kulinda utaratibu mzuri wa kutetea maslahi ya umma bila jazba na hoja zenye mashiko kama jinsi ilivyokuwa miaka ya nyuma CUF ilipokuwa ikiongoza kambi hiyo.
CUF tunaitaka kambi rasmi ya upinzani ijipange upya kwa utaratibu ulio na mikakati mizuri ya kutetea hoja za Wananchi bungeni bila kuyumbishwa na wabunge wa CCM.
MATUMIZI MABAYA YA MUDA NA MATUSI
Hivi sasa Bunge linatumia muda vibaya kwa ubishi usio na tija yoyote ama maslahi kwa wananchi. Wabunge wamekuwa wakiwaingilia wabunge wenzao kwa hoja na miongozo isiyo na mashiko wanapozungumza ilimardi tu ama amemvuruga mwenzake asiendeleee ama kwa lengo la kutaka kuua hoja ya mbunge mwengine.
Utaratibu huu umekuwa si mzuri kwani muda mwingi umekuwa ukitumiwa na wabunge kujibizana ama kutaka tu asikike akiongea hata kama jambo analotaka kuongea halina mantiki yoyote. Haya matumizi mabovu ya pesa za mlipa kodi anayelala njaa ili wabunge walipwe posho. Badala yake wabunge wanalipana kubishana na kutokujenga hoja za kumtetea mwananchi, wabunge lazima wawatendee haki wananchi.
Kwa muda sasa bunge limekuwa likisikika kwa matusi makali na ya aibu hata kutamka. Hii imetokana na wabunge wengi kutotambua hasa ni nini kilichompeleka bungeni na anapaswa akifanye vipi. Jazba na kukosa subira miongoni mwa wabunge na tabia ya kutaka kutumia hoja ya nguvu badala ya nguvu ya hoja kumechangia sana wabunge wengi kutumia matusi wakidhani ndio wataeleweka.
CUF tuanawataka wabunge wote kutumia hoja zaidi katika kujadili na si aina yoyote ya nguvu. Kawaida kutumia nguvu ama matusi ni ishara ya kuishiwa uwezo wa kufikiri juu ya jambo husika. Halikadhalika kujenga tabia ya kuvumiliana wakati mbunge mwengine akiwasilisha mawazo yake kuliko kumkatiza kwa kutumia kanuni na miongozo, jambo ambalo halionyeshi ukomavu wa kisiasa na ujengaji hoja.
HOJA HATARISHI
Bunge hivi sasa limekuwa likijikita katika hoja hatari zaidi kwa umoja na amani ya nchi yetu tena bila tahadhari kubwa. Mfano mzuri ni sula la udini, wabunge wanashindwa kujenga hoja za namna ya kuondoa tatizo hili la udini na badala yake wao wenyewe wanageuka wadini. Hii ni hatari kwani bunge litajikuta linawasha moto wa udini ambao ni vigumu sana kuuzima kwa Wananchi. Ni vyema bunge likawa makini sana linapojadaili hoja ya udini hasa kipindi hiki cha sasa hivi ambapo wapiga kura na wafuasi wamekuwa wakifuatilia mwenendo wa Bunge lao.
BUNGE UWANJA WA MASHINDANO YA VYAMA
Siasa ya vyama vya siasa zinalitafuna bunge letu .Wabunge na serikali wamesahau kwamba wameingia bungeni si kutetea vyama vyao bali kutetea Wananchi. Vyama vyao ni tiketi tu ya kuingia bungeni ili kuwatetea wanachi. Wabunge wa vyama tofauti nje ya bunge wanaongea na wanaelewana lakini ndani ya bunge hawaelewani na hata hawako tayari kuunga mkono kwa pamoja mambo yanayogusa maslahi ya umma ama kupinga kwa pamoja mambo yanayokandamiza maslahi ya umma.
Badala yake bunge limekuwa uwanja wa kuonesha chama chako kinafanya nini huko nje ya bunge na harakati zake zikoje.
Bunge kwa kiasi kikubwa limesahau kabisa kulinda maslahi ya umma na kuongelea matatizo ya msingi ya wanachi na badala yake wanagusa mambo yale tu yanayoangalia maslahi ya vyama vyao mfano kesi za vyama. Migogoro ya vyama na serikali ama migogoro ya vyama na vyama. Hii ni hatari kubwa sana kwa nchi ambayo imo ndani ya dimbwi la umaskini.
Chama Cha CUF kinawataka wabunge watambue kwamba wananchi wana matatizo makubwa umaskini, ukosefu wa ajira, elimu mbovu, huduma mbaya za afya, wakulima hawalipwi bei stahiki ya mazao yao, ardhi inaporwa na haki zao za msingi zinavunjwa. Hayo ndiyo wanapaswa kuyapigania. Pia tunaitaka serikali ya CCM iwajibika katika kutetea maslahi ya Watanzania wote na siyo maslahi ya CCM.
WABUNGE WA CCM
Kwa bunge linavyoendelea hivi sasa kimsingi kumekuwa na hoja ambazo hazilengi kumsaidia mwananchi. Wabunge wa CCM wamekuwa goigoi sana katika kulinda na kutetea maslahi ya umma. Badala yake wabunge wa upinzani ndio wamekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya Wananchi na wa CCM wamekuwa mbele kutetea maslahi ya serikali na kusahau wananchi. Hivyo kwa uwingi wao CCM, maslahi ya serikali yamekuwa yakipewa kipaumbele zaidi kuliko maslahi ya Wananchi. Hii imepelekea wabunge wengi wa upinzani kutoridhika na maamuzi mbalimbali ya bunge.
WITO KWA UJUMLA
SPIKA
CUF tunataka spika ofisi ya Spika irudi kwenye misingi ya utawala wa haki na usawa katika kuliongoza bunge. Itikadi za Uccm zisitumike kuliongoza bunge bali utashi sahihi na nia ya dhati ya kutaka kuliongoza bunge ili liwatumikie Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao katika kulinda, kutetea na kuendeleza maslahi ya wananchi.
Spika lazima awabane mawaziri wa CCM watoe majibu makini na yaliyosahihi kwa hoja na maswali ya Wabunge bila woga wa aina yoyote.
WABUNGE
Wabunge lazima wajenge moyo wa kuvumiliana ili kufanikisha hoja bila ya matumizi ya ubabe, kebehi wala lugha ya matusi. Ikumbukwe kwamba wabunge wanapaswa kutumia muda mwingi kufikiri na kutafakari hoja na kuiwasilisha vizuri bila kutumia ubabe, matusi na utovu wa nidhamu.
CUF tunawataka wabunge ambao wameshindwa kufikiri kwa usahihi na kujenga hoja zenye nguvu na kuwasilisha kwa mbinu safi kwa watanzania bila kuvunja amani na kanuni za bunge ni bora warudi majimboni na kuvua ubunge ili wachaguliwe wengine wenye sifa na uwezo wa kutimiza majukumu ya kibunge.
Wabunge wanapaswa kufikiri kwa undani kero za wananchi wao na kuzipeleka bungeni na si maslahi ya vyama vyao.
Wabunge wanapaswa kuwa na moyo wa utaifa utakaowapelekea kwenye umoja katika kutetea maslahi ya Taifa bila kujali hoja imetolewa na chama gani.
Wabunge wabadilishe mtazamo kwamba bunge ni sehemu ya mashindano ya vyama vya siasa bali waone kwamba bunge ni mahali pa kupambana kati ya wawakilishi wa Wananchi dhidi ya unyonyaji na ukandamizaji wowote wa maslahi ya umma na si vita ya wao kwa wao.
SERIKALI
Serikali lazima sasa ibadilike katika namna ya kutoa majibu yake kwa wabunge. Kumekuwa na tabia ya mawaziri na manaibu mawaziri kutoa majibu mepesi kwa masawali magumu kutoka kwa Wananchi kupitia wawakilishi wao. Majibu mengi ya mawaziri yamekuwa ya juujuu na ambayo hayajibu maswali ya wanachi. Mbaya zaidi majibu ya mawaziri hawa yamekuwa mbali na kutojibu maswali ila yamekuwa yakiongeza maswali magumu zaidi kutoka kwa Wananchi.
Spika afanye kazi kwa uadilifu na awabane Mawaziri kujibu maswali ya Wabunge.
Katika Katiba Mpya pendekezo la CUF la Spika asiwe mbunge wa Chama chochote bali achaguliwe na Wabunge kutokana na watu wenye sifa watakaoomba nafasi ya kuwa Spika lizingatiwe.
2:MIKUTANO YA CUF MATUKIO YA UHARIBIFU WA MALI WILAYA YA LIWALE
Tarehe 17/04/2013 CUF-Chama cha Wananchi kilihitimisha Mikutano ya Hadhara Liwale Mjini. Mikutano hii inatokana na makubaliano baina ya Jeshi la Polisi na CUF-Chama cha Wananchi Wilaya ya Liwale kama sharti la kutofanya Maandamano. Baada ya kumalizika kwa Mikutano ya Hadhara ya Wilaya ya Liwale, siku sita baadae Viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika Wilaya ya Liwale, walienda kulipa Fedha za Korosho kwa Wananchi wa Liwale. Wananchi walikabidhiwa Tshs 200/= kwa kilo badala ya Tshs 600/= kama ilivyoahidiwa na kukubaliwa kwenye Mkataba wa Mauzo uliofanyika 2012. Hapo ndipo ilipoanza balaa na Maandamano yalioambatana na uharibifu wa Mali. Katika vurugu hizo zilizodumu kwa usiku mzima, Nyumba kadhaa ziliharibiwa ikiwemo za viongozi wa Vyama vya Ushirika na Viongozi wa Vyama vya Kisiasa,Mbunge na Madiwani.
CUF- Chama cha Wananchi kinaitaka Serikali kutatua tatizo hili la uuzaji wa Ufuta na Korosho katika utaratibu wa STAKABADHI GHALANI. Utaratibu wa STAKABADHI GHALANI unaoleta usumbufu na unaongeza umasikini kwa watu wa Mikoa ya Kusini na hatimae kuvuruga AMANI ya Mikoa hiyo.
CUF-Chama cha Wananachi kinaitaka Serikali kufanya utafiti wa Wafanyabiashara wa Korosho kupitia Vyama vya Ushirika ili kuweza kubaini ukweli wa madai ya kwamba Korosho za Mwaka 2012 hazijauzwa na ndio maana Serikali inashindwa kufanya malipo kwa wakati.
Mwisho CUF-Chama cha Wananchi kinaitaka Serikali kwa mara nyingine tena kuondosha UTARATIBU WA STAKABADHI GHALANI ili kutoa fursa kwa wakulima wa kusini kuuza mazao yao kwa mnunuzi wanaemtaka (kwa maana ya kuwepo kwa Soko Huria) ili kukuza kipato chao na kudumisha Amani ya Mikoa ya Kusini.
HAKI SAWA KWA WOTE
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti Taifa
About mahamoud
This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
0 comments:
Post a Comment