Mnadhimu wa jeshi la Israeli Lt. Jen. Benny Gantz |
Mnadhimu wa jeshi la Israeli amerejelea kauli za vitisho vya nchi yake dhidi ya Iran, akisema kuwa utawala huo unaweza kuivamia Iran bila kutaka msaada wowote kutoka nje.
Kiongozi huyo wa jeshi, Luteni Jenerali Benny Gantz aliyasema hayo katika mahojiano yake na redio moja ya umma Mashariki mwa al-Quds (Jerusalem) leo Jumanne, AFP imeripoti.
"Tuna mipango na dira yetu...muda ukifika tutaamua" juu ya kuchukua hatua ya kijeshi dhidi ya Iran, alisema.
Maneno kama hayo yaliwahi kusemwa na maafisa wengine wa Israeli, akiwem waziri mkuu Benjamin Netanyahu na Waziri Masuala ya kijeshi na vita Moshe Ya'alon.
Wakati huo huo, Netanyahu anasema kuwa vikawazo vinavyoongozwa na Marekani dhidi ya Iran kuhusu programu yake ya nishati ya nyuklia vinaweza visisaidie.
Ya'alon pia alisema kuwa programu ya nishati ya nyuklia ya Iran ndiyo tishio la hatari zaidi kwa dunia.
Marekani, Israel na washirika wao wengine wamekuwa wakiituhumu Iran kuwa ina malengo yasiyokuwa ya kiraia katika programu yake ya nyuklia huku utawala wa Israeli mara kwa mara ukitishia kuvishambulia vinu vya nyuklia vya Iran.
Iran imekuwa ikikanusha tuhuma hizo na kusema kuwa kama nchi mwanachama iliyosaini Mkataba wa kuzuia kuenea kwa silaha za Nyuklia (NPT) na kama mwanachama wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), ina haki ya kutumia teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani.
Aidha, IAEA imefanya ukaguzi kadhaa wa vinu vya nyuklia vya Iran lakini haijapata ushahidi unaoonesha kuwa programu ya nyuklia ya Iran imebadilishwa kuwa programu ya uzalishaji wa silaha za nyuklia.
Tofauti na Iran, Israel ambayo inaaminika kumiliki vichwa vya silaha za nyuklia baina ya 200 na 400, haijasaini mkataba wa NPT na imeendelea kukiuka miito ya kimataifa inayoitaka kusaini mkataba huo.
IMEANDALIWA NA MZIZIMA 24 KWA MSAADA WA MTANDAO
0 comments:
Post a Comment