MAALIM SEIF: HAKUNA UGAIDI ZANZIBAR




MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amepinga kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi kuwa mauaji ya viongozi wa dini Zanzibar ni ugaidi na kusema kuwa wanaofanya hivyo ni watu wenye nia ya kuvunja umoja wa Wazanzibari.

Baada ya mauaji ya Padre Evarist Mushi, akizungumza na wandishi wa habari,Nchimbi alielezea kusikitishwa na mauaji hayo akisema kuwa ni ya kigaidi na yana lengo la kuingiza nchi katika machafuko. Amesema kuwa tukio hilo si tukio la ujambazi bali tukio la kigaidi kwani limelenga zaidi katika kuwashambulia viongozi kidini.

Watu hawa wameamua kuyatumia matukio ya kuuawa na kujeruhiwa kwa viongozi wa kidini ili kuvunja umoja wa Wazanzibari, lakini nasema hakuna ugaidi Zanzibar,” alisema Maalim Seif juzi usiku alipohutubia kwenye hafla ya Maulid mjini Kiuyu, Wilaya ya Wete, Kaskazini Pemba.

Alisema inasikitisha kuona wapo baadhi ya viongozi wenye nia chafu dhidi ya Zanzibar wenye tabia ya kutoa kauli za kujenga chuki na fitina miongoni mwa Wazanzibari chini ya kivuli cha matukio hayo.

Makamu huyo wa Kwanza wa Rais alisema, kinachoonekana kuna ajenda imetayarishwa ya kutaka kulazimisha chuki za kidini Zanzibar,

Aliwataka wananchi wote wa Zanzibar hivi sasa kuwa macho na ajenda zinazolengwa kuwavuruga na waendelee kuishi kwa mshikamano na umoja kama ambavyo wamekuwa wakiishi.

Maalim Seif alisema vitendo vya kuuawa na kujeruhiwa viongozi wa kidini Zanzibar ni mambo mageni na kwa miaka mingi Zanzibar imekuwa ni mfano bora wa uvumilivu wa kiitikadi za kidini, licha ya kuwa asilimia 98 ya wananchi wake ni Waislamu.

Alisema Katiba ya Zanzibar imeweka wazi haki ya mtu kuabudu kwa mujibu wa imani yake na uhuru wa mtu kuabudu umelindwa.

Hata hivyo, Maalim Seif alisema inasikitisha kuona wakati Rais Jakaya Kikwete katoa maelekezo uchunguzi wa kina ufanyike na Kamishna wa Polisi Zanzibar ameshaweka wazi kuwa uchunguzi unaendelea, baadhi ya viongozi na vyombo vya habari vinachochea chuki za kidini na kusema kuwa Zanzibar kuna ugaidi.
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment