JUMLA ya wanafunzi 12 wa Shule ya Sekondari Kingani wilayani Bagamoyo, wameshindwa kuendelea na masomo yao ya elimu ya sekondari, baada ya kupata ujauzito muda mfupi baada ya kuchezwa unyago.
Taarifa hizo zilitolewa jana na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Magomeni, Omary Kakombe, wakati akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada kwa wanafunzi watano wa Kitongoji cha Nia Njema A wilayani hapa.
Kakombe alisema kuwa, wanafunzi hao walipata ujauzito baada ya kuchezwa ngoma ya unyago wakiwa shuleni na hivyo kuanza harakati za mapenzi na kushika ujauzito.
“Ni jambo la fedheha na la kusikitisha wazazi wenzangu kwani Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa za kuhakikisha kuwa watoto wote wanaotakiwa kupata elimu wanasaidiwa kufanya hivyo, lakini hali ni tofauti kwa wazazi wa Bagamoyo,” alisema.
Alisema kuwa mara baada ya kugundulika kuwa na ujauzito wanafunzi walipohojiwa na viongozi wa Serikali ya kata walieleza kuwa wamepata mimba hizo kutokana na hamu waliyokuwa nayo ya kutaka kujaribu mambo waliyofundishwa wakiwa unyagoni.
Alisema kuwa, wakazi wengi wa wilaya hiyo wamekuwa wakikataa kupeleka watoto shule kwa madai kuwa hawana uwezo, lakini inapofika wakati wa ngoma wanakuwa radhi hata kuchangishana michango ili kuwacheza ngoma.
“Wengi wao sisi viongozi wa Serikali tukiwaambia wanahoji mbona hata Rais Kikwete kawacheza watoto wake lakini ni tofauti Rais yeye kawacheza watoto wake mara baada ya kuhitimu masomo yao ya kidato cha sita.
“Hivyo utaona umuhimu wa mila ulikuwapo lakini kasubiri watoto wake wahitimu masomo yao kwanza ndio wachezwe, lakini wao wanakatisha masomo ya watoto hii ni tofauti,” alisema Kakombe.
Akizungumzia hatua ya wakazi hao wa Kitongoji cha Nia Njema A kujichangisha fedha kwa ajili ya kuwasaidia watoto waliopo katika mazingira hatarishi, Kakombe alisema hatua hiyo inapaswa kuigwa na kuungwa mkono na jamii yote ya wakazi wa Bagamoyo.
Akizungumzia kuhusiana na michango hiyo Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Hassan Ramadhanina na katibu wake Maganga Mohamed, walisema fedha hizo za ada pamoja na vifaa mbalimbali vya shule vimetolewa kwa jumla ya wanafunzi watano ambao wamechaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza wilayani humo.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya hiyo, Ahmed Kipozi amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani kwake haitakuwa na simile na mzazi au mtu yeyote atakayebainika kuhusika na kupata ujauzito kwa mwanafunzi.
Akizungumza na gazeti hili ili kujua hatua zilizochukuliwa na Serikali wilayani humo, Kipozi alisema Serikali inafuatilia kwa karibu tatizo hilo na kwamba imefikia katika hatua za mwisho za uchunguzi wake.
CHANZO: MTANZANIA
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment