PRESHA YAZIDI KUPANDA GESI YA MTWARA

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, amesema wanasiasa wanaopinga suala la gesi ya Mtwara kusafirishwa kwenda Dar es Salaam, hawatumiki na mataifa ya nje kutaka kuvuruga nchi.

Zitto alisema hayo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, ambapo alisema Serikali haitashinda vita ya kung’ang’ania kujenga bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam. 

Alisema Serikali lazima ijitazame yenyewe na bila kufanya hivyo, wananchi wataendelea kupigania haki yao kwa kuwa hii ni vita ya uwajibikaji. 

“Wananchi wanataka kufaidika na rasilimali za nchi yao. Kwa vyovyote vile upande wa wananchi utashinda. Vita ya uwajibikaji katika rasilimali za nchi si ya vyama vya siasa, ni vita ya wananchi,” alisema na kuongeza: 

“Chama cha siasa kitakachokwenda kinyume na matakwa ya wananchi, kinajichimbia kaburi chenyewe.

“Kwa wiki ya tatu mfululizo kumekuwa na malumbano kuhusiana na suala la ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Kumekuwa na madai yenye nguvu ya hoja kutoka kwa wananchi wa Mtwara dhidi ya porojo kutoka kwa viongozi wenye dhamana ya kujibu madai haya ya watu wa Mtwara. 

“Watu wa Mtwara kwa umoja wao na kwa kuungwa mkono na viongozi wa dini zote wamekuwa wakitaka Serikali ifikirie upya suala la mradi wa ujenzi wa Bomba la gesi na badala yake kujenga mitambo ya kufua umeme mkoani Mtwara na kusafirisha umeme huo kwenda maeneo mengine ya nchi.”

Alisema watu wa Mtwara wanatekeleza matakwa hayo ya Katiba kwa kukataa mrundikano wa shughuli za kiuchumi wa nchi na utajiri wa nchi kuwa katika mikoa michache na hasa Dar es Saalam.

Alisema Serikali iliyokosa uhalali wa kutawala ndio inaweza kudharau hisia za wananchi wa Mtwara.

“Serikali ielewe kwamba kamwe haitaweza kulinda kila nchi ya bomba hili iwapo italijenga kwa nguvu. Badala ya kuzungumza na vyombo vya habari Serikali ifanye mazungumzo na wananchi wa Mtwara na kukubaliana na matakwa yao. 

“Kitendo cha Serikali kung’ang’ania msimamo wake dhidi ya watu wa Mtwara, ni kitendo kinachoweza kuipasua nchi na hivyo kwenda kinyume na masharti ya Katiba ibara ya 28 ambayo inasema kila raia ana wajibu wa kulinda uhuru wa nchi, mamlaka na umoja wa Taifa,” alisema Zitto.

Alisema inawezekana Serikali inaogopa kuvunja makubaliano na Wachina ya mkopo wa Dola bilioni 1.2 za Marekani ambao imeuingia bila hata kushirikisha Bunge. 

Alisema inawezekana Serikali na hasa watendaji wa Serikali waliojadili mkopo huo wameshapata chao na hivyo kuogopa kusikiliza madai halali ya wananchi. 

“Lakini yote hayo hayawezi kuwa zaidi ya umoja wa nchi yetu. Hatuwezi kukubali nchi yetu ipasuke vipande vipande kwa sababu tu ya kulinda mkataba wa bilioni 1.2 tuliokopa China, ambayo Serikali inang’ang’ania.

“Tunafahamu kwamba ubalozi wa China umeandika barua serikalini kuwaondoa raia wa China waliopo Mtwara kwa hofu ya maisha yao. 

“Serikali inaficha ukweli huu kama ilivyoficha ukweli kwamba Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alifukuzwa na wananchi wa Mtwara alipokwenda hivi majuzi. Serikali itaficha ukweli hadi lini? Lazima tupate majibu,” alisema Zitto.

Alisema Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ilipokuwa inapitia hesabu za Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), iliomba mkataba na kwa mshangao mkubwa wabunge wakaambiwa mkataba haupo TPDC bali upo wizarani. 

“Kwanini mkataba huu wa matrilioni ya fedha unafichwa? Mkataba huu ulisainiwa pamoja mikataba mingine miwili, mmoja wa kujenga nyumba za wanajeshi wa thamani ya Dola milioni 400 za Marekani 400 na mwingine wa mawasiliano jeshini wa Dola milioni 110 za Marekani na mikataba yote mitatu imesainiwa kimya kimya bila kushirikisha wananchi kupitia Bunge. Lazima mikataba yote hii iwekwe wazi.

“Mkataba huu uchunguzwe kama unalingana na thamani ya fedha maana kwa utafiti wa awali inaonyesha kuwa, bei ya ujenzi wa bomba imepandishwa maradufu. 

“Wastani wa kujenga bomba la gesi duniani ni Dola milioni 1.2 za Marekani kwa maili moja. Mradi huu wa Tanzania utagharimu Dola milioni 2.2 za Marekani kwa kilomita moja (maili moja ni sawa na kilomita 1.6),” alisema Zitto.

Alisema Serikali ibadilishe mkataba huu kuwa wa mkopo wa kujenga mitambo ya kufua umeme Mtwara na ujenzi wa msongo wa umeme kama gridi ya pili ya Taifa. 

“Ni dhahiri kwamba kwa usalama wa Taifa na hata kwa gharama nchi itafaidika zaidi kwa kujenga gridi nyingine kutokea Mtwara badala ya kusafirisha gesi kuja Dar es Salaam.

Wakati huo huo, Mbunge wa Kigamboni Dk. Faustine Ndugulile (CCM), ameibuka na kuitaka Serikali kutodharau madai ya wananchi wa mikoa ya kusini kuhusu sakata la gesi.

Hatua hiyo ya mbunge huyo imekuja siku chache baada ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara kufanya maandamano ya amani kupinga ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka mkoani humo kwenda jijini Dar es Salaam.

Dk. Ndugulile, alisema suala hilo lina sura mbili tofauti ambazo zote zina hoja za msingi ikiwemo umaskini wa mikoa ya kusini pamoja na tatizo la ajira kwa vijana.

Kutokana na hatua hiyo mbunge huyo ameitaka Serikali ijitokeza kueleza vigezo vilivyotumika kuamua kujenga bomba la gesi, ili kusafirisha rasilimali hiyo kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

“Nimefuatilia kwa makini kuhusu hoja ya wananchi wa Mtwara, lakini vile vile nimefuatilia kwa makini majibu yanayotolewa na viongozi mbalimbali wa Serikali. 

“Kinachoonekana hapa ni kwamba, viongozi hawajajipanga vizuri kuhusiana na suala hili, kila mtu anasema lake na kila mtu anafanya lake.

“Kwa mtazamo wangu, katika sakata hili kuna mambo mawili makubwa ya msingi Mosi, maendeleo duni katika mikoa ya Kusini ikiwa ni pamoja na Mtwara. Pili, tatizo la ajira kwa vijana.

“Haya ndio mambo ya msingi na kinachohitajika ni kutoa elimu ya kutosha itakayolenga kuwashibisha wananchi wa Mtwara jinsi gani watanufaika kimaendeleo na kwa upande wa ajira kwa vijana,” alisema Dk. Ndugulile

Mbunge huyo alionya na kusema kuwa, hatua ya kuwabeza wananchi hao na kutumia hoja za nguvu havitasaidia na badala yake inahitaji nguvu ya hoja zitakazowaelimisha na kuwashawishi wananchi wa Mtwara.

“Moja ya maeneo muhimu ni Serikali iseme ni vigezo gani vilitumika kufikia maamuzi ya kujenga bomba la gesi toka Mtwara hadi Dar es Salaam? Kwa nini mtambo wa kuzalisha umeme usijengwe Mtwara na kusambazwa kuja Dar es Salaam? Je mchanganuo wa gharama ukoje?

“Je upatikanaji wa gesi hii utakuwa na manufaa gani kwa wananchi wa eneo husika? Je kutakuwa na viwanda vya kusindika gesi vitakavyojengwa huko Mtwara?

“Je mikoa inayozalisha itapata asilimia ya mapato ya gesi inayozalishwa katika eneo hilo? na je, ajira ngapi zitakazozalishwa na sekta hii, na asilimia ngapi ya ajira zitakuwa kwa ajili ya wakazi wa eneo hili?,” alisema na kuhoji mbunge huyo.

Alisema kutokana na hali hiyo mbunge huyo amezishauri pande zote mbili kuhakikisha suala hilo linashughulikiwa mapema na kwa haraka wakati likiwa bado ni kipele.

“Tatizo likishakuwa jipu au kansa, gharama za kulishughulikia zitakuwa kubwa sana. Wananchi kuhoji si dhambi wala uhaini.

“Uelewa wa wananchi umekuwa, wanahitaji kushirikishwa na kupewa majibu ya kina. Tuzibe ufa sasa hivi lasivyo tutajenga ukuta,’’ alisema.

CHANZO: MTANZANIA
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment