Mwandishi auawa katika mazingira ya kutatanisha


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai. 


MWANDISHI wa Habari wa Kituo cha Redio Kwizera wilayani Kakonko, Mkoa wa Kigoma, Issa Ngumba (45), ameuawa kwa kupigwa risasi na kunyongwa na watu wasiofahamika.
Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa mwili wa mwandishi huyo ulikutwa porini, siku tatu tangu alipotoweka nyumbani kwake katika mazingira ya kutatanisha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai alithibitisha tukio hilo, lakini akasema asingeweza kulizungumzia kwa undani kwa kuwa polisi walikuwa bado eneo la tukio.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamesema mwandishi huyo alikutwa jana akiwa amekufa, huku mwili wake ukiwa na majeraha ya risasi na ukiwa umenyongwa na pembeni yake kulikuwa bastola iliyokuwa imetelekezwa pamoja na simu zake mbili za mkononi.
“Mwili wake ulipatikana jana katika Pori la Mlima Kajuluheta ulioko katika Kijiji cha Muhange, Kakonko asubuhi baada ya wananchi kufanya msako wa siku tatu tangu Jumapili iliyopita ikiwa ni siku moja baada ya kupotea katika mazingira ya kutatanisha,” alisema mmoja wa  mashuhuda hao.
Imeelezwa kuwa pamoja  na vifaa hivyo, pia katika eneo hilo la tukio kulikutwa risasi tano na katika mfuko mmoja wa suruali ya marehemu, kulikuwa na noti moja ya Sh10,000.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Kigoma (KPC) Deogratius Nsokolo alisema: “Sisi ndiyo kwanza tunaelekea eneo la tukio, lakini waandishi wa Wilaya ya Kibondo ambao waliwahi kufika eneo la tukio na kushuhudia uchunguzi wa daktari, wameeleza kuwa marehemu amekufa kwa kunyongwa na kupigwa risasi mkono wa kushoto.”
“Tunaelekea Wilaya ya Kakonko kutoka Kigoma Mjini, lakini daktari amesema maiti inaonekana kunyongwa shingo na kupigwa risasi mkononi.”
Alisema mwili huo ulifanyiwa uchunguzi na daktari Primus Ijumaa wa Hospitali ya Wilaya ya Kibondo.
Kamanda Kashai alisema jeshi lake linasubiri taarifa ya daktari aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu pamoja na taarifa za awali za uchunguzi kabla ya kutoa taarifa kamili kwa waandishi wa habari.
Naibu Mhariri wa Kituo cha Redio Kwizera kinachorusha matangazo yake kutoka wilayani Ngara mkoani Kagera, Seifu Upupu alisema mwandishi huyo alipotea tangu Januari 5, mwaka huu saa kumi na moja jioni.
“Simu zake zilikuwa zikiita bila kupokewa kwa muda wote na hadi jana (juzi) zikawa hazipatikani kabisa,’ alisema Upupu na kuongeza:
“Maelezo kutoka kwa mke wake, Rukia Yunus ni kwamba marehemu aliondoka nyumbani kwake jioni na kumuaga mkewe kuwa alikuwa akienda madukani (center), lakini tangu hapo hakurudi wala kuonekana tena. Ilipofika Jumapili, Serikali ya kijiji ilianzisha msako kwa ajili ya kumtafuta hadi jana (juzi), asubuhi walipoukuta mwili wake porini.”
Utendaji wa kazi
Akizungumzia utendaji kazi wa mwanahabari huyo, Upupu alisema: “Habari ya mwisho ambayo marehemu aliiandika ilikuwa ni Novemba 24, mwaka jana. Ilikuwa ni habari ya tukio la mfugaji mmoja aliyedaiwa kumla nyama mchungaji wake aliyetajwa kwa jina moja la Susuruka na kumjeruhi vibaya sehemu za usoni.”
Upupu alieleza kuwa katika habari hiyo, mwandishi alieleza kuwa Susuruka alijeruhiwa kwa kuliwa nyama za uso wake na mwajiri wake aliyekuwa akimfanyia kazi ya kuchunga ng’ombe katika Kijiji Muhange.
“Baada ya taarifa ile, Jeshi la Polisi likamkamata mfugaji huyo na tayari limemfikisha mahakamani,” alisema.
Upupu alisema kabla ya kumla nyama za usoni mfugaji huyo, alimuua mbwa wake na kula ulimi wa mbwa huyo. Majeruhi amepelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo kwa matibabu.
CHANZO: MWANANCHI
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment