RAIS BOZIZE: SING'OKI NG'O


Central African president Francois Bozize speaks during a news conference at the presidential palace in Bangui January 8, 2013. (REUTERS/Luc Gnago)
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Francois Bozize Yangouvonda akizungumza wakati alipokutana na waandishi wa habari katika ikulu ya Rais mjini Bangui jana Januari 8, 2013. 


Rais Francois Bozize Yangouvonda wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, alikataa kufikiria wazo la kuachia madaraka kama ilivyotakiwa na waasi ambao wametuma wajumbe kwenda Gabon kwa ajili ya mazungumzo ya amani.

“Sitaki kuzungumzia suala la kuondoka," alisema akijibu suali aliloulizwa katika mkutano wake na wanahabari mjini Bangui waliotaka kujua kama alikuwa tayari kukubali masharti na matakwa ya waasi.

“Je, waasi wanawawakilisha watu wa Afrika ya Kati? Sihitaji kuzungumzia nafasi ya mkuu wa nchi," aliongeza Bozize huku akiwaita waasi kuwa ni "magaidi mamluki."

Alisema kuwa waasi hao wanaonekana kuwa ni wapiganaji wa Janjaweed -- kutoka katika jimbo la magharibi mwa Sudan la Darfur -- wakiwa sambamba na "watu wasiozungumza lugha ya Sango (lugha ya kwanza ya Jamhuri ya Afrika ya Kati), Kifaransa, au hata Kiingereza," na wanatoka nchi nyingine.

Vile vile, BozizĂ© alizungumzia kuhusu mazungumzo ya amani yaliyopangwa kuanza wiki hii katika mji mkuu wa Gabon, Libreville. 
"Iwapo magaidi watakuja kuzungumzia ugaidi, dunia itajua... Wakija kuzungumzia kulinda maslahi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, tutawasikiliza. Kama kuna kitu kizuri, tutakikubali. Kama ni unyang'anyi wa sialaha, hatutaukubali," alisema Bozize.


Siku ya Jumatatu, wajumbe kutoka pande zote mbili walipangiwa kuwasili Gabon, lakini ndege ya maafisa wa Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati haikuondoka Bangui kama ilivyokuwa imepangwa kutokana na "tatizo la kiufundi."

Hata hivyo, ujumbe wa waasi wa Seleka uliwasili Gabon siku hiyo ya Jumatatu.

Pamoja na hayo, licha ya uamuzi wa waasi kushiriki mazungumzo ya kusaka amani, siku hiyo hiyo msemaji wa kundi hilo, katika mahojiano mjini Paris, alisema kuwa kundi lake bado lina uwezo wa kuuteka mji wa Damara au Bangui lakini linaangalia usalama wa raia 700,000 wanaoishi katika mji huo.

"Tungetaka kuuchukua mji wa Damara, tungekuwa tumeshafanya hivyo. Tuna uwezo wa kuuchukua mji wa Damara na pia mji wa Bangui leo leo, lakini hatutaki mji mkuu upatwe na zahama ya mashambulizi," alisema Eric Massi. 

Hata hivyo, rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati alisema, “Magaidi wa kigeni wanaishambulia mamlaka halali katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Katika mazingira hayo, ninajivunia kuwa nimeitumikia nchi yangu vizuri, kwamba demokrasia inafanya kazi vizuri."

Waasi wa Seleka walianzisha mashambulizi dhidi ya serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati mwezi Desemba.

Waasi wamekuwa wakisonga mbele kuelekea mji mkuu Bangui, wakisema kuwa Rais  Francois BozizĂ© Yangouvonda lazima aachie madaraka. 

Katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kuna rasilimali nyingi za madini, ikiwemo dhahabu na almasi. Hata hivyo, nchi hiyo, kama ilivyo kwa nchi nyingi za Kiafrika, inaogelea katika umaskini wa kutisha na imekuwa ikikabiliwa na mfululizo wa matukio ya uasi tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1960 kutoka kwa Ufaransa.




Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment