Mgogoro Jamhuri ya Afrika ya Kati: Vita ya Maneno Yazidi kupamba moto

Central African president Francois Bozize speaks during a news conference at the presidential palace in Bangui January 8, 2013. (REUTERS/Luc Gnago)
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Francois Bozize




Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na kundi la waasi la Seleka wanafanya mazungumzo ya kutafuta amani nchini Gabon, lakini pande zote zinaonekana kushikilia misimamo yao.

Waasi wamemtaka Rais Francois Bozize kuondoka madarakani na ashitakiwe katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu kwa kudaiwa kutenda jinai mbalimbali za kivita, ikiwa ni pamoja na "kuwasikilia na kuwafunga watu bila hatia, kuwapoteza, kuwaua na kuwanyonga."

Maneno hayo yamekuja siku moja baada ya Bozize kuwatuhumu waasi hao kuwa ni "magaidi mamluki" wanaoungwa mkono kutoka nje.

Mazungumzo hayo ya pande tatu baina ya Serikali, waasi na vyama vya upinzani yanasimamiwa na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Katikati mwa Afrika (ECCAS) mjini Libreville, nchini Gabon.

Mazungumzo yalitarajiwa kujikita kwenye makubaliano ya amani yaliyosainiwa mjini Bangui kati ya mwaka 2007 na 2011, ambayo waasi wanasema yalikiukwa.

"Ninataka kila mtu kuonesha hali ya kujizuia, na kwa muktadha huo, mwanzo wa mazungumzo tutapendekeza yasainiwe makubaliano ya kusitisha mapigano," alisema Basile Ikouebe, waziri wa mambo ya nje wa Congo, ambayo ndiyo inayosimamia mazungumzo hayo.

'KIPINDI CHA MPITO'

Kundi la Seleka, ambalo ni mwamvuli wa makundi mbalimbali ya waasi, lilianzisha mashambulizi yake katika eneo la kaskazini tarehe 10 Desemba na wameitwaa  miji kadhaa katika eneo la kaskazini la nchi hiyo.

Bozize amekuwa akitegemea msaada wa kijeshi kutoka nje katika kuzima mfululizo wa matukio madogo madogo ya uasi. Mara hii nchi za eneo hilo,hasa Chad, zimetuma mamia ya wanajeshi kwenda kulisaidia jeshi lake.

Waasi walikuwa wakielekea upande wa kusini mahali ulipo mji mkuu Bangui, lakini walisimama karibu kilometa 160 baada ya mataifa jirani kutuma wanajeshi kwenda kulisaidia jeshi la serikali.

Vyama tisa vya upinzani vinavyoshiriki mazungumzo hayo navyo vimetaka rais aondoke madarakani, vikimtuhumu kuwa aliiba kura katika uchaguzi wa mwaka 2005 na 2011 na kwamba anaigawa nchi.

"Kujiuzulu kwa Rais Bozize na kuanzishwa kwa kipindi cha mpito ni sharti la msingi katika kumaliza mgogoro huu," vilisema vyama hivyo katika tamko lao la pamoja.

Vilevile walitaka kusitishwa kwa katiba na kuteua serikali na bunge la mpito itakayohudumu kwa muda usiozidi  miaka mitatu na kisha utaitishwa uchaguzi.  Bozize ametaka amalizie kipindi chake ambacho kitafikia ukomo mwaka 2016, na ameahidi kutogombea tena.

Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment