Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Zambia cha Movement for Multi-party Democracy (MMD) leo Jumatano amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za ufisadi.
Timu ya pamoja ya uchunguzi iliyoundwa na serikali imemshtaki Nevers Mumba kwa ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka alipokuwa Balozi wa Zambia nchini Canada.
Mumba anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya kiasi cha dola 123,840 zilizotolewa msaada na Kampuni ya Barrick Gold Corporation kwa serikali ya Zambia.
Vilevile anashutumiwa kutoa kandarasi zinazokadiriwa kuwa na thamani ya dola 34,550 kinyume na sheria, ambapo waendesha mashitaka wameeleza kuwa hayo ni matumizi mabaya ya ofisi.
“Tumesikitishwa na kushangazwa sana kwamba sasa serikali inaweza kufikiria kuzua mashtaka dhidi ya Dr. Mumba,” alisema Chembe Nyangu, naibu katibu mkuu wa chama cha MMD.
“Hii ni kesi yenye mkono wa kisiasi,” alisema Nyangu.
Wafuasi wa MMD wanasema kuwa mashitaka dhidi ya Mumba ni hatua nyingine ya chama tawala cha Patriotic Front (PF) kujaribu kuufuta upinzani.
“Wazo la kumkamata linalenga kuidhoofisha MDD,” Nyangu alisema. “Kwa kweli tusipokuwa na kiongozi hatuwezi kufanya kazi. Hivyo wanataka kumdhoofisha kila anayeipa changamoto Patriotic Front.”
Hata hivyo, wafuasi wa PF, wanasemakuwa mashitaka hayo yanaonesha kuwa serikali inajaribu kutekeleza ahadi yake ya kumaliza ufisadi.
Nyangu alionya kuwa kuendelea kuwasumbua na kuwadhalilisha viongozi wa upinzani kunaweza kuibua wasiwasi na kuzusha vuruğu.
“Hili halipaswi kuendelea, kwa sababu litaleta matatizo mengi nchini, kwa sababu watu wetu wataibuka na kuanza kupambana na serikali,” alisema Nyangu.
Nyangu anasema viongozi wa chama watakutana hivi karibuni kuamua kinachoendelea.
“Tutapaswa kukaa kama kamati ya Utendaji na kuamua nini cha kufanya na jinsi tunavyoweza kumsaidia kiongozi wetu na kuijadili kadhiahiyo pamoja na wanachama wetu kuangalia kama tuko salama kamachama,” alisema.

0 comments:
Post a Comment