
Waasi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wameutwaa mji wa kusini wa Alindao takriban kilometa 100 kutoka kwenye mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hayo yalithibitishwa na msemaji wa Serikali.
Hatua hiyo inatokea leo Jumamosi baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwataka waasi wasitishe mashambulizi na waondoke katika miji mingine waliyoiteka hapo mwanzo.
"Kuna uhakika mkubwa wa uwepo wa waasi katika eneo hilo [Alindao] na hakuna upinzani wowote kutoka upande wa vikosi vya serikali," anasema mwandishi wa al-Jazeera, Andrew Simmons, wakati akiripoti kutoka mji mkuu, Bangui.
"[Wanajeshi wa Serikali] wamelikimbia eneo hilo, hata baada ya majeshi ya kigeni kuja kuliunga mkono jeshi la serikali."
Baraza la Usalama lilisema katika ripoti yake kuwa hatua ya waasi kusonga mbele "inazorotesha sana" usalama na uthabiti wa nchi, na ni "kitisho kwa raia na kinakwaza shughuli za utioaji wa huduma za kibinaadamu."
Waasi hao wanaomtaka Rais Francois Bozize ajiuzulu wameiteka miji kadhaa ndani ya mwezi mmoja, lakini walisitisha harakati ya kuelekea mjini Bangui Desemba 29 wakisubiri hatua ya mazungumzo.
Baraza la Usalama limezitaka pande zote kutafuta suluhu ya amani na kuanza mazungumzo yaliyopangwa kufanyika mjini Libreville, nchini Gabon, kuanzia Jumanne "bila masharti yoyote na kwa nia njema".
Aidha, Baraza la usalama limeihimiza serikali, makundi yenye silaha, vyama vya upinzani na pande zote zenye kuhusika kutumia mazungumzo hayo "kujadili suluhisho la maana la kisiasi".
MAANDALIZI YA MAZUNGUMZO
Balozi wa Pakistan katika Umoja wa Mataifa, Masood Khan, ambaye ndiye rais wa sasa wa baraza na ambaye alisoma waraka huo, aliulizwa iwapo kweli mazungumzo hayo yatafanyika kwa kuwa hakuna uhakika kama waasi na makundi yote yatashiriki.
"Kwa sasa maandalizi yanafanyika na tunataraji kuwa mazungumzo yatafanyika, na pande zote zimetakiwa kufanya hivyo," alisema Khan.
| "Mazungumzo haya ni muhimu ili kupunguza wasiwasi, kutuliza hali ya mambo na kutafuta suluhisho la kidiplomasia." Muungano wa waasi wa Seleka, ambao una maana ya "umoja" kwa lugha ya Sango, unaundwa na makundi manne tofauti ambayo zamani yaliwahi kupigana. Bozize aliahidi kuuunda serikali ya umoja wa kitaifa lakini waasi wanahoji nia yake hiyo na wanamtaka aachie madaraka. Vilevile, waasi wanaitaka serikali kuheshimu makubaliano ya amani yaliyowahi kufanyika huko nyuma ambayo yanataka kuweka silaha chini na kuwaingiza waasi wa zamani katika maisha ya kiraia ndani ya jamii. Baraza limeelezea wasiwasi wake kuhusu utekaji, uporaji na kuyalenga makundi ya jamii za wachache na pia kuwapa mafunzo na kuwatumia watoto katika mapambano. Wanachama wa baraza hilo wamezitaka pande zote kusitisha mashambulizi dhidi ya raia na kuheshimu haki za binaadamu huku likisema kuwa wale watakaohusika watawajibishwa. Siku ya Ijumaa, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika masuala ya watoto, lilisema kuwa limepokea "ripoti za kuaminika kuwa makundi ya waasi na wapiganaji wanaoiunga mkono serikali wanaendelea kuwapa mafunzo watoto na kuwaingiza katika mapambano." Jamhuri ya Afrika ya Kati ni nchi maskini sana ambayo imeathiriwa na matukio kadhaa ya uasi tangu ilipopata uhuru wake kutoka kwa Wafaransa. Rais Bozize mwenyewe aliingia madarakani mwaka 2003 kupitia mapinduzi yaliyoungwa mkono na vikosi vya Chad na tokea wakati huo amekuwa akishinda chaguzi mbalimbali. Anasema kuwa hataondoka madarakani mpaka atakapomaliza muhula wake mwaka 2016. Licha ya utajiri unaopatikana katika nchi hiyo, kama vile dhahabu, almasi, misitu na madini ya Urani, serikali imeendelela kuwa ombaomba. Vilevile masaibu ya nchi hiyo yamekuwa yakihusishwa na kuwa karibu na nchi zenye migogoro mingi, kama vile jimbo la Darfur nchini Sudan. Kundi la Uasi kutoka Uganda la Lord's Resistance Army limetumia udhaifu wa serikali kukimbilia katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambapo huwashambulia na kuwateka raia bila upinzani wowote. CHANZO: AL-JAZEERAH NA MASHIRIKA MBALIMBALI YA HABARI. |
0 comments:
Post a Comment