![]() |
| MFALME ABDULLAH WA SAUDI ARABIA |
Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia amewateua wanawake 30 kuingia katika Baraza la Shura ambalo hapo mwanzo lilikuwa limetawaliwa na wanaume tu. Mabadiliko hayo yametangazwa katika amri ya kifalme iliyochapishwa leo Ijumaa.
Amri hiyo iliyochapishwa na shirika la habari la Saudi Arabia, inawapa wanawake asilimia 20 ya viti katika Baraza la Shura, ambalo huteuliwa na Mfalme kumshauri katika masuala ya sera na sheria.
Amri moja imeweka mabadiliko katika sheria ya baraza ili kuwapa wanawale uwakilishi wanawake huku nyingine ikiteua wajumbe 150, kati yao 30 ni wanawake.
Mfalme Abdullah amechukua uamuzi huo baada ya kushauriana na viongozi wa kidini.
Maagizo hayo yameeleza kuwa wanaume na wanawake watakaa tofauti ndani ya Baraza, ambapo wanawake watawekewa eneo maalumu na wataingia kupitia mlango maalumu ili kuepusha mchanganyiko wa jinsi hizo mbili.
Mfalme Abdullah amekuwa akichukua hatua za mabadiliko, ambapo amesharuhusu kufanyika kwa chaguzi za manisipaa mwaka 2005 kwa mara ya kwanza nchini Saudi Arabia.
Mwaka 2011 aliwapa wanawake haki ya kupiga kura na kugombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka 2015.
Wakati akitangaza mabadiliko, pia alisema kuwa alikuwa akipanga kuwateua wanawake kuingia katika Baraza la Shura, yaani Bunge.
CHANZO; /www.dailystar.com.lb

0 comments:
Post a Comment