![]() |
| Waasi wa kundi la M23 wakiwa msituni katika jimbo la Kivu ya Kaskazini nchini Kongo. |
Wizara ya fedha ya Marekani inasema kuwa inawawekea vikwazo viongozi wawili wa vuguvugu la Machi 23 (M23), ambalo lilijipa utawala katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Siku ya Jumanne wizara hiyo iliwatuhumu Baudoin Ngaruye na Innocent Kaina kuwa wanawatumia watoto kama askari.
Ilisema kuwa watu hao wameadhibiwa kwa "kuhusika katika kuwaandaa na kuwatumia watoto kama askari katika mgogoro wa DRC na kwa kuwa viongozi wa kundi linalokwamisha mpango wa kuweka silaha chini, usuluhishi au kuwatuliza wapiganaji."
Vilevile ilimtuhumu Ngaruye kwa kuwalenga watoto kwa “kuwaua, kuwatesa na dhulma za kingono.”
Wataalamu wa Kinshasa na wale wa Umoja wa Mataifa, wanasema kuwa Rwanda inawasaidia, kuwaunga mkono na kuwapa amri waasi wa M23, ambao wanaimarisha udhibiti wao katika majimbo ya Kivu ya Kaskazini na Kivu ya Kusini mashariki mwa Kongo na wanaweza kutishia vikali udhibiti wa serikali ya Kongo katika eneo hilo.
Waasi wa M23 walijiondoa katika jeshi la Kongo mwezi Aprili wakipinga kile kinachodaiwa kuwa ni muamala mbaya waliokuwa wakifanyiwa katika Jeshi la Kongo (FARDC). Awali waasi hao walikuwa wamejumuishwa katika jeshi la serikali chini ya mkataba wa amani uliosainiwa mwaka 2009.
Tangu mwezi wa Mei, zaidi ya watu 900,000 wameyakimbia makazi yao katika eneo la mashariki mwa Kongo. Wengi wao wameweka makambi ndani ya Kongo, lakini makumi kwa maelfu walivuka mpaka na kuingia katika nchi jirani za Rwanda na Uganda.
Eneo la mashariki mwa Kongo limekuwa likikabiliwa na mlolongo wa machafuko tangu mwaka 1998, na zaidi ya watu milioni 5.5 wameuawa katika vitavilivyodumu kwa miaka 14.

0 comments:
Post a Comment