KENYA YAWATAKA WAKIMBIZI KUREJEA KAMBINI
Serikali ya Kenya imeamuru makundi ya maelfu ya wakimbizi wanaoishi katika maeneo ya mjini nchini humo kurudi katika kambi za zamani na zenye msongamano mkubwa wa watu. Taarifa rasmi iliyotolewa jana na serikali ya Kenya imeeleza kuwa watu wote wanaotafuta hifadhi na wakimbizi kutoka Somalia wanapaswa kuripoti katika kambi za Daadab, na raia kutoka nchi nyingine wanaotafuta hifadhi pia wanapaswa kuripoti katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma. Serikali imetoa agizo hilo baada ya maeneo ya Kenya ya kaskazini mashariki yanayokaliwa na Wakenya wenye asili ya Kisomali pamoja na mji mkuu wa nchi hiyo Nairobi kukumbwa na mashambulizi ya mfululizo. Milipuko kadhaa pia imetokea katika eneo la Eastleigh linalokaliwa na Wasomali wengi. Taarifa hiyo imeongeza kuwa Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa na washirika wengine wanaotoa misaada kwa wakimbizi wanatakiwa kuacha kutoa huduma za moja kwa moja kwa raia wanaotafuta hifadhi na wakimbizi wanaoishi katika maeneo ya mijini na badala yake waelekeze misaada hiyo katika kambi za wakimbizi.
CHANZO: IRIB
0 comments:
Post a Comment