POLISI AJIUA KWA RISASI


Askari Polisi mwenye cheo cha Konstebo, Edward Chacha (25) amejiua kwa kujifyatulia risasi kidevuni baada ya kumpiga risasi za moto, Hadija Kiswaga (37), mkazi wa Mtaa wa Majengo mjini Mpanda wakigombea tanuru la matofali ya kuchoma, kila mmoja akidai tanuru hilo ni mali yake.




Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Joseph Myovela alisema kuwa mkasa huo ulitokea juzi saa tisa alasiri katika kitongoji cha Nsemulwa mjini Mpanda ambapo inadaiwa tanuru hilo waliuziwa kila mmoja wao kwa wakati wake bila wao wenyewe kufahamiana.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Kamanda Myovela alisema kuwa Konstebo Chacha mwenye nambari G 8627 aliyekuwa akifanya kazi katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Mpanda, siku ya tukio akiwa na askari wenzake walipangiwa lindo.

Alidai kuwa baada ya kupangiwa lindo, alichukua bunduki ya kivita na risasi zake akapanda pikipiki na kuondoka mwendo wa kasi huku akiwaacha wenzake kituoni hapo wakisubiri gari la Polisi ili liwasambaze kwenye malindo yao.

“Lakini dakika kumi baadaye nilipigiwa simu iliyonitaarifu kuwa kuna mlio wa risasi za moto katika kitongoji hicho cha Nsemulwa, lakini kabla sijafika kwenye tukio, nikapigiwa tena simu nyingine iliyonitaarifu kuwa askari huyo amejiua kwa kujipiga risasi baada ya kumpiga risasi mwanamke mmoja,” alisema.

Inadaiwa kuwa asubuhi hiyo ya tukio, Chacha alimkuta Hadija akisomba matofali yaliyochomwa kutoka katika tanuru lililokuwa katika kiwanja chake na kuhamishia kwenye kiwanja kingine.
Kwa mujibu wa madai hayo, Chacha alimumuru Hadija aache mara moja kuyasomba kwa kuwa yalikuwa mali yake na katika kiwanja chake lakini mwanamke huyo alikaidi na kuendelea kuyasomba akidai ni mali yake pia.

Kamanda Myovela alisema taarifa kutoka katika eneo la tukio zilieleza kuwa wote wawili kwa nyakati tofauti walikuwa wameuziwa tanuru hilo la matofali ya kuchoma bila ya wao wenyewe kufahamiana, na Polisi inamsaka mtu huyo ambaye hadi jana, jina lake lilikuwa halijafahamika.
“Baada ya Hadija kukaidi ndipo askari Chacha alifoka na kumweleza mwanamke huyo kuwa kama unajifanya mkaidi basi atamtambua yeye ni nani na kisha akapanda pikipiki na kwenda moja kwa moja Kituo Kikuu mjini hapa.

“Baada ya kukabidhiwa bunduki hiyo iliyokuwa tayari na risasi zake alirudi eneo la tuki na kumkuta Hadija akiendelea kusomba matofali, ndipo bila kusema lolote alimfyatulia risasi mfululizo hadi akaanguka chini huku akidhani kuwa ameua naye pia aliweka mtutu wa bunduki kidevuni na kujilipua na kufa papo hapo,” alidai Kamanda Myovela.

Kwa mujibu wa kamanda Myovela, risasi hizo za moto zilichana nyama ya matiti ya Hadija ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya mjini hapa kwa matibabu huku hali yake ikielezwa kuimarika.

Kamanda Myovela alisema pia mwili wa marehemu upo katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda, huku Polisi ikifanya maandalizi ya kumsafirisha kijijini kwao katika Wilaya ya Tarime mkoani Mara kwa maziko.

HABARILEO
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment