BOSI ANG'OKA BOHARI YA DAWA KWA DAWA BANDIA

SERIKALl inaonekana haitaki tena mchezo katika taasisi zake na hivyo imeamua kuchukua uamuzi mzito kwa kuendelea kusimamisha kazi wakuu wa taasisi hizo ili kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma mbalimbali. Hatua hizo zinalenga kuondoa malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na wananchi dhidi ya utendaji mbovu wa baadhi ya viongozi hao, lakini pia ikitafuta kujiridhisha kwa kuthibitisha tuhuma hizo kwa ushahidi usio na shaka. Lengo pia ni kuhakikisha kila mtu anatendewa haki na hakuna anayeonewa na hatimaye utendaji kazi serikalini na katika taasisi zake unakuwa wa kuridhisha. Wimbi la viongozi hao kusimamishwa liliendelea jana, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Joseph Mgaya alisimamishwa kazi kwa tuhuma za ununuzi wa dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV). Mbali na Mgaya, wengine aliosimamishwa pamoja naye ni Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora, Sadiki Materu na Ofisa Udhibiti wa Ubora, David Masero. Mgaya anakuwa kiongozi wa sita wa taasisi nyeti nchini kusimamishwa kazi kwa tuhuma hizo kwa mwaka huu. Serikali pia kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), imesitisha uzalishaji wa dawa zote katika kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI) hadi uchunguzi unaofanywa kupitia vyombo vya usalama kuhusu uzalishaji wa dawa bandia utakapokamilika kwa hatua zaidi za kisheria. Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi alisema tuhuma za MSD kununua dawa bandia kutoka TPI ziligundulika baada ya matokeo ya ukaguzi, ufuatiliaji na uchunguzi wa kimaabara. Alisema mwanzoni mwa Agosti, Wizara kupitia TFDA kwa kuzingatia Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ilibaini kuwapo ARVs bandia aina ya TT-VR 30 toleo namba OC.01.85 katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara. Baada ya kubainika kwa tatizo hilo, Dk Mwinyi alisema Wizara kupitia TFDA ilifanya ukaguzi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Mara na baadaye ukaguzi wa kina katika mikoa mingine nchi nzima kwa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama. "Ukaguzi huu ulifanyika kati ya Agosti 6-31 mwaka huu na ulihusisha MSD makao makuu na kanda pamoja na kiwanda cha TPI ambacho ndicho kilitengeneza dawa hiyo. Pia sampuli za dawa husika zilichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara," alisema. Alisema baada ya kubaini tatizo hilo, waliwataarifu waganga wakuu wa mikoa yote nchini na kuwaelekeza wasimamishe matumizi ya ARVs toleo namba OC.01.85 katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya katika mikoa yao. Mbali na kusitisha matumizi, waganga hao walielekezwa kuiondoa dawa hiyo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kuirudisha kwa msambazaji ambaye ni MSD na Wizara kupitia TFDA ilifanya uchunguzi wa kimaabara ili kuainisha viambata vya dawa hiyo. Dk Mwinyi alisema katika ukaguzi na ufuatiliaji huo pamoja na uchunguzi wa kimaabara, walibaini kwamba dawa yenye jina la biashara TT-VIR 30 toleo namba OC.01.85 ni bandia kwa mujibu wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi .
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment