Waziri Mkuu Mpya wa Ethiopia Hailemariam Desalegn ameapishwa kushika wadhifa huo, siku chache baada ya mazishi ya Waziri Mkuu wa zamani, Meles Zenawi yaliyofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Addis Ababa.
“Meles [waziri mkuu wa zamani] alikuwa akijihesabu kuwa mwana wa watu...Ninaahidi kuendeleza historia ya Meles bila kubadilisha chochote...Tutaimarisha demokrasia na haki za binaadamu nchini. Iwapo yatatokea matatizo tutayatatua...Tutafanya kazi pamoja na mashirika ya haki za binaadamu, tume ya uchaguzi na baadhi ya vyama vya upinzani," aliongeza.
Wiki iliyopita, wabunge walimteua mhandisi huyo wa maji mwenye umri wa miaka 47 kuwa mwenyekiti wa muungano wa chama cha Ethiopian Peoples' Revolutionary Democratic Front (EPRDF) na waziri mkuu wa nchi hiyo.Mapema mwezi Agosti, Meles Zenawi [waziri mkuu wa zamani] alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 57 katika hospitali moja nchini Ubelgiji na mwili wake kuzikwa katika makaburi ya Holy Trinity Cathedral katika mji mkuu wa nchi hiyo.
Wakati huohuo, ripoti zinasema kuwa sababu za kifo cha Zenawi bado hazijajulikana.
Zenawi, ambaye alikuwa madarakani tangu mwaka 1991, alisifika kwa ukuaji wa uchumi wa Ethiopia.

0 comments:
Post a Comment