Ndege ya Marekani isiyokuwa na rubani (drone) |
Kufuatia hali ya sintofahamu iliyoukumba uhusiano wa
Washington na Islamabad, Pakistan imeviamuru vikosi vyake vya anga kuzitungua
ndege zozote zisizokuwa na rubani (drones) zitakazoingia katika anga ya nchi
hiyo, zikiwemo zile za jeshi la Marekani ambazo zinasadikiwa kuhusika na idadi
kubwa ya vifo vya raia katika taifa hilo la Asia.
“Hatutoruhusu yeyote kukiuka sheria za anga yetu. Nimetoa
amri kwa PAF (jeshi la anga la Pakistan) kuzitungua droni, zikiwemo zile za
Marekani, kama zitaingia anga yetu, na kwenda kinyume na uhuru wa nchi yetu na
mshikamano wa eneo letu,” Mkuu wa kikosi cha anga cha nchi hiyo, Sohail Aman amesema
katika taarifa yake mjini Islamabad, kama ilivyoripotiwa na mtandao wa Times of
India.
Amri hiyo ni tofauti na sera ya mwanzo ya jeshi la anga
la nchi hiyo, ambapo lilikuwa likilalamikia mashambulizi ya droni za Marekani
kwenye ardhi yake, lakini halikuwahi kutoa kitisho cha kuzitungua.
Tangazo hilo linakuja wiki mbili baada ya droni moja ya
Marekani kushambulia eneo linaloshukiwa kuwa kambi ya wanamgambo katika mpaka
wa nchi hiyo na Afghanistan na kuua watu wasiopungua watatu.
Marekani imekuwa ikitumia ndege zisizokuwa na rubani
kufanya upelelezi na mashambulizi nchini Pakistan tangu Washington na washirika
wake walipoivamia Afghanistan mwaka 2001.
Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Habari za Kiuchunguzi,
mamia ya raia, wakiwemo wanawake na watoto, wameuawa katika mashambulizi ya
droni za Marekani yanayolenga kile kinachoelezwa kuwa ni maeneo ya wanamgambo
nchini Pakistan na Afghanistan tangu mwaka 2004.
Islamabad imekuwa ikilaani mashambulizi ya droni za
Marekani kwenye ardhi yake, ikiielezea kuwa ni kukiuka uhuru wa Pakistan.
Operesheni ya droni za Washington imekuwa ikipingwa
vikali na wananchi wa Pakistan ambao wamefanya maandamano kadhaa kwa miaka
kadhaa kupinga vifo vilivyosababishwa na mashambulizi hayo.
Waandamanaji wa Kipakistan wakichoma moto bendera ya Marekani wakati wa maandamano ya kulaani shambulizi la droni ya Kimarekani mnamo Mei 27, 2016 mjini Peshawar. |
Kamanda Aman alikumbushia pia tukio la kuvunja uaminifu
kuhusu ndege aina ya F-16 zilizotengenezwa na Marekani ambazo Pakistan ilizilipia,
lakini hazikutolewa.
Kamanda huyo wa jeshi la anga la Pakistan alisifu uwezo
wa kikosi chake akisema kuwa wanajeshi wake wako tayari kulinda uhuru wa nchi hiyo.
Amri hiyo mpya kabisa imekuja kufuatia sintofahamu
iliyojitokeza kwenye uhusiano wa washirika hao wawili kufuatia shutuma za Rais
wa Marekani Donald Trump dhidi ya Islamabad akiituhumu kuunga mkono makundi ya
wanamgambo.
Maafisi mjini Islamabad wamekanusha vikali tuhuma hizo. Wanasema
kuwa Pakistan imefanya kazi kubwa kupambana na ugaidi.
Mwezi Agosti Trump aliikosoa vikali Pakistan wakati
akitangaza mkakati mpya wa utawala wake nchini Afghanistan. Kauli za rais huyo
ziliibua hasira miongoni mwa maafisa na wananchi wa Pakistan.
Aidha, amri hiyo imekuja wiki moja baada ya ziara
iliyofanywa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Jim Mattis nchini humo ambapo
aliwataka kuongeza mara dufu juhudi zao za kupambana na wanamgambo ambao
wanashukiwa kuitumia nchi hiyo kama ngome yao na kufanya mashambulizi katika
nchi jirani ya Afghanistan.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani James Mattis (kushoto) akiwasili mjini Islamabad, Pakistan, Desemba 4, 2017. |
Mattis pia alikutana na maafisa wa ngazi za juu wa jeshi
la Pakistan, akiwemo mkuu wa jeshi Jenerali Qamar Javed Bajwa na Luteni
Jenerali Naveed Mukhtar, ambaye ni mkuu wa shirika mama la ujasusi ambaye
serikali ya Marekani inasema kuwa ana uhusiano na wanamgambo wa Haqqani na
Taliban.
Afisa mmoja kutoka wizara ya ulinzi ya Marekani,
akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alinukuliwa na taarifa za vyombo vya
habari akisema kuwa mazungumzo ya Mattis alikuwa ya moja kwa moja na ya wazi.
Aliongeza kuwa miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni
kuifanya Pakistan isaidie kuwaleta wanamgambo wa Taliban kwenye meza ya
mazungumzo.
0 comments:
Post a Comment