Rais wa Marekani, Donald Trump |
Baada ya kusita kwa muda, hatimaye Rais wa Marekani,
Donald Trump ametia saini sheria inayoziwekea vikwazo nchi za Urusui, Iran na
Korea ya Kaskazini hali inayoashiria kuwa amesalimu amri mbele ya mbinyo wa
ndani, jambo linalotazamiwa kuzorotesha juhudi za kuboresha uhusiano na Urusi.
Trump amesaini sheria hiyo akiwa amejifungia ndani na
pasipo kamera za wanahabari baada ya kushindwa katika juhudi zake za kuzuia
upitishwaji au upunguzaji wa sheria hiyo.
Hali ya kusita kusaini sheria hiyo ilionekana wazi
katika matamshi yake makali ambapo alisema kuwa sheria hiyo ina upungufu na
“kasoro nyingi”.
SHERIA
INAMZUIA RAIS KUONDOSHA VIKWAZO
Trump alisema kuwa bunge la Congress lilifanya haraka
katika hatua yake ya kupitisha vikwazo hivyo ambapo alidai kuwa kuna baadhi ya
mambo ambayo yanakiuka katiba, ikiwa ni pamoja kuufunga uwezo wa rais
kutekeleza sera zake za mambo ya nje.
Sheria hiyo, ambayo inazigusa pia Korea ya Kaskazini na
Iran, inalenga sekta ya nishati ya Urusi na inaipa Washington uwezo wa
kuyaadhibu makampuni yatakayoshiriki katika ujenzi wa mabomba ya mafuta ya
Urusi, na inaweka vikwazo dhidi ya wanunuzi wa silaha za Urusi.
Aidha, sheria hiyo inaufunga uwezo wa rais wa kuondosha
vikwazo, katika hatua inayoonesha kuwa wabunge wa Republican ambao
wanalidhibiti bunge la Congress hawana imani na Trump na wanatiwa wasiwasi na
matamshi ya rais wao kuhusu Rais wa Urusi, Vladmir Putin.
Vikwazo hivyo vinalenga kuiadhibu Urusi kwa madai kwamba
iliingilia mchakato wa uchaguzi wa Urais wa Marekani wa mwaka 2016 ambapo bwana
Trump aliibuka mshindi, na pia hatua yake ya kuimega peninsula ya Crimea.
Trump amesema kuwa “atatekeleza” baadhi ya mambo katika sheria
hiyo, lakini akajizuia kusisitiza iwapo atayatekeleza yote, huku Ikulu ya nchi
hiyo ikiishia kusema kuwa Trump “atazingatia kwa umakini na kwa heshima
maazimio ya Congress”.
Trump alipokea muswada huo jioni ya Ijumaa lakini akawa
hajaisaini mpaka Jumatano.
Hatua hiyo ya kuchelewa kusaini iliibua minong’ono kuwa
Trump anaipinga sheria hiyo au anajaribu kuichelewa kwa njia moja au nyingine
baada ya wajumbe wa bunge la seneti kuikubali kwa kura 98 dhidi ya kura mbili.
Kwa kusaini sheria hiyo, Trump aliepuka hatua ambayo ingechukuliwa
na Congress ikiwa ni pamoja na kuipitisha kwa hali yoyote, jambo ambalo lingekuwa
ni sawa na kumdunisha.
TILLERSON:
UPITISHWAJI WA SHERIA HIYO KUNAWEKA MAZINGIRA MAGUMU YA KUBORESHA UHUSIANO NA
MOSCOW
Mapema siku ya Jumanne, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa
Marekani, Rex Tillerson alisema kuwa atakutana na mwenzake wa Urusi Sergey
Lavrov mwishoni mwa juma, lakini akatahadharisha kuwa uhusiano wa Urusi na
Marekani unaweza kuzorota. Alisema kuwa hatua ya Congress kupitisha sheria ya
vikwazo imefanya juhudi za kuboresha uhusiano na Moscow kuwa “ngumu zaidi”.
Moscow ambayo ilitarajia kupitishwa kwa sheria hiyo,
iliiamuru Washington kupunguza wanadiplomasia wake walioko Urusi mpaka kufikia watu
455 kabla ya Septemba mosi ili iendane na ukubwa wa wanadiplomasia wa Urusi
waliopo nchini Marekani.
MOSCOW
YALAANI SERA “HATARI NA ZA MTAZAMO MFUPI”
Katika jibu la kwanza baada ya Trump kusaini sheria
hiyo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Urusi ilikosoa vikali kile ilichokieleza
kuwa ni siasa “hatari” na “za mtazamo mfupi” za Washington.
Katika taarifa yake, wizara hiyo ilisema kuwa “ni
mwenendo wa siasa zisizotazam mbali na za hatari ambazo zinatishia usalama wa
dunia ambao Moscow na Washington zinahusika nao kwa namna maalumu”.
Ikiongeza kuwa: “Tumekwishatangaza
kwamba hatutaacha vitendo vya kiuadui vipite bila jibu… tunasubiri kuchukua
hatua nyingine kali”.
Aidha, Moscow iliitolea wito Marekani “kuachana na mambo
ya kufikirika na kutambua kuwa kitisho chochote au jaribio lolote la shinikizo
halitailazimisha Urusi kubadilisha sera zake au kuyatoa mhanga maslahi yake ya
kitaifa”.
Pia wizara hiyo ilieleza kuwa Moscow itaendelea kufungua
mikono ya ushirikiano na Marekani katika maeneo ambayo inayachukuliwa kuwa yana
faida kwake na kwa usalama wa dunia, hususan katika utatuzi wa migogoro ya
kieneo na kikanda.
Lakini ikasema kuwa ushirikiano hautakuwa na matunda
isipokuwa pale ambapo watunga sera mjini Washington watakapoacha kuutazama
ulimwengu kupitia jicho la Marekani pekee.
#Mzizima 24/ Mashirika ya habari
0 comments:
Post a Comment