Arsene Wenger ametupilia mbali ripoti kuwa Alexis
Sanchez ameiambia Arsenal kuwa anataka kuondoka katika msimu huu wa majira ya
joto.
Wenger alitoa kanusho la mkato na la moja kwa moja
alipoulizwa kuhusu tetesi kuwa mchezaji huyo alimtaarifu azma yake ya kutaka
kuondoka kwenye klabu hiyo yenye makao yake kaskazini mwa jiji la London katika
juhudi zake za kutaka kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa katika klabu ya Manchester
City.
Meneja huyo wa muda mrefu aliendelea kutokuwa wazi
kuhusu mustakbali wa Sanchez licha ya tetesi zilizozagaa zikimhusisha nyota
huyo mwenye umri wa miaka 28 kwamba anataka kuungana na kocha wa zamani wa
Barcelona Pep Guardiola katika dimba la Etihad.
Hilo limewapelekea watu wengi kuamini anaweza kuendelea
kubaki Arsenal mpaka mwishoni mwa mkataba wake licha ya kwamba amekataa kusaini
mkataba mpya na klabu hiyo ya dimba Emirates.
Wenger ambaye yuko mjini Sydney kwa ajili ya michezo
miwili ya kirafiki na kilabu za ligi kuu ya nchi hiyo, A-League, za Sydney FC na
Western Sydney, amesisitiza azma yake ya kutomuuza Sanchez kwa mahasimu wao wa
Ligi Kuu ya Uingereza.
"Hakuna ajuaye leo kama Sanchez atakuwa katika
mwaka wa mwisho wa mkataba wake, kwa sababu anaweza kuongeza mkataba wake na
sisi mwanzoni mwa msimu au katikati ya msimu," Wenger alisema.
"Hivyo, sio lazima huu uwe mwaka wa mwisho wa
mkataba wake kwenye klabu ya Arsenal."
Sanchez ameachwa katika safari hiyo ya Australia
baada ya kuichezea timu yake ya taifa la Chile kwenye michuano ya Kombe la
Mabara iliyomalizika hivi karibuni nchini Urusi.
Mchezaji mwingine aliyezungumzwa sana, Olivier Giroud, ameungana
na kikosi hicho katika safari yake ya Sydney.
Straika huyo raia wa Ufaransa anaelezwa kuwa anawindwa
na vilabu vya Everton, Marseille na West Ham.
Giroud alipoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza
kwa sehemu kubwa ya msimu uliopita ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Sanchez na
wakati mwingine Danny Welbeck, jambo lililomfanya kueleza kuwa anataka
kuchezezwa mara kwa mara.
Kuwasilia kwa Alexandre Lacazette kunaweza kupunguza
zaidi ushiriki wake dimbani, lakini Wenger amesisitiza kuwa Giroud, ambaye
aliongeza mkataba wake mwezi Januari, ni mchezaji muhimu kwa kikosi chake.
Bosi huyo wa Arsenal alithibitisha kuwa Lacazette atashiriki
katika mchezo wa Alhamisi dhidi ya Sydney FC kabla ya kipute cha Jumamosi dhidi
ya Western Sydney.
"Ndiyo, Lacazette ataanza kucheza hapa" alisema
Wenger.
"Bila shaka Alhamisi usiku atashiriki mchezoni. Atacheza
mechi zote mbili."
Usajili wa mchezo huyo mwenye umri wa miaka 26, ambaye
alifunga magoli 100 kwenye michezo 203 aliyocheza na klabu ya Lyon katika ligi
kuu ya Ufaransa, Ligue 1, ni mapinduzi kwa Wenger ambaye klabu yake imeshindwa
kuingia katika nafasi nne za juu na kushindwa kufuzu kwa michuano ya Klabu
Bingwa katika hatua ambayo inaonekana kuwa ni zama mbaya kabisa katika kipindi
chote cha kazi ya ukocha kwa miaka 21.
Mchezaji mwingine aliyesajiliwa hivi karibuni, raia wa Bosnia-Herzegovina,
Sead Kolasinac, naye amesafiri na klabu na anaweza kucheza katika ziara hiyo ya
kwanza nchini humo kwa kipindi cha miaka 40, kabla ya kuendelea na ziara ya
kujiandaa na msimu mpya watakayoifanya nchini China.
0 comments:
Post a Comment