Muandamanaji akikabiliana na askari wa kutuliza ghasia wakati wa maandamano dhidi ya serikali ya Rais wa Venezuela Nicolas Maduro mjini Caracas, Venezuela, Julai 22, 2017. |
Upinzani nchini Venezuela umetangaza siku mbili za mgomo wa
kitaifa dhidi ya Rais wa nchi hiyo Nicolas Maduro baada ya siku iliyoshuhudia
ghasia na makabiliano mjini Caracas siku ya Jumamosi ambapo waandamanaji kadhaa
walijeruhiwa.
Muungano wa Kidemokrasia wa vyama vya upinzani – ambao uliratibu mgomo
wa saa 24 wiki hii ambao uliitikiwa na mamilioni ya watu na kulemeza sehemu
kubwa ya shughuli katika taifa hilo la Amerika ya Kusini – umesema kuwa mgomo ujao
utafanyika siku za Jumatano na Alhamisi.
Maandamano makubwa pia yameandaliwa kwa siku za Jumatatu na Ijumaa
katika juhudi za kumlazimisha Rais Nicolas Maduro afute uchaguzi wenye utata wa
bunge jipya uliopangwa kufanywa Julai 30.
Mzozo huo wa kisiasa unaokua kwa kasi katika taifa hilo unakuja
baada ya zaidi ya watu 100 kupoteza maisha na maelfu wengine kujeruhiwa katika
maandamano ya kuipinga serikali tangu ghasia zilipoanza mwezi Aprili.
"Wananchi wa Venezuela hawatokata tamaa, wana ujasiri,
watajitokeza kuitetea demokrasia na katiba," alisema mbunge wa upinzani Simon
Calzadilla kwenye mkutano na wanahabari huku akiwa amezungukwa na maafisa wengine
wa muungano wa upinzani.
Wapinzani wanamtuhumu Maduro kuipeleka Venezuela kwenye udikteta
na kuua uchumi. Wanataka uchaguzi huru na kuhitimishwa kwa utawala wa miongo miwili
wa siasa za kisoshalisti.
Maduro mwenye umri wa miaka 54, anajitambulisha kama mbeba bendera
ya siasa mrengo wa kushoto duniani dhidi ya anaowaita kuwa ni “magaidi” wa
mrengo wa kulia wanaotaka kufanya mapinduzi kwa kuchochewa na Marekani na
vyombo vya habari vya kimataifa.
Upinzani unatumia mbinu ya kuingia mitaani ijulikanayo kama “saa
sifuri” kwa Venezuela ili kujaribu kuzuia Bunge jipya la Katiba ambalo Maduro
anataka kuliweka kwa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa juma lijalo.
Wapinzani hao wamegomea uchaguzi huo wakiuita kuwa ni fedheha na badala
yake wanataka kufanyike uchaguzi wa kawaida.
Bunge hilo ambalo kanuni zake zinaonekana kuipa serikali kura nyingi,
ingawa ina uungaji mkono mdogo, linaweza kuandika upya katiba na kulivunja
bunge la sasa linaloongozwa na upinzani.
“TUMECHOSHWA NA UGAIDI”
Kwenye maandamano kinzani ya wale wanaoiunga mkono serikali yaliyofanyika
siku ya Jumamosi, wagombea wa Bunge la Katiba walisema kuwa hiyo ndio njia
pekee ya kurejesha amani nchini Venezuela. "”Hatutowaruhusu waiharibu nchi
yetu tunayoipenda," alisema Delcy Rodriguez, ambaye aliachia nafasi yake
ya uwaziri wa mambo ya nje ili aweze kugombea kwenye bunge jipya.
"Sote tulioungana tunaenda kuwaambia wale wa mrengo wa kulia ‘Tumechoshwa
na ugaidi’," mke wa Maduro Cilia Flores, ambaye pia anagombea nafasi kwenye
bunge hilo aliuambia umati uliokusanyika kwenye maandamano hayo mjini Caracas.
Aidha, siku hiyo ya Jumamosi, idara ya upelelezi ya serikali
ilimkamata Angel Zerpa, ambaye ni miongoni mwa mahakimu 13 walioapishwa na
upinzani kuwa mahakimu wa mahakama kuu katika hatua ya wapinzani hao kuipinga
serikali iliyopo madarakani.
Serikali imetishia kuwakamata majaji wote walioteuliwa na
wapinzani na kuwafikisha kwenye mahakama za kijeshi.
Shinikizo la kimataifa limeongezeka dhidi ya Maduro akitakiwa
kufuta kura hiyo inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa juma lijalo, ikiwa ni
pamoja na kitisho kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump aliyetishia
kumuwekea vikwazo vya kiuchumi.
Lakini serikali haioneshi kuachana na wazo hilo, huku ikitangaza
kuwa itawaweka barabarani askari wapatao 232,000 kuhakikisha kuwa Bunge la
Katiba linaendelea.
Siku ya Jumamosi, vikosi vya Walizi wa Jamhuri, vilionekana
kuwarushia waandamanaji mabomu ya kutoa machozi, hatua inayochukuliwa kuwa ni
ukiukaji wa kanuni za kimataifa.
"Kumekuwepo na ukandamizaji mkubwa na dunia inapaswa kujua
hali inayotukabili katika mitaa ya Venezuela," alisema kiongozi wa upinzani
Maria Corina Machado.
0 comments:
Post a Comment