Waziri wa mambo ya nje wa Misri
Sameh Shoukry (kulia) akisalimiana na mwenzake wa Saudi Arabia Adel al-Jubeir (kushoto). Wakati
wa mkutano wa pamoja kwa vyombo vya habari baada ya kikao chao kilichofanyika
mjini Cairo nchini Misri Julai 5, 2017. Pembeni ni Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu Abdullah bin Zayed Al
Nahyan.
|
Nchi za Saudi Arabia, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu
na Bahrain zimesema kuwa ziko tayari kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya Qatar
kufuatia hatua ya Doha kuyakataa masharti yao ya kukomesha mzozo wa
kidiplomasia unaoendelea kati ya Qatar na mataifa hayo.
Katika taarifa yao iliyotolewa mapema leo, mataifa hayo
manne yanasema kuwa kitendo cha Qatar kukataa mapendekezo yao kinaonesha namna
nchi hiyo inavyounga mkono ugaidi na kuendeleza juhudi za kuvuruga usalama na
amani katika eneo hilo.
Mataifa hayo unaituhumu Qatar kuwa haijali usalama na
inaenda kinyume na maslahi ya wananchi wa ukanda huo.
Aidha, walimshukuru Amiri wa Kuwaiti Sheikh Sabah
al-Ahmad al-Jaber al-Sabah kwa juhudi zake za usuluhishi na kuikosoa vikali
Qatar kwamba inamuangusha kwa kutaka kuurejesha mzozo huo katika hatua ya
mwanzo kabisa.
Mnamo Juni 5, mataifa hayo yalikata rasmi uhusiano wake
na Qatar baada ya kuituhumu kuwa inaunga mkono “ugaidi” na kuvuruga amani ya
Mashariki ya Kati, tuhuma ambazo Qatar inasema hazina uhalali wowote na kwamba
zinatokana na madai ya urongo.
Katika hatua ya wazi ya kutaka uungaji mkono Kutoka
Marekani na Israel, mataifa hayo yamesitisha safari zote za ardhini, angani na
baharini kwenda na kutoka Qatar, kuwafukuza wanadiplomasia wake na kuwaamuru
raia wa Qatar kuondoka katika nchi hizo.
Saudi Arabia ilifunga moja kwa moja mpaka wake wa
ardhini na Qatar ili kusitisha usafirishaji wa chakula nchini humo. Hatua hiyo
iliwafanya viongozi wa Qatar kuzigeukia
nchi za Iran na Uturuki kuziba ombwe hilo.
Kukifunga kituo cha utangazaji cha Al Jazeera kilichopo
mjini Doha, kukata uhusiano wa kidiplomasia na Iran, kufunga kambi ya kijeshi
ya Uturuki nchini Qatar na kulipa kiwango fulani pesa kama fidia ni miongoni
mwa masharti ambayo mataifa hayo yaliipatia Qatar ili kumaliza mgogoro huo.
Doha inasema kuwa vikwazo ilivyowekewa ni “hujuma ya
wazi” na masharti yaliyotolewa ili kuviondosha hayana “uhalisia”.
Mnamo siku ya Jumatano, waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar,
Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, alisema kuwa masharti ya mataifa hayo
yanamaanisha Qatar kusalimisha mamlaka na uhuru wake.
Pia aliondoa uwezekano wa maridhiano ya haraka na kusema
kuwa nchi yake iko tayari na imejiandaa kikamilifu iwapo mzozo huo utaendelea
zaidi.
0 comments:
Post a Comment