Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akitoa
hotuba wakati wa mkutano maalum ulioyakutanisha mabunge mawili ya nchi hiyo
kwenye Kasri la Versailles, jirani na Paris, Ufaransa, Julai 3, 2017.
|
Bunge la Ufaransa limepiga kura kuongeza muda wa hali ya
hatari nchini humo kwa kipindi cha miezi sita zaidi, huku serikali ikitangaza
kuwa itafunga misikiti mitatu zaidi kama sehemu ya hatua hiyo.
Mapema Alhamisi, wabunge nchini humo walipitisha azimio hilo
kwa kura 137 dhidi ya 13. Hali hiyo itaendelea mpaka mwezi Novemba. Hii ni mara
ya sita kuongozwa kwa muda wa hali ya dharura.
Hali ya dharura huvipa vikosi vya usalama uhuru zaidi wa
kufanya uvamizi na upelelezi. Pia huzipa mamlaka uwezo wa kuzuia safari za watu
na magari katika nyakati na maeneo maalum.
Misikiti itakayoonekana kufumbia macho ugaidi itafungwa
chini ya hali hiyo ya hatari.
“Leo kuna misikiti mitatu tunayotaka kuifunga,” Waziri
wa Mambo ya Ndani Gerard Collomb alisema na kuongeza: “Tangu kuanza kwa hali ya
hatari tumeifunga misikiti 16.”
Ni mara ya kwanza hali ya hatari kuongezewa muda chini
ya utawala wa Rais Emmanuel Macron, ambaye hapo mwanzo alikuwa ameahidi
kuiondosha lakini pia chini ya muswada mpya baadhi ya hatua zimegeuzwa kuwa sheria
za kudumu.
Aidha, Collomb alieleza kuwa kuna sababu njema ya
kuongeza muda wa hali ya hatari.
“Ni hakika kwamba tunahitaji kuongeza muda wa hali ya
hatari. Kwa nini? Kwa sababu tangu kuanza kwa mwaka huu, tumefanikiwa kuzuia
mashambulizi saba ambayo yangewaathiri watu wengi,” alisema Collomb.
Miaka kadhaa nyuma Ufaransa iliwahi kukumbwa na mashambulizi
ya kigaidi ya mara kwa mara ambayo yaliwaua watu wengi kuliko nchi nyingine
yoyote ya Ulaya. Mfululizo wa mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea Novemba mwaka
2015 yaliua watu 130 na kuifanya serikali ya Rais wa wakati huo Francois
Hollande kutangaza hali ya hatari kwa mara ya kwanza.
Hali ya hatari na muswada huo wa sheria uliowasilishwa
na serikali ya Rais Macron vimekoselewa na mashirika ya haki za binadamu ambayo
yanasema kuwa zinaminya uhuru wa kiraia.
0 comments:
Post a Comment