Saed Kubenea, Makamu Mwenyekiti Kanda ya Pwani (Chadema) akizungumza na Waandishi wa habari |
CHADEMA wameanzisha operesheni maalum ya kumwondoa
Profesa Ibrahimu Lipumba, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF)
katika chama hicho imezinduliwa leo, anaandika Irene David.
Oparesheni hiyo iliyopewa jina la “Operasheni Ondoa
Msaliti CUF (OBM) imezinduliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kwa kushirikiana na viongozi wa CUF wanaomuunga mkono Maalim Seif Sharif Hamad,
Katibu mkuu wa CUF.
Maamuzi hayo yalifikiwa jana baada ya kikao cha pamoja
kilichofanywa na viongozi wa Chadema Kanda ya Pwani na viongozi wa CUF kujadili
mgogoro ndani ya CUF na mstakakbali wa chama hicho na vyama vinavyounda Umoja
wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Saed Kubenea, Makamu Mwenyekiti Kanda ya Pwani ambaye
pia ni Mbunge wa Ubungo (Chadema) amesema: “Sisi kama Chadema kwa umakini
kabisa tutawasaidia viongozi wa CUF na wanachama wao kumwondoa msaliti Prof.
Lipumba Buguruni.”
“Katika hili pia tumeamua kila siku ambayo kesi ya CUF
inaendeshwa mahakamani wanachadema tutajitokeza kuisindikiza CUF tunayoitambua;
tumekubaliana Mameya wetu wote wa jiji la Dar es Salaam wasitoe ushirikiano kwa
mtu yeyote wa vimelea vya Lipumba.”
Kwa upande wake Dkt. Makongoro Mahanga, Mwenyekiti wa
Chadema mkoa wa Dar es Salaam amesema: “Chadema ni washirika wa CUF katika
Ukawa. Hivyo tunaamini wanavyoyumbishwa CUF hata sisi hatuwezi kubaki sarama.”
“Tumeona tunaathirika. Makao makuu ya Chadema na CUF
yapo katika kanda yetu. Tumejiridhisha kwamba mgogoro si kati ya Lipumba na
Seif, ni kati ya dola. Tumeamua kupambana na dola kwa kuanza na hawa wasaliti
wakiongozwa na Lipumba.”
Aidha, Riziki Ngwali, Mbunge wa Viti Maalum na Kiongozi
wa Wabunge wa CUF bungeni, amesema “Tunataka pia Watanzania watambue kuwa
mgogoro wa dola dhidi ya CUF ni wa kupandikizwa. Kwa sababu vyombo vyake
vinatumika.”
CHANZO: Mwanahalisi Online
0 comments:
Post a Comment