MAELEZO YA MAALIM SEIF ALIPOKUTANA NA WANAHABARI NCHINI



THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF –Chama Cha Wananchi)

Office of the Secretary General
P.O.BOX 3637, Zanzibar, Tanzania

MAELEZO YA KATIBU MKUU WA CUF, MAALIM SEIF SHARIF HAMAD, KWENYE MKUTANO NA WAHARIRI WA VYOMBO VYA HABARI NCHINI

Ndugu zangu wahariri na waandishi wa Habari,

Assalam alaykum.

Awali ya yote sina budi kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uhai na uzima wa afya na tukaweza kukutana wakati huu katika eneo hili kwa ajili ya mkutano huu maalum na waandishi wa vyombo mbali mbali vya habari vya ndani na nje ya nchi.

Pili, nitumie fursa hii kukushukuruni nyinyi wahariri na waandishi wa habari kwa kuitikia wito wetu na kuja kutusikiliza. Naamini mtatusikiliza kwa makini, na kisha mtawafikishia watanzania yale ambayo tutawaeleza.

Ndugu Wahariri na Waandishi wa Habari,

Kama mnavyofahamukuwa CUF-Chama Cha Wananchi kinapitia katika wakati mgumu na changamoto nyingi katika kutekeleza majukumu yake ya Kikatiba,
Kisheria na Kidemokrasia kutokana na vitendo vya hujuma dhidi yake vinavyofanywa kwa mashirikiano makubwa baina ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi na Profesa Ibrahim Lipumba ambaye amekuwa akipatiwa msaada wa kila hali na Jeshi la Polisi Tanzania. Kwa sababu hiyo, tumewaita leo hii kukuelezeni kwa kina juhudi tulizozichukuwa katika kukabiliana na hujuma zinazofanywa dhidi ya taasisi yetu na watendaji wake, na hatua zetu za kuendelea kutimiza wajibu wetu kama taasisi inayowajibika kwa mujibu wa sheria za nchi kwa lengo la kukabiliana na uhuni unaofanywa dhidi ya Haki na Demokrasia.

Ndugu wahariri na waandishi wa Habari,

Sehemu kubwa ya vitendo vinavyofanywa na Jaji Francis Mutungi dhidi ya CUF kama taasisi ndio msingi wa shauri nambari 23/2016 (Miscellaneous case namba 23/2016) lililofunguliwa na wadhamini wa Chama cha CUF dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (kwa niaba ya Serikali yote), Profesa Ibrahim Haruna Lipumba na wenzake 9.

Hata hivyo, wakati shauri nambari 23/2016 linaendelea katika Mahkama Kuu ya Tanzania, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba na wafuasi wake wakiungwa mkono kwa nguvu kubwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, kama ilivyobainika katika matukio kadhaa, wamekuwa wakifanya na kutekeleza vitendo vinavyohujumu Chama cha Wananchi (CUF), visivyohusiana kabisa na siasa, demokrasia, wala majukumu ya CUF kama taasisi, huku jeshi la polisi na watendaji wake likiwawekea ulinzi wahalifu hao na kuhakikisha kuwa vitendo hivyo na vyengine vya kijinai vinafanikiwa.

Jeshi la polisi limekuwa likimlinda na kumkingia kifua Profesa Ibrahim Haruna Lipumba na wafuasi wake katika vitendo vyao dhidi ya Taasisi ya CUF. Polisi wameambatana nae kila alipokwenda kufanya hujuma dhidi ya CUF tofauti kabisa na ilivyotegemewa kuwa ulinzi ingewekewa CUF kwa kuwa ni taasisi halali iliyosajiliwa kisheria hivyo kustahiki haki ya ulinzi na msaada kutoka Jeshi la Polisi kwa mujibu wa kifungu cha 11(1) (b) cha sheria ya Vyama vya Siasa nchini sura ya 258 ya Sheria za Tanzania.

Ndugu wahariri na waandishi wa Habari,

Msingi wa maelezo haya kwenu ni kuwajuilisha namna ya jeshi la Polisi linavyoshiriki katika kuhakikisha kuwa hujuma zinazofanywa dhidi ya Chama cha Wananchi (CUF) zinafanikiwa.  Mtiririko wa matukio yafuatayo unaonesha wazi kuwa ushiriki wa Jeshi la Polisi katika hujuma hizi si jambo la sadfa bali ni jambo linaloratibiwa kwa makusudi kwa ushirikiano kati ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jeshi la Polisi na Profesa Ibrahim Haruna Lipumba.  Mtiririko wa matokeo hayo ni kama ifuatavyo:

1. KUVAMIA NA KUSABABISHA VURUGU ZISIZO ZA LAZIMA KATIKA MKUTANO MKUU MAALUMU WA TAIFA WA CUF, ULIOFANYIKA BLUE PEARL HOTEL, UBUNGO PLAZA, TAREHE 21 AGOSTI 2016

Itakumbukwa kuwa tarehe 21 Agosti 2016 CUF Chama Chetu cha CUF kiliitisha Mkutano Mkuu Maalumu wa Taifa ukiwa na agenda mbili; nazo ni Kupokea taarifa ya kujiuzulu kwa aliekuwa Mwenyekiti wetu, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, na kufanya uchaguzi kujaza nafasi zilizowazi ikiwemo nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa. Mkutano huo ulipokea na kukubali kujiuzulu kwa Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kwa kura 476 ambayo ni sawa na asilimia 70 dhidi ya kura 14 zilizotaka Profesa Lipumba aendelee kuwa Mwenyekiti. Na baadhi ya wajumbe hawakupiga kura. Mkutano ulikuwa na wajumbe 687  Profesa Ibrahim Haruna Lipumba akiwa na kundi la wahuni akiongozwa na OC-CID wa Wilaya ya Kinondoni alivamia Mkutano huo na kusababisha vurugu kubwa, kuvunja vifaa vya mbalimbali vya hoteli ya Blue Pearl ikiwemo meza na viti vyenye thamani ya shilingi 8,500,000.  Wakati Profesa Lipumba na wahuni wake hao wakifanya vurugu hizo askari wengi wa Jeshi la Polisi, walikuwepo na kushuhudia fujo hizo bila ya kuchukua hatua zozote. Hilo hatukuliona likitokea katika Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika pale Dodoma mwezi July/June mwaka huu. Chama kilitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi Kituo cha Magomeni lakini hakukuwa na hatua zozote zilizochukuliwa mpaka sasa zaidi ya kupewa RB namba MG/RB/9072/2016 ya tarehe 22 Agosi 2016.  Mkutano ule uligharimu takribani shilingi milioni mia sita. (600 milioni) bila kukamilisha ajenda yake ya pili ya kupata viongozi wa kitaifa Mwenyekiti na Makamu wake.

2. UTEKAJI WA WANACHAMA NA VIONGOZI WA CUF;

Kumekuwa na majaribio na matukio kadhaa ya utekaji wa viongozi na wanachama wa CUF lakini matukio hayo yalipotokea na kuripotiwa Polisi pamoja na ushahidi usio na shaka, wahusika hawakuchukuliwa hatua na jeshi hilo. Tarehe 16 Septemba 2016, Kaimu Naibu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wetu wa Uchumi na Fedha Mhe. Joran Bashange alitekwa akitoka nyumbani kwake Mtaa wa Madenge, Buguruni, Wilaya ya Ilala.  Walinzi wa Profesa Lipumba wanaofahamika kwa majina, sura, mahali wanapoishi na shughuli wanazofanya, walimvamia, wakamkamata na kumuingiza kwa nguvu kwenye gari aina ya Toyota NOAH yenye namba za usajili T760 CEX. Mhe. Bashange alipiga kelele kuomba msaada na wananchi wakajitokeza kwa wingi, wakawadhibiti na kuwakamata watekaji wakiwa ndani ya gari, wananchi wakaidhibiti gari husika pia. Taarifa zikafikishwa Kituo cha Polisi Buguruni, Polisi wakafika eneo la tukio, wakawakamata watuhumiwa hao wane (4) na gari lao na kuwapeleka Kituo cha Polisi Buguruni. Watuhumiwa wakahojiwa na sambamba na maelezo ya Mhe. Bashange na mashahidi kuchukuliwa. Likafunguliwa Jalada la kesi Namba BUG/IR/5937/2016 la tarehe 16 Oktoba, 2016 lakini hakuna hatua yoyote muhimu iliyochukuliwa na Jeshi la Polisi. Mpaka muda huu tunapozungumza na nyinyi wanahabari, gari lililokuwepo kituoni kama kielelezo/ushahidi imeondolewa kituoni hapo na watuhumiwa wote wameachiwa huru na wapo mitaani huku wakitamba kuwa wao wanalindwa na Jeshi la Polisi.  Mhalifu alieteka na kutishia maisha ya raia asie na hatia, pamoja na kukamatwa kwenye tukio hilo polisi wanaona hana kosa la kujibu. Sijui jeshi la polisi walitaka wananchi wachukue sheria mkononi za kuwapiga na kuwachoma moto? kama ambavyo tumeshuhudia matukio kama hayo yakitokea maeneo mbalimbali nchini kutokana na kukosekana kwa uadilifu wa kutenda haki unaofanywa na jeshi la Polisi nchini. Utekaji ni uhalifu mkubwa na haukupaswa kuachwa bila ya hatua kuchukuliwa.  Kuachiwa huru kwa watuhumiwa wa utekaji kunahatarisha sio tu usalama wa viongozi wa CUF na wanachama wake bali pia wananchi wengine. Hivi sasa wafuasi wa Profesa Lipumba wanatoa vitisho katika mitandao ya kijamii na katika mazingira ambapo wapo wanachama wa CUF bila ya khofu kwani wanaamini na kusema waziwazi kwamba Jeshi la Polisi ni sehemu yao na halitawafanya kitu.  Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wameshindwa kuchukua hatua zinazostahiki dhidi ya uhalifu huo uliomlenga kiongozi wa ngazi za juu wa Chama cha Wananchi – CUF.  Kinyume chake Jeshi la Polisi limewafikisha mahakamani kwa kuwabambikizia kesi ya jinai namba 354/2016 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, vijana 23 walinzi wa CUF (Blue Guard).  Kwa kuwa tu vijana hawa hawamuungi mkono Profesa Lipumba.

3. UVAMIZI WA AFISI KUU YA CHAMA BUGURUNI DAR ES SALAAM, TAREHE 24 SEPTEMBA, 2016:

Tarehe 24/9/2016 Prof Lipumba na wafuasi wake walivamia Ofisi Kuu ya Chama iliyopo Buguruni, Wilaya ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam kuvunja mageti na milango ya ofisi, kuwapiga walinzi binafsi wa Kampuni ya Ironsides Security Guard, kuwanyanganya silaha na kufanya uharibifu mkubwa wa mali za Chama. Kundi hilo la wafuasi wa Profesa Lipumba lilipewa ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi wakati wakitekeleza hujuma zao hizo na uvamizi huo ulipewa baraka zote na Jaji Francis Mtungi Msajili wa vyama vya siasa nchini na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Polisi ambayo kazi yake kubwa ni ulinzi wa raia na mali zao siku hiyo ilisimamia zoezi zima la uhalifu wa kijinai uliotendwa na Prof. Lipumba na wafuasi wake dhidi ya Chama cha CUF. Mpaka sasa hatuna thamani halisi ya uharibifu wa mali za chama na matumizi ya hovyo ya Magari ambayo mengine yanaonekana mtaani na makundi ya vijana wahuni. Mwenyekiti na Katibu wa Bodi ya Wadhamini walipokwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi Buguruni, OCCID aliwakatalia kupokea taarifa hiyo na kutoa sharti la kupelekewa muhtasari wa kikao cha Bodi kinachowapa mamlaka ya kutoa taarifa kituoni hapo. Hata hivyo taarifa ya uhalifu huo ilitolewa na walinzi wa Kampuni ya ulinzi ya Ironsides na kupewa RB Na.BUG/RB/8741/2016 ya tarehe 24 Septemba 2016 lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa mpaka sasa dhidi ya watuhumiwa.

4. UVAMIZI NA KUVUNJA OFISI ZA WILAYA BAGAMOYO NA MKURANGA:

Tarehe 4 Novemba 2016 Profesa Lipumba na wafuasi wake wakilindwa na Jeshi la Polisi walikwenda Ofisi za Chama za Wilaya ya Bagamoyo ambako walivunja kufuli na milango ya Ofisi za Chama na kuzifunga kwa kutumia kufuli zao mpya. Ofisi hizo zina nyaraka za Chama na hivyo shughuli za kiutendaji za Chama zimesimama. Kundi hilo pia limekwenda Mkuranga ambapo walifanya vurugu. Viongozi wetu wa wilaya hizo kupitia vikao halali vya Chama walitoa taarifa Polisi kabla ya matukio hayo, kutotambua ujio wa Lipumba lakini Jeshi la Polisi walipuuza na badala yake wakamkamata mmliki wa ukumbi na kumlazimisha kukubaliana na kufanyika kwa kikao cha Lipumba. Kuna uhalifu unaoendelea dhidi ya Chama cha CUF na dhidi ya sheria za nchi kwa kuvamia Ofisi za Chama za wilaya mbalimbali nchini na kuzifunga kwa makufuli tofauti ili kuzuia shughuli za Chama. Uhalifu huo unaratibiwa na Prof. Lipumba mwenyewe akiwa na ulinzi wa Jeshi la Polisi na kupata baraka zote na Jaji Francis Mtungi Msajili wa Vyama vya Siasa nchini. Hujuma hizo zinafanywa sehemu zote ambazo viongozi na wanachama hawamuungi mkono Prof. Lipumba na hata pale viongozi wa Chama wilayani wanapopeleka barua rasmi Polisi kutoa taarifa ya kutotambua ziara za Prof. Lipumba, Polisi wamekuwa wakitumia nguvu kuhakikisha kuwa Lipumba anatimiza azma ya kukihujumu Chama kwa kutekeleza matakwa ya wanaomtuma. Itakumbukwa kuwa licha ya kunakili taarifa ya kumtambua Lipumba kama Mwenyekiti wa Chama kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) ili ampatie ulinzi wakati wa uvamizi wa Ofisi Kuu za Chama Buguruni tarehe 24 Septemba 2016, Jaji Francis Mtungi aliandika barua nyingine kwa Profesa Lipumba yenye Kum.Na.HA.322/362/14/88 ya tarehe 28/9/2016 na kuinakili rasmi kwa IGP ambayo ndiyo inatumika kumhakikishia ulinzi kwa uhalifu unaoendelea sasa.

5. WABUNGE NA WAJUMBE WA BARAZA KUU LA UONGOZI CUF TAIFA KUZUILIWA KUFANYA KIKAO CHA NDANI NEWALA NA KUKAMATWA NACHINGWEA:

Wakati jeshi la polisi likimpa ulinzi profesa lipumba kufanya shughuli za kisiasa, maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo Mtwara Mjini, Newala, Nachingwea, Lindi, Tabora, Kahama, Bagamoyo, Mkuranga, Kisarawe, Morogoro, Kondoa na kwingineko. Tarehe 15 Oktoba,  2016 siku chache baada ya ziara ya Profesa Lipumba Jeshi la Polisi hao hao wakiwa na mabomu ya machozi na silaha za moto walivamia na kuwazuia wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na wabunge wa CUF, kufanya kikao cha ndani wilayani Newala na kuwatawanya wajumbe wote waliohudhuria. Jeshi la Polisi halikutoa sababu za kufanya hivyo. Tarehe 16 Oktoba, 2016 Jeshi la Polisi lilizuia vikao vya ndani kwa wajumbe hao Kufanyika Mtwara Mjini. Wakiwa Nachingwea Jeshi la polisi liliwakamata wajumbe wa Baraza Kuu na wabunge na kuwaweka ndani kwa mahojiano na baadae kuwaachia na kuzuia kufanya shughuli yeyote ya kisiasa ndani ya wilaya hizo.

6. KUZUIA KUFANYIKA KWA MKUTANO MKUU MAALUMU WA WILAYA YA TANGA TAREHE 29/10/2016:

Tarehe 29/10/2016 Uongozi wa wilaya ya Tanga ulinialika kuhudhuria ufunguzi wa Mkutano wao Mkuu Maalumu wa Wilaya, Jeshi la Polisi bila ya sababu za msingi na kuingilia majukumu ya kiutendaji kisiasa wakadai kuwa kwa kuna pande mbili zinazovutana juu ya kumtambua Meya wa Jiji aliyetangazwa kwa kutumia mabavu na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga au wasimtambue. Jeshi limeonelea liingilie kati suala hilo kwa kuzuia kufanyika kikao cha kikatiba ambacho kilipaswa kulipatia ufumbuzi suala hilo kwa kutoa mapendekezo yake kwa Baraza Kuu la Uongozi wa Taifa, kutokana na kupata taarifa ya zuio hilo nikalazimika kutokwenda Tanga kwa ajili ya shughuli hiyo.


7. UTEKAJI WA MLINZI WA CHAMA ULIOFANYIKA MAHAKAMA KUU TAREHE 10/11/2016:

Tukio lingine la utekaji lilifanywa tarehe 10 Novemba, 2016 maeneo ya Mahakama Kuu ya Tanzania. Siku hiyo shauri namba 23/2016 lilipangwa kutajwa.  Baada ya kesi kuahirishwa, wafuasi wa Profesa Lipumba waliovalia fulana zenye picha yake, waliwavamia viongozi wa Chama na wanachama kwa lengo la kuwashambulia. Vijana wa ulinzi wa CUF walifanikiwa kuwaokoa viongozi hao na kuwaweka katika jengo la Sukari House na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi juu ya tukio hilo. Katika tukio hilo wafuasi wa Prof. Lipumba walimkamta mlinzi mmoja wa Chama Mhe. Mohamed Said na kwenda naye mpaka Buguruni na kumkabidhi kwa Prof. Lipumba ambaye alimuhoji kwa nini anakataa kumuunga mkono katika harakati zake. Wakati akiwa mikononi mwao, wafuasi hao wa Prof. Lipumba walimpiga sana mlinzi huyo wa Chama, kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo kichwani na mdomoni, na kumpora fedha, simu, vidani na kila kitu alichokuwa nacho na kisha kumwachia. Tukio la kutekwa Mohamed Said lilitokea mbele ya Askari wa Jeshi la Polisi waliokuwa na gari lakini waliangalia bila kuchukua hatua yoyote. Watekaji hao walijipiga picha wakati wanafanya tukio hilo na kurusha kwenye mitandao ya kijamii huku wakitamba na kutoa vitisho zaidi kwa viongozi na wanachama wa CUF! Taarifa za tukio hilo zilitolewa kwa Jeshi la Polisi kituo kikuu cha kati (Central Police) na baada ya kuzungushwa sana, Mohamed Said alipewa fomu ya PF3 kwa ajili ya matibabu na kufunguliwa jalada Na.CD/CID/PE/88/2016 la tarehe 10/11/2016, lakini hadi sasa hakuna taarifa wala juhudi za Polisi kuwakamata watuhumiwa ambao wote wapo Ofisi za Chama Buguruni wanakokaa kwa mabavu na kupewa msaada wa kiusalama na Jeshi la Polisi.

8. KUHUSU JESHI LA POLISI KUZUIA KUFANYIKA KWA KIKAO CHA NDANI MKOANI MTWARA NA LINDI:

Ndugu Wahariri na Waandishi  wa Habari,

Jumamosi ya tarehe 19 Novemba, 2016 na Jumapili tarehe 20 Novemba, 2016 Chama chetu kilipanga kufanya ziara ya ukaguzi wa shughuli za Chama na kufanya vikao vya ndani katika Mkoa wa Mtwara na baadae Mkoa wa Lindi. Tarehe 16/11/2016 Nilimuandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini -IGP ya kumjulisha kwa maana ya kutoa taarifa ya ziara yangu kwa barua yenye Kumb.Na.CUF/HQ/AKM/003/016/032 na pia niliwajulisha Wakuu wa Jeshi la Polisi Mkoa (Ma-RPC) wa Lindi na Mtwara kwa barua Kumb. Na. CUF/HQ/AKM/003/016/030 ya tarehe 16 Novemba 2016. Kwa mujibu wa sheria hatupaswi kuomba kibali au kutoa taarifa kwa jeshi la Polisi kwa utekelezaji wa shughuli za Chama kwa vikao vya ndani, hata hivyo kutokana na hali ya kisiasa nchini na ili kuepuka migongano isiyo ya lazima na pengine kusababisha muingiliano wa majukumu na kuharibu rasilimali chache zilizopo kwa madhumuni ya kufanikisha shughuli yetu tukaonelea ni vyema kuwajulisha kwa kuwapa taarifa ili kama kuna suala lolote linalohitaji kushauriana tuweze kutoa ushirikiano unaofaa.  Wasaidizi wangu walitangulia Mtwara siku tano kabla ya ziara na walipata fursa ya kuonana na RPC na Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya- OCD na kuwajulisha juu ya ziara hiyo. Baada ya mazungumzo na maelekezo kadhaa waliyotoa na kuweza kukamilishwa OCD wa Mtwara (Ndugu I.M.MUSHI-SSP) aliandika barua ya kukubaliana na kuendelea na maandalizi ya kikao hicho kwa barua ya tarehe 18/11/2016 yenye Kumb. Na. MT/32/VOL.VIII/200. Barua hizo tumeziambatanisha na taarifa hii. Vilevile kwa upande wa Mkoa wa Lindi, OCD Ndugu AGUSTINE G. TITUS-SP baada ya kukutana na viongozi wetu wa wilaya na kujulishwa juu ya Ziara hiyo na kumuachia Barua ya kumtaarifu alikubaliana na ziara hiyo na kuahidi kutoa ulinzi na kuwataka waendelee na maandalizi pamoja na kuwashauri kuwa wasitumie pikipiki katika mapokezi ili kuepusha msongamano na ajali.

Jumamosi majira ya saa 2 asubuhi wakati viongozi na wanachama wakiwa wamefika uwanja wa ndege wa Mtwara kwa ajili ya kunipokea, OCD wa Mtwara alipeleka vijana wake (askari polisi) wengi eneo la ukumbi wa kikao kilichopangwa kufanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha SAUT-PARISH na kutawanya watu na kuzuia kuingia chuoni hapo hata kwa wanafunzi na wafanyakazi huku wakiendesha msako mkubwa kwa kila anayefika hapo na kufanya ukaguzi wa vitambulisho kwa kila aliyetaka kuingia chuoni hapo. Askari walikwenda ukumbini na kuwataka watayarishaji kuacha kufanya matayarisho ya ukumbi huo na kuwataka waondoke. Lakini pia alituma askari kadhaa uwanja wa ndege kuja kudai kupewa barua yake aliyoandika kukubaliana na kufanyika kwa kiako hicho na kuwachukua wasaidizi wangu na walinzi wetu kwenda nao kituoni. Mara walipofika kituoni wakatoa barua ya kuzuia kufanyika kwa kikao hicho masaa mawili kabla ya kuanza kwa kikao kwa madai kuwa kuna taarifa ya kufanyika kwa vurugu na kuna zuio la kufanyika kwa kikao hicho kutoka kwa katibu wa CUF wilaya. Kutokana na sababu za kiusalama jeshi la Polisi limezuia kufanyika kwa kikao hicho. Magari kadhaa ya askari na magari ya maji ya washawasha yalikuwa yakipita kila eneo la mjini Mtwara kutisha watu na kuonyesha kama kuna tukio la hatari. Tukalazimika kuitisha mkutano na vyombo vya habari na muda huohuo baada ya RPC kujulishwa kuwa CUF inataka kuzungumza na waandishi naye akaitisha mkutano na waaandishi wa habari kuzungumzia suala hili mbali na hapo awali kudai kuwa masuala haya ni ya OCD-Mtwara.  Baada ya majadiliano marefu na Wabunge wetu na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi CUF Taifa wakadai kuwa wao wamepokea amri kutoka juu ya kuzuia kufanyika kwa kikao hicho. Wakati Mtwara wanadai kuwa wamepokea barua ya katibu wa CUF wilaya ikiwa ndio sababu moja wapo ya kuzuia kikao hicho, OCD wa Lindi yeye alidai alizuia kutokana na taarifa za kiitelijensia na sababu za kiusalama ingawa hakuna kiongozi yeyote wa CUF wilaya ya Lindi Mjini aliyekuwa anapingana na ziara hiyo. Baada ya kujadiliana sana na viongozi wetu wa wilaya na Wabunge wetu baadae nao wakadai kuwa wamepokea amri kutoka juu. Wabunge wetu walifanya juhudi za kumtafuta Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) na Waziri wa Mambo ya Ndani na wote Walipatikana. Hata hivyo majibu ya IGP yalikuwa yanaunga mkono maamuzi yaliyochukuliwa na watendaji wake.

9. WALINZI WA PROFESA LIPUMBA KUTAKA KUZUIA VIONGOZI WA CUF WASIINGIE NDANI YA CHUMBA CHA MAHAKAMA KUFUATILIA SHAURI:

Tarehe 24/11/2016 kesi dhidi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini na wenzake ilipangwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kutajwa. Kutokana na ujumbe wa vitisho uliokuwa unasambazwa mitandaoni Mwenyekiti wa kamati ya uongozi CUF taifa Mheshimiwa Julius Mtatiro alifanya mawasiliano na Jeshi la Polisi kuwajulisha hali halisi jinsi inavyoendelea. Hata hivyo hazikuchukuliwa hatua sahihi za kuzuia viashiria vya vurugu mahakamani hapo. Walinzi wa Profesa Lipumba walitaka kuzuia viongozi wa CUF wasiingie ndani ya chumba cha Mahakama kufuatilia shauri hilo. Vurugu zikatokea na baadae Mheshimiwa Jaji Akalazimika kuita askari wa Jeshi la Magereza ambao walikuwepo Mahakamani hapo.

Orodha ya matukio ya uhalifu na hujuma dhidi ya Chama chetu ni ndefu na si rahisi kuielezea yote kwani ni historia ya kuandikiwa kitabu. Hata hivyo, tumeona ni vyema kubainisha haya machache kwa kina ili kutoa picha halisi ya ushirika uliopo kati ya Profesa Lipumba, Msajili wa Vyama vya siasa na Jeshi la Polisi. Nimechukua hatua za kumtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. Hata hivyo sikuweza kuonana naye kutokana na kubanwa na majukumu ya kazi. Nimemuandikia barua tarehe 24/11/2016 yenye Kumb. Na CUF/HQ/OKM/2016/VOL.003 kwa madhumuni ya kumueleza yanayofanywa na watendaji wa wizara yake na kumuomba kuchukua hatua za kurekebishwa hali hii.

Sisi kwa upande wetu kama Chama inatutia shaka kubwa kuona Jeshi la Polisi linakuwa ni sehemu ya mkakati huu dhidi ya CUF. Jeshi la Polisi ni chombo kilichotarajiwa kulinda usalama wa raia na mali zao. Inashangaza sana kuona jeshi hilo likishirikiana na wahalifu kuhatarisha usalama wa raia na mali zao. Chombo kilichotarajiwa kukamata wahalifu na kuwachukulia hatua kwa kuwafikisha katika vyombo vya sharia, leo tunashuhudia chombo hicho kikiwalinda wahalifu na kuwakingia kifua wasifikishwe mbele ya vyombo vya sheria. Chombo kilichotarajiwa kusimamia sheria za nchi, leo Chombo hicho tunakishuhudia kikisimamia uvunjwaji wa sheria za nchi. Chombo kilichotarajiwa kutenda haki kwa raia wote bila ubaguzi, leo chombo hicho kinafanya ubaguzi wa wazi kwa kulazimisha haki kwa kundi moja dogo na kunyima haki hiyo kundi jengine ambalo ni kubwa. Yote haya yanafanywa kwa maslahi ya kisiasa. Jeshi la Polisi leo linatulazimisha kuliona kuwa ni sehemu ya wenye maslahi ya kisiasa katika kile kinachoitwa Mgogoro wa Uongozi ndani ya CUF.

Baada ya miaka 54 ya kujitawala pamoja na mara kwa mara kulitaka Jeshi la Polisi kujiepusha kufanya kazi zake kwa misingi ya kiushabiki wa kisiasa,  Jeshi la Polisi nchini limeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa waledi na kwa kuzingatia Haki, Usawa na kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. Jeshi la Polisi limekuwa likiingilia na kuzuia utekelezaji wa shughuli za kawaida na za kikatiba za chama chetu, na kushirikiana na kuwalinda wahalifu wanaotishia maisha ya wanachama wetu na viongozi wake, uharibifu wa mali za Chama, na kufanya vitendo vinavyohatarisha amani na utulivu wa nchi yetu. Aidha, kumekuwa na vitendo vya kihalifu na vya kijinai ambavyo vimefanywa na baadhi ya watu wasio na nia njema na chama chetu cha CUF na viongozi wake mbali na wananchi kujizuia kuchukua sheria mkononi (kwa kuwadhuru wahalifu) Jeshi la Polisi pamoja na kukabidhiwa wahalifu hao wameshindwa kuchukua hatua za kisheria kwa kuwafikisha mahakamani na badala yake wamekuwa wakishirikiana nao kufanya njama ovu dhidi ya chama na viongozi wake. Jeshi la polisi limekuwa likishirikiana na kuwatii wahalifu bila shuruti. Ni vizuri tukajenga taasisi imara za kidemokrasia nchini na tukashindanisha hoja zetu kuliko kutumia mabavu ya vyombo vya dola kukandamiza demokrasia. Mwenendo huo hautasaidia kustawisha jamii yetu na kupata maendeleo endelevu kwa mustakbali mwema wa Taifa.

HITIMISHO:

Ndugu Wahariri na Waandishi wa Habari,

Sote tunafahamu na ni mashahidi kuwa Profesa Ibrahimu Lipumba alijiuzulu kwa matashi yake mwenyewe, mchana kweupe mbali na sisi wote kama viongozi wenzake kumnasihi na kumshauri kutofanya hivyo kwa wakati ule. Wanachama wa rika zote na viongozi wa madhehebu ya dini mbalimbali walimnasihi sana sana kuacha kufanya hivyo lakini alikataa katakata na kuendelea na msimamo wake wa kung’atuka katika uongozi wa Chama katika Hotel hii hii ambayo leo tunazungumza nanyi. Hoja yake wakati ule ilikuwa kwamba Dhamira na nafsi yake zinamsuta. Kwamba hakubaliani na masuala kuhusu UKAWA, hasa ya kusimamisha mgombea mmoja wa nafasi ya Urais.Tarehe 5/8/2015 aliandika barua hiyo ya kujiuzulu.

Alituacha katika wakati mgumu sana tukiwa katika maandalizi makubwa ya kushiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana na katika kipindi ambacho Makamu Mwenyekiti wetu, Mheshimiwa Juma Duni Haji alishahamia CHADEMA kwa makubaliano kuwa Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kukidhi matakwa ya kikatiba na sheria za Uchaguzi. Sote ni mashuhuda wa mafanikio ya Ushirikiano wa vyama vyetu katika UKAWA. Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC ulimpa mgombea wetu Mheshimiwa Edward Lowassa asilimia 39.% ya kura, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa katika historia ya chaguzi zote zilizopita. Huko Zanzibar CUF tumeshinda nafasi ya Urais na kushuhudia CCM na Dola kulazimisha kwa kumuamuru Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar –ZEC, kufuta uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 na matokeo halali ya uchaguzi wa Oktoba 25, 2016. Mheshimiwa Edward Lowassa amemshinda Mhe. Magufuli katika matokeo ya kura za urais Zanzibar. Kwa mashirikiano yetu tumeweza kufanya Kampeni kubwa za kisasa zilizoleta ushindani mkubwa na kufanikiwa CUF kupata wabunge katika majimbo kumi (10) ya Tanzania Bara na kuongoza Halmashauri nne nchini. Grafu ya mafanikio kwa CUF na kwa watanzania wapenda mabadiliko imepanda kwa kiwango cha kuridhisha. Bila shaka kujiuzuru kwa Profesa Lipumba imeleta athari kwa CUF na upinzani kwa jumla, ikiwemo kupoteza baadhi ya majimbo na madiwani, kwani CCM waliitumia nafasi hiyo kueneza propaganda chafu wakati wa kampeni. Hakuna Mtanzania ambaye mwenye chembe kidogo kabisa ya kupenda mabadiliko ya kisiasa nchini ambaye hakuumizwa na maamuzi ya ‘Bwana yule’ Chama cha CUF ni Chama cha kidemokrasia, maamuzi yetu yote hupitishwa na vikao rasmi vya Chama ambavyo kwa ngazi ya Taifa ni Kamati ya Utendaji au Baraza Kuu la Uongozi. 

Nasikitika kusema kuwa sababu za kujiuzulu kwake sasa zimekuwa zikibadilika siku hadi siku. Mara  Wazanzibar hawamtaki yeye, Mara Maalim Seif Hamtaki Profesa Lipumba, mara inataka iaminishwe kuwa kuna mgogoro baina ya Maalim Seif na Profesa Lipumba. Amekuwa akifanya propaganda za kuwagawa wanachama katika misingi ya Utanganyika na Uzanzibari. Katika vikao vyake vya ndani anasema tunataka kujitoa katika makucha ya Wazanzibari, eti rasilimali za Chama zitumike Tanganyika, eti Wazanzibari wanapendelewa, na eti Chama kimeuzwa na au kinataka kuuzwa kwa CHADEMA na LOWASSA. Wakati mwingine anazungumzia udini. Ndugu zangu haya yote si kweli hata kidogo na hayana mashiko. Profesa Lipumba bado hajasema sababu za kujiuzulu kwake. Aseme sababu za kujiuzulu kwake, asirukeruke.

Suala la UKAWA nani aliyeleta UKAWA ndani ya CUF ?  UKAWA umeanzia Bunge la Katiba. Katibu Mkuu Maalim Seif hakuwa mjumbe wa Bunge la Katiba. Yeye Profesa Lipumba ndiye aliyekwenda kumuona Lowassa na kumtaka ikiwa CCM itamuengua ajiunge na UKAWA. Akashauri ajiunge na NCCR–Mageuzi na CHADEMA na CUF tumuunge mkono. Ni yeye aliyemgotoa kwa waandishi wa Habari. Leo hii yule aliyekuwa anamuita msanii na angemfanya waziri wa sanaa ili aandae mashindano ya warembo ndiye amekuwa rafiki mkubwa wa ‘Bwana yule’ na ndiye aliyesimamia uharibifu wa matokeo ya uchaguzi Zanzibar. Na kama anasema amekosana na Katibu Mkuu Maalim Seif jambo ambalo halijawahi kutokea, na yeye mwenyewe amewahi kukaririwa akisema hivyo. Siku za hivi karibuni lugha imebadilika. Anazungumzia ubaguzi, ‘Usultan’ na ‘Udikteta’ ambao nao ndani ya dhati ya nafsi yake anajua pia kuwa suala hilo ndani ya CUF halipo, Je? aliyawasilisha katika kikao gani cha Chama ili kuyazungumzia masuala haya  kama yalikuwepo ili kuyapatia ufumbuzi? Mahala gani Duniani kuna kiongozi wa juu wa taasisi kubwa kama ya CUF ambaye aliandika barua ya kujiuzulu na kuiacha ofisi yake kwa muda wa miezi kumi, taasisi ikachagua au kuteua kiongozi mbadala wa nafasi hiyo kisha baadae mtu huyo akalazimisha kurejea katika nafasi yake? Profesa LIpumba hakufukuzwa, alijiuzulu kwa hiari yake sasa inakuaje kulazimisha lazima aendelee kuwa mwenyekiti wa Taifa. Mimi naamini hang’ang’anii kwa nia njema. Labda alidhani alipojiuzulu Chama kingeyumba na kufanya vibaya katika uchaguzi. Pia alidhani UKAWA ungeyumba. Matokeo yake yakawa tofauti sana. Ilipoonekana kuwa Wazanzibari na CUF tumekaza uzi katika kudai haki yetu ya kuporwa ushindi wetu, Profesa Lipumba ndio akaja na mpya ya muongo kutengua barua ya kujiuzulu. Nia ikiwa tuache kudai haki yetu na tushughulikie kinachoitwa mgogoro katika Chama. Tunaendelea kudai haki yetu na papo hapo kujidhatiti kuimarisha umoja ndani ya Chama. Chama cha CUF kina ngazi za maamuzi Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lenye wajumbe 63 kwa uwiano sawa kwa pande zote mbili za Muungano. Wajumbe wane (4) wamehama Chama, Mjumbe mmoja amefukuzwa chama na wajumbe sita wamesimamishwa uanachama. Kati ya wajumbe 53 waliobaki wajumbe 46 walikubaliana kwa pamoja na kuazimia kumvua uanachama Profesa Lipumba, kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukiukaji wa katiba na kanuni za chama, na dhamira ovu iliyojidhihirisha dhidi ya Chama. Si Maalim Seif aliyefanya hivyo, Ni maamuzi ya kikao halali. Mashirikiano ya UKAWA yalipata Baraka ya Baraza KUU la Uongozi Taifa na baadae Mkutano MKUU wa Kawaida wa Chama uliofanyika Ubungo Plaza Mwezi June 28-30 Mwaka 2014 wa kujaza nafasi za uongozi kwa kipindi cha miaka mitano. Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu muhimu tuzingalie changamoto na mapungufu yaliyojitokeza katika ukawa mwaka jana 2015 kuelekea Uchaguzi Mkuu na turekebishe dosari hizo tusonge mbele.

Katika kuendeleza hujuma za wazi dhidi ya CUF Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ilimuandikia Meneja wa Benki ya NMB tawi la Ilala amtambue Profesa Lipumba kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CUF na aruhusu kufungua akaunti mpya ya Chama itakayosimamiwa nay eye Profesa Lipumba ili aweze kupewa ruzuku ya Chama hali akijua hata kama angekuwa ni Mwenyekiti halali wa CUF kwa mujibu wa taratibu na katiba ya CUF Mwenyekiti hausiki na mambo ya fedha, iliposhindikana kumfungulia Profesa Lipumba akaunti Msajili amezuia ruzuku kwa CUF ili tukwame. Profesa Lipumba hana mamlaka ya chochote kwa sasa katika Chama kwa kuwa Baraza Kuu la Uongozi Taifa limeshamchukulia hatua za kinidhamu na yeye amekata rufaa kwa Mkutano Mkuu wa Taifa juu ya maamuzi hayo. Baraza Kuu la Uongozi Taifa kwa mujibu wa katiba ibara ya 118 limeteua Kamati ya Uongozi Taifa inayoongozwa na Mheshimiwa Julius Mtatiro. Kamati hii ni halali na inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

Ndugu wahariri na waandishi wa Habari,

Tumekuelezeni haya si kwa lengo la kulalamika tu, bali tunaweka kumbukumbu sahihi ya mtiririko wa matukio katika historia ya demokrasia na kuendeleza utaratibu wetu tangu kuasisiwa kwa CUF. Na kutoa tanbihi kwa Jeshi la Polisi na taasisi nyengine za kitaifa kama Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kufuata sharia zilizopelekea kuundwa huko badala ya kuwa ni sehemu ya kutengeneza machafuko na mifarakano kwa maslahi ya kisiasa.  Vyombo vya dola havikutarajiwa kuweza kukubali kutumiwa kwa maslahi ya kundi Fulani la kisiasa.

Itakumbukwa kuwa CUF imevuka vigingi vizito katika nyakati tofauti kila ilipojaribiwa ikiwa kwa uadui wa ndani au wa nje. Na kwa ithibati, dhati na imani kubwa ni kwamba mwisho wa vitimbi hivi vyote, CUF itaibuka mshindi. Tunatoa wito kwa wanachama, wapenzi wa CUF, na watanzania wote kwa ujumla wapenda mabadiliko, waendelee kuwa na Subira. Hakika hili litapita. Subra uvuta kheri.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

HAKI SAWA KWA WOTE

MAALIM SEIF SHARIF HAMAD


KATIBU MKUU
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment