Leo Jumatano bunge la Israel limeahirisha zoezi la
kuipigia kura miswada miwili yenye utata, mmoja ukiwa ni ule wa kuweka vizuizi
vya matumizi ya spika kwa ajili ya adhana misikitini na ule wa kuhalalisha maelfu
ya makazi ya walowezi wa Kiyahudi katika eneo la Ukingo wa Magharibi.
Kura hiyo imeahirishwa mpaka siku ya Jumatatu kufuatia
uamuzi wa mawaziri wa serikali, msemaji wa bunge ameliambia shirika la habari
la AFP.
Wabunge walitarajiwa kuupigia kura muswada wa kuzuia matumizi
ya spika kwa adhana za alfajiri misikitini, hatua ambayo imewakasirisha
Waislamu.
Aidha, muswada wa kuhalalisha mradi wa makazi 4,000 ya
walowezi katika eneo la Ukingo wa Magharibi ulitarajiwa kusomwa kwa mara ya
kwanza, lakini nao pia uliahirishwa.
Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa zoezi la
kura liliahirishwa kwa sababu ya hofu ya kutopatikana kwa wingi wa kura za
kutosha. Majadiliano yalikuwa yakiendelea kuhusu miswada yote miwili.
Muswada wa sauti ungepiga marufuku matumizi ya spika
kati ya saa 5 usiku na saa 1 asubuhi. Ingezihusu rasmi dini zote, lakini ni
muswada unaotazamwa kuwa unawalenga Waislamu na misikiti yao.
Wakosoaji wa serikali wanasema kuwa hatua hiyo haina
umuhimu na inatishia uhuru wa dini bila sababu za msingi. Rais wa Israel, Reuven
Rivlin ni miongoni mwa wale wanaoupinga muswada huo.
Muswada wa makazi ya walowezi umeutia majaribuni muungano
wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, ambao unaonekana kuwa wenye mrengo mkali
zaidi katika historia ya utawala huo.
Netanyahu hataki muswada huo upite akionya kuwa unaweza
kukiuka sheria za kimataifa na kusababisha kushitakiwa katika Mahakama ya
Kimataifa ya Uhalifu.
Mataifa mengi, ikiwemo Marekani, yameukosoa vikali muswada
huo na Netanyahu ana wasiwasi juu ya radiamali ya kimataifa.
Lakini pia anakabiliwa na changamoto ya kuuweka pamoja
muungano wake na asionekane kama mpinzani wa mradi huo mkubwa wa makazi ya
walowezi.
Jumuiya ya Kimataifa inayachukulia makazi yote ya
walowezi wa Kiyahudi katika eneo la Jerusalem ya Mashariki na Ukingo wa
Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel kuwa ni makazi haramu, iwe kwa
kuidhinishwa na serikali au la.
0 comments:
Post a Comment