Rais wa Uzbekistan, Islam Karimov, amefariki dunia akiwa
na umri wa miaka 78 baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kiharusi yaliyomuweka
katika hali mbaya, kwa mujibu wa duru tatu za kidiplomasia.
"Ndiyo, amefariki dunia,” kilisema chanzo kimoja
kuhusu kiongozi huyo mkongwe ambaye alikuwa hospitalini tangu Jumamosi
iliyopita.
Serika ya nchi hiyo ilitoa taarifa leo kuwa Rais huyo alikuwa
katika hali mbaya kufuatia tetesi kwamba rais huyo aliyeitawala nchi hiyo kwa
miaka 27 alikuwa karibuni kupoteza maisha.
"Ndugu wananchi, kwa masikitiko makubwa tunawataarifu
kuwa afya ya Rais wetu imezorota sana ndani ya saa 24 na kufikia kiwango cha
umahututi, kwa mujibu wa madaktari,” serikali ilisema katika taarifa yake.
Tangazo la leo linafuatia ripoti zisizokuwa rasmi
zilizoenea kwa siku kadhaa kuwa Karimov alikuwa anakaribia kufariki dunia au
amefariki. Binti yake Lola alisema mapema wiki hii kuwa kiongozi huyo mwenye
umri wa miaka 78 alitokwa na damu nyingi kwenye ubongo wake.
Karimov ameitawala nchi hiyo ya Asia ya Kati tangu mwaka
1989. Hajaonekana hadharani tangu katikati mwa mwezi Agosti, na wiki iliyopita
serikali yake ilikiri kuwa alikuwa mgonjwa.
Mnamo siku ya Alhamis, Uzbekistan ilisherehekea Sikukuu
ya Uhuru na ilidhaniwa kuwa serikali ingetoa taarifa kuhusu hali yake, hata
hivyo haikuchukua hatua hiyo.
Mtandao wa habari unaoheshimika katika eneo la Asia ya
Kati, Fergana.ru, mapema leo uliweka picha mbalimbali kutoka mji wa Samarkand
aliozaliwa Karimov, zikionesha watu wakifanya kazi kwenye eneo la makaburi ya
kihistoria ambapo familia ya Karimov imezikwa.
Hali ya afya ya Karimov iliibua wasiwasi kwamba Uzbekistan
ingeweza kutumbukia katika mapigano ya kikabila kugombania madaraka, jambo
ambalo watu wenye msimamo mkali wangeweza kulitumia kama fursa.
0 comments:
Post a Comment