MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imewaachia
huru wabunge watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliokuwa wanakabiliwa na
mashitaka ya kuomba rushwa ya Sh milioni 30. Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius
Mwijage aliwaachia huru washitakiwa hao baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),
kuwasilisha hati ya kuwafutia mashitaka.
Wabunge hao na majimbo yao katika mabano ni Kangi Lugola
wa Mwibara mkoani Mara maarufu kama ‘Nyoka wa Shaba,’ Suleiman Saddiq ‘Murad’
(Mvomero – Morogoro) na Victor Mwambalaswa (Lupa – Songwe). Awali Wakili wa
Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi akisaidiwa na Wakili Emmanuel Jacob
kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), waliieleza mahakama
kuwa kesi hiyo imetajwa kwa ajili ya washitakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Kishenyi alidai mbali na kutaka kuwasomea maelezo ya
awali washitakiwa hao, DPP anaomba kuwafutia mashitaka yao kwa kuwa hana nia ya
kuendelea na mashitaka dhidi yao.
Baada ya maelezo hayo, Wakili wa Utetezi, Mpale Mpoki
aliiomba mahakama itoe agizo ili apewe maelezo ya mlalamikaji. Hakimu Mwijage
alisema, mahakama imekubali ombi la DPP hivyo kuanzia sasa wabunge hao wapo
huru.
Aidha, alisema wakili Mpoki anatakiwa afanye juhudi
kwenda katika ofisi za DPP ili kupata taarifa hizo, kinyume cha hapo mahakama
haiwezi kutoa amri kwamba apatiwe maelezo hayo.
Baada ya washitakiwa hao kuachiwa huru, ndugu na
marafiki wa wabunge hao waliokuwa wamefika mahakamani, walianza kuangua kilio
cha furaha. Akizungumza kwa niaba ya wabunge wenzake, Lugola alisema watakaa na
wanasheria hao ili wajue nini cha kufanya kutokana na udhalilishaji
waliofanyiwa na Takukuru.
"Tumesikitishwa sana na kitendo cha Takukuru
walivyotufikisha mahakamani na kutushitaki kwa kashfa ya rushwa na dunia nzima
imetambua, lakini tangu tufike mahakamani mioyo yetu ilimtanguliza Mungu na leo
(jana) Mungu ametoa majibu,” alisema Lugola.
Alisema walikuwa wanajua kuwa kesi hiyo ni ya kutunga na
ilijaa siasa kwa kuwa awali Takukuru ilisema upelelezi umekamilika, lakini
hawakuwa na ushahidi na ndio maana wameamua kuifuta.
Kwa mara ya kwanza wabunge hao walipandishwa kizimbani,
Aprili mosi mwaka huu wakidaiwa kuwa Machi 15 mwaka huu, kati ya saa mbili na
saa nne usiku, katika Hoteli ya Golden Tulip, Kinondoni jijini Dar es Salaam, kwa
pamoja wakiwa kama wabunge na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali za Mitaa (LAAC), waliomba na kushawishi kupewa rushwa ya Sh milioni
30.
Inadaiwa waliomba fedha hizo kutoka kwa Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Gairo, Mbwana Magotta, kama kishawishi
cha kutoa mapendekezo ya hati safi kwa halmashauri hiyo, jambo ambalo ni
kinyume cha sheria.
Kupandishwa kizimbani kwa wabunge hao kulitokana na
kashfa ya rushwa iliyomsababisha Spika wa Bunge, Job Ndugai kupangua wenyeviti
na makamu wenyeviti kwa kuwaondoa kwenye kamati walizokuwa wanaziongoza.
Mabadiliko hayo yaliwagusa pia wabunge 27, ambao baadhi yao wanadaiwa
kujihusisha na vitendo vya rushwa.
0 comments:
Post a Comment