Baadhi ya magazeti ya Marekani yanaona kuwa mkutano wa Rais Erdogan na Rais Putin utadhoofisha uhusiano kati ya Uturuki na mataifa ya Magharibi |
Licha ya juhudi za maafisa wa Marekani za kutoupa uzito
ukaribu wa Uturuki na Urusi baada ya mkutano wa Marais Recep Tayyip Erdogan na
Vladmir Putin na kusema kuwa hautadhoofisha uhusiano kati ya Marekani na
Uturuki, na kwamba hakauna mvutano kati ya Washington na Ankara tangu jaribio
la mapinduzi lililotokea katikati ya mwezi uliopita, mtu anayefuatilia vyombo
vya habari vya Marekani atagundua kuwa Washington imekerwa na ukaribu huo,
lakini haijafikia kiwango cha kutia wasiwasi.
Gazeti la New York Times katika toleo lake la Agosti 9,
limeeleza kuwa Urusi na Uturuki zilikubaliana kuboresha uhusiano wao, ambapo
Magharibi inalifuatilia jambo hilo kwa wasiwasi na kutolifurahia.
Gazeti hilo limeeleza kuwa ukaribu huo “utadhoofisha
uhusiano wa Uturuki na mataifa ya Magharibi na Jumuiya ya Kujihami ya NATO, kwa
sababu Putin anafanya juhudi za kuivuta Ankara kwenye kambi yake” na hilo ndilo
litakalomfanya atengwe na Magharibi.
Kauli hiyo inafanana na ile ya gazeti la Washington Post
lililosema kwamba “hatua ya Erdogan kumgeukia Putin inatokana na uhusiano mbaya
na Magharibi”.
MAMBO HAYAJAANZA LEO
Hata hivyo, mwandishi mwandamizi wa masuala ya Uturuki
na Marekani, Elhan Taner, ametupilia mbali wazo la kwamba ukaribu wa Uturuki na
Urusi utaongeza mvutano kati ya Washington na Ankara kwa sababu uhusiano kati
ya mataifa hayo haujaanza kuwa mbaya leo, bali umekuwa mbaya kwa miaka mingi,
na umezidi kuzorota baada ya jaribio la mapinduzi lililofeli.
Anasema: “Ninaamini kuwa uhusiano huo umekuwa mbaya
zaidi kuliko hata mwaka 1974 pale Congress ilipoiwekea vikwanzo Ankara kwa
sababu ya kulimega eneo la Cyprus kaskazini kutoka kwa Ugiriki”. Na akaongeza
kuwa mivutano katika uhusiano huo ilianza baada ya mapinduzi ya Bustani ya Gezi
mjini Istanbul mwaka 2013, na tangu wakati huo uhusiano kati ya mataifa haya
mawili umeendelea kuwa mbaya.
Mwandishi huyo anaona kwamba jaribio la mapinduzi nchini
Uturuki lilizidisha kuzorota kwa uhusiano baina ya Marekani na Uturuki kwa
sababu nyingi, kubwa kabisa ikiwa ni hatua ya Washington kukataa kumkabidhi
kiongozi wa kundi la Hizmet, Fethullah Gulen, ambaye anatuhumiwa kuwa kinara wa
jaribio hilo, na hatua ya Ankara kuikosoa kambi ya Magharibi kwa kutosimama
upande wa Uturuki au hata kufanya ziara ya kutoa mkono wa pole. Hiyo inaonesha
kuwa Washington na mataifa ya magharibi hazibadili misimamo yake.
IMANI THABITI
Taner anaona kuwa mataifa ya Magharibi yanaweza kuwa
yanautazama ukaribu wa Uturuki na Urusi kwa kukereka na hata wasiwasi, lakini
mataifa hayo yana imani thabiti kuwa Moscow haiwezi kuwa mbadala kwa Magharibi
kwa Uturuki kwa sababu ya matatizo ya kiuchumi na kijeshi yanayoielemea. Na anasema
kuwa Uturuki inajaribu kutoa picha kwamba Putin ni mbadala wa Magharibi, lakini
Washington haiamini hilo.
Mvutano mkali katika uhusiano wa mataifa hayo mawili ulijionesha
wazi katika kauli ya mwisho iliyotolewa na Rais wa Uturuki kabla ya ziara yake
nchini Urusi, ambapo alisema kuwa Washington inapaswa kuchagua kati ya Uturuki
au kuendelea kumhifadhi Gulen ambaye Ankara inamtuhumu kupanga jaribio la
mapinduzi lililoshindwa.
Baadhi ya Waturuki wanaituhumu Washington kuwa ilikuwa
na mkono kwenye jaribio hilo, jambo ambalo lilimfanya msemaji wa Wizara ya
Mashauri ya Kigeni ya Marekani kusema kuwa kauli hiyo haisaidii kuboresha
mambo.
Aidha, kuna habari za uwezekano wa waziri wa mashauri ya
kigeni wa Marekani, John Kerry, kuitembelea Uturuki katika wiki ya mwisho ya
mwezi huu kwa lengo la kujaribu kutuliza mvutano kati ya mataifa hayo mawili,
lakini wizara ya mambo ya nje ya Marekani haijathibitisha ziara hiyo mpaka sasa.
Wafuatiliaji wa mambo wanaona kuwa ziara hiyo
ikifanyika, haitaweza kuleta mabadiliko ya haraka kwenye uhusiano huo
uliozorota, hasa iwapo Washington itaendelea kumhifadhi Gulen na kukataa
kumkabidhi kwa Ankara.
Ungana nasi katika WhatsApp: +255 712 566 595
0 comments:
Post a Comment