Rais Erdogan (kulia) alipokutana na Rais Putin (kushoto) pembezoni mwa kilele cha mkutano wa G20 uliofanyika mjini Antalya, Uturuki mwezi Novemba mwaka jana. |
RAIS wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan anatarajiwa leo
kukutana na Rais wa Urusi, Vladmir Putin mjini San Petersburg katika ziara yake
ya kwanza nje ya nchi baada ya jaribio la mapinduzi lililoshindwa.
Mkutano huo utakuwa wa kwanza unaowakutanisha marais hao
wawili baada ya mgogoro wa kidiplomasia uliozikumba nchi hizo mbili kufuatia
ndege mbili za Uturuki kuiangusha ndege ya kivita ya Urusi iliyoingia katika
anga ya Uturuki mwezi Novemba mwaka jana.
Katika mahojiano na shirika la habari la Urusi, Tas, Rais
Erdogan amesema kuwa Urusi ni miongoni mwa pande muhimu sana katika mchakato wa
amani ya Syria na kuelezea matumaini yake kuwa mwenzake wa Urusi ataona umuhimu
wa kuisaidia Uturuki baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli.
Aidha, Rais huyo wa Uturuki ameelezea utayari wake wa
kuondosha mtanziko katika uhusiano wake na Urusi kuhusu ujenzi wa vinu vya
nyuklia, na kusema kuwa anataka kurejesha uhusiano imara kati ya Ankara na
Moscow kwa kuanza ukurasa mweupe.
Amesema kuwa mkutano wake na Putin utafungua ukurasa
mpya katika uhusiano baina ya mataifa hayo katika nyanja za kisiasa, kijeshi,
kiuchumi na kiutamaduni pamoja na “mambo ambayo mihimili hiyo miwili ya kieneo
inaweza kuyafanya”.
Aidha, Erdogan amekanusha madai kwamba Urusi iliitarifu
mapema Uturuki juu ya mpango wa mtandao wa Fethullah Gulen kutaka kufanya
mapinduzi nchini mwake, akisema “Mimi ndiye mtu wa kwanza ninayepaswa kulijua
hilo, lakini sikupata taarifa yoyote kutoka vyombo vya upelelzi wala kutoka
upande wowote ule.”
Akielezea kuhusu ziara hii, mkuu wa muungano wa upinzani
nchini Syria, Anas Abdeh amesema kuwa anatarajia kwamba ziara ya Erdogan nchini
Urusi itakuwa “chanya” na itasaidia kufikisha “ujumbe wa wazi” kwa Rais Putin
kuhusu mgogoro wa Syria.
Aidha, amesema kuwa Rais wa Uturuki ni mshirika mkuu wa
taifa la Syria na ana fursa ya kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali na
kusisitiza kwamba Uturuki imewahakikishia kuwa haitabadili msimamo wake kuhusu
mgogoro wa Syria baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli.
Anas ameonesha matumaini yake kwamba Rais Erdogan
atautaka upande wa Urusi kuacha kuwalenga raia wa kawaida katika mashambulizi
yake na kujielekeza kwenye mchakato wa kisiasa ambao wananchi wa Syria ndio
watakaokuwa na uamuzi kupitia “malengo ya mapinduzi” ambayo ni kuiunganisha
Syria, kuondoka madarakani Rais Bashar Al-Assad na kujenga mfumo jumuishi wa
kisiasa, wa kiraia na wa kidemokrasia.
Ungana nasi kupitia WhatsApp: +255 712 566 595
Ungana nasi kupitia WhatsApp: +255 712 566 595
0 comments:
Post a Comment