Rais John Magufuli |
Wakati katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ataongoza
timu yake ya sekretarieti kukabidhi barua za kujiuzulu Julai 23, makada wanne-
William Lukuvi, Amos Makala, Abdallah Bulembo na Dk George Nangale wanatajwa
kurithi nafasi hiyo ya mtendaji mkuu wa chama tawala.
Kinana, anayeaminika kuwa alichangia kwa kiasi kikubwa
kurejesha nguvu za chama hicho katika kipindi cha miaka mitano alichoshika nafasi
ya katibu mkuu, analazimika kujiuzulu pamoja na timu yake ya watu saba wa
sekretarieti kuendeleza utamaduni wa CCM unaofanyika wakati wa mabadiliko ya
uongozi wa juu.
CCM itampata mwenyekiti wake mpya, ambaye ni Rais John
Magufuli Julai 23, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza utamaduni wa chama hicho wa
kumuachia kada aliyechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, kiti cha
kuongoza chama baada ya Jakaya Kikwete kumaliza kipindi chake cha urais.
Kikatiba, uchaguzi mkuu wa CCM unatakiwa kufanyika
mwakani, lakini CCM imejenga utamaduni wa kumpa uenyekiti Rais mpya ili
ajiandae vizuri kwa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kuunda timu yake kwenye chama.
“Kwa desturi ya
CCM, baada ya mwenyekiti mpya kupatikana, sekretarieti yote hujiuzulu ili kumpa
nafasi aunde timu yake mpya ya kwenda nayo,” msemaji wa CCM, Christopher Ole
Sendeka aliwaambia waandishi wa habari jana mjini Dodoma.
“Kwa hiyo, Kinana
atawasilisha barua yake ya kujiuzulu Julai 23 na sekretarieti nzima na
mwenyekiti mpya ataunda nyingine.”
Kinana amekuwa katibu mkuu tangu mwaka 2012, akiongoza
kampeni ya kuwaaminisha wananchi kuwa CCN ina sera nzuri, huku akiwashutumu
hadharani viongozi wa Serikali kuwa wanakwamisha maendeleo ya nchi. Wengi
wanaamini kuwa kampeni hiyo ilichangia kuifanya CCM iweze kukabiliana na
ongezeko la nguvu ya upinzani.
Lakini atalazimika kuachia ngazi kumpisha mwenyekiti
mpya aamue kama ataendelea naye, au ataamua kumpumzisha ili aanze na nguvu
mpya.
Iwapo ataamua kupumzisha, tayari majina mengi yameanza
kutajwa kwa kuangalia uteuzi ambao Rais amekuwa akiufanya, ukada na uzoefu.
Lukuvi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
ni miongoni mwa wanaopewa nafasi kubwa kutokana na uzoefu wake ndani ya chama,
akiwa ameanzia uongozi Umoja wa Vijana, ukuu wa mkoa hadi uwaziri.
“Lukuvi ana
nafasi kubwa kutokana na uzoefu wake mkubwa kwenye chama na Serikali,” alisema
kada wa CCM ambaye aliomba jina lake lisitajwe.
Lukuvi, ambaye aliongoza katika orodha ya viongozi
wanaojulikana kwa wananchi kwa mujibu wa utafiti wa Sauti za Wananchi
uliofanywa na Twaweza, alikuwa akitajwa kuwa mmoja wa watu waliokuwa wanapewa
nafasi ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu baada ya Magufuli kushika madaraka.
Mwingine anayetajwa kuwa anaweza kupewa nafasi hiyo ni
Makala, mkuu wa Mkoa wa Mbeya, ambaye alianzia pia UVCCM hadi kuwa mweka hazina
wa CCM na baadaye naibu waziri.
“Msimsahau
Makala, huyu ni kati ya waliokulia ndani ya chama. Anajua mengi kuhusu chama na
ameshika nafasi serikalini na bado ni kijana,” alisema kada mwingine wa CCM
ambaye pia aliomba jina lake kisitiriwe.
Makala alishindwa kwenye uteuzi wa mgombea ubunge wa
Jimbo la Mvomero ndani ya CCM na baadaye kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro kabla ya kuhamishiwa mkoani Mbeya.
Dk Nangale ni kada mwingine ambaye jina lake linatajwa
kuwa miongoni mwa watu wanaopewa nafasi hiyo nyeti kwenye chama.
Mwaka jana Nangale, ambaye ni mmiliki wa kituo cha redio
cha Sibuka FM, aliingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge wa Jimbo la Maswa
Mashariki, lakini akaangushwa na Haroun Nyongo ndani ya CCM. Pia aliingia
kwenye kinyang’anyiro cha uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, lakini
hakufanikiwa.
“Huyu ni msomi
ambaye amekuwa kwenye chama muda mrefu. Kwa kuangalia jinsi Rais anavyozingatia
elimu, Dk Nangale ana nafasi kubwa ya kuwa katibu mkuu wa chama,” alisema kada
huyo akimzungumzia mbunge huyo wa zamani wa Afrika Mashariki.
Wakati Dk Nangale akipewa nafasi kutokana na elimu yake,
Bulembo, ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM anapewa nafasi
kutokana na kuelewana na Rais na pia uzoefu wake ndani ya chama hicho.
Bulembo alikuwa karibu na Rais Magufuli wakati wote wa
kampeni za uchaguzi mkuu na amekuwa mmoja wa watu wa karibu wa kiongozi huyo wa
nchi, hali inayofanya wengi waamini kuwa anaweza kumpa nafasi hiyo nyeti kwenye
chama tawala.
Mbali na Kinana, wajumbe wengine wa sekretarieti
wanaotarajiwa kuachia ngazi ni Vuai Ali Vuai, ambaye ni naibu katibu mkuu
upande wa Zanzibar, Rajab Luhavi (naibu katibu mkuu-Bara), Mohamed Seif Khatib
(katibu wa oganaizesheni wa Halmashauri Kuu), Asha Rose Migiro (katibu wa siasa
na mahusiano ya kimataifa), Zakia Meghji (katibu wa uchumi na fedha), na Nape
Nnauye ambaye ni katibu wa itikadi na uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM.
Mara baada ya kuchaguliwa, Magufuli ataweza kufanya
mabadiliko ya watu watano ambao ni wa Bara na kupokea majina mawili kutoka kwa
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
Nafasi za upande wa Zanzibar ni ile ya naibu katibu mkuu
upande wa Zanzibar na ya katibu wa oganaizesheni.
Katika kufanikisha hilo, Dk Magufuli ama atatoa
mapendekezo ya majina mapya au kupendekeza waliopo kwa Halmashauri Kuu ya CCM
kwa ajili ya kuyapitisha.
Tayari inaelezwa kuwa katika nafasi hizo saba, Nape
ameshaomba kuachia ngazi baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo. Amekuwa katibu mwenezi wa CCM tangu mwaka 2012.
Kwa upande wa Zanzibar, tayari Vuai anaonekana kukalia
kuti kavu baada ya kudaiwa kuwa hakufanya kazi ya kutosha kuhakikisha CCM
inashinda katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana kwa maelezo kuwa
alitumia muda mwingi kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Vuai amesema kuwa maneno hayo ni ya fitina ya kundi dogo
la watu wasiozidi 15 ambalo halimtakii mema.
Nafasi nyingine ni ya Migiro ambaye sasa ameteuliwa kuwa
balozi nchini Uingereza.
Kwa sasa nafasi hiyo inakaimiwa na Dk Pindi Chana ambaye
pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
Katika hatua nyingine, CCM imesema mjini Dodoma kuwa
haitarajii kuwa na upinzani wowote dhidi ya Rais Magufuli katika uchaguzi wa
mwenyekiti wa chama hicho.
Akizungumza katika ziara ya kukagua jengo la ukumbi wa
mkutano ambalo litatumiwa Jumamosi kumpata mwenyekiti mpya wa CCM, msemaji wa
chama hicho, Christopher Ole Sendeka alisema chama ndiyo chenye jukumu la
kufanya kampeni na kwamba haoni mwanachama yoyote anayeweza kuvuruga uchaguzi
huo kwa kupiga kura za hapana au kufanya vurugu ndani ya ukumbi.
Ole Sendeka alisema suala la ulinzi katika mkutano huo
halina shaka kwa kuwa katika kila mlango kutakuwa na kamera maalumu za usalama
na baada ya kuingia ndani ya jengo kutakuwa na ukaguzi maalumu utakaohusisha mashine
maalumu, hivyo mtu yeyote asiye na kitambulisho hataruhusiwa kuingia.
“Tumepata taarifa
kuna kikundi cha watu kimeamua kuja kuvuruga mkutano na kuhakikisha wajumbe
wanapiga kura za hapana. Kikundi hicho pia kimesambaza habari katika mitandao
ya kijamii. Niwahakikishie hilo halitakuwepo na tumejipanga vilivyo. Huu ni
utamaduni wetu na ni lazima tuuheshimu,” alisema Ole Sendeka.
“Niwasisitize
wasithubutu kufanya chochote kwa kuwa tumejiandaa na vyombo vya ulinzi na usalama
vipo nyuma yetu. Vimetuhakikishia ulinzi upo kwa asilimia 100,” alisema Ole
Sendeka.
Msemaji huyo alisema baada ya kumalizika kwa mkutano
huo, kutakuwa na hafla fupi ya kumuaga Kikwete itakayofanyika kwenye viwanja
vya ukumbi huo.
Awali mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya shughuli
hiyo, Kilumbe Ng’enda alisema asilimia 99 ya marekebisho na maandalizi ya ukumbi huo yamekamilika.
“Vitu vyote
vimekamilika, usafi na ukarabati wa jengo na kuandaa kumbi zote zitakazotumika,
yamekamilika. Tunachofanya sasa ni hatua za mwisho za mapambo tayari kwa
mkutano,”alisema Ng’enda ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM.
CHANZO: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment