
Mwigizaji nyota wa filamu nchini Nigeria, Emeka Ike
ameiambia mahakama moja ya mwanzo mjini Lagos kuwa amepeleka ombi mbele ya
Mahakama Kuu kuizuia mahakama ya mwanzo isisikilize kesi ya talaka
iliyowasilishwa na mkewe waliyefarakana, Emma Ike.
Emma ambaye amekuwa kwenye ndoa na nyota huyo wa
Nollywood kwa miaka 16, aliwasilisha ombi la talaka mahakamani mwaka 2015,
akidai kuwa mumewe huyo alikuwa akimpiga bila sababu.
Hata hivyo, Ike anakanusha madai hayo na kuiomba
mahakama ya Lagos isimtenganishe na Emma.
“Bado ninampenda”, alisema mbele ya mahakama hiyo siku
ya Jumanne Julai 12.
Wakili wa Emeka, Abdul Labi-Lawal, aliieleza mahakama
hiyo kuwa mteja wake alikuwa amewasilisha mbele ya Mahakama Kuu ombi la
kusitisha usikilizaji wa kesi hiyo.
Ombi la Emeka kwenye Mahakama Kuu lililenga kuitaka
mahakama hiyo kutamka kuwa mahakama ya mwanzo ya Lagos haina uwezo na uhalali
wa kisheria wa kuamua madai hayo ya talaka.
Ombi hilo linasema kuwa ndoa hiyo ilifungwa katika Jimbo
la Enugu kwa taratibu za kimila na tamaduni za kabila la Igbo.
Aidha, Emeka aliitaka Mahakama Kuu kutangaza kuwa vikao
vyote vilivyofanywa na mahakama ya mwanzo kuhusu ndoa hiyo kuwa ni batili.
Akipinga suala hilo, mwanasheria wa Emma, Iheanyi Awa
aliitaka mahakama kutozingatia ombi hilo na badala yake itoe hukumu.
Awa, ambaye alisema kuwa ombi la Emeka lililenga kuzuia
hukumu ya mahakama hiyo, aliitarifu mahakama hiyo kwamba si mteja wake wala yeye
mwenyewe waliopokea ombi la upande wa mshitakiwa.
WhatsApp: +255 712 566 595
0 comments:
Post a Comment