
Mkongwe wa masumbwi duniani Muhammad Ali amefariki
dunia akiwa na umri wa miaka 74, msemaji wa familia amethibitisha.
Bingwa huyo aliyewahi kutwaa taji la uzito wa juu mara tatu
alikuwa amelazwa katika hospitali huko Phoenix katika jimbo la Arizona nchini
Marekani tangu siku ya Alhamisi  kwa
tatizo la kushindwa kupumua.
Pia Ali alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya Parkinson
tangu mwaka 1984. Mshindi huyo wa medali ya dhahabu katika mashindano ya Olympic
alikuwa na tatizo la upumuaji ambalo linahusishwa na ugonjwa huo wa Parkinson.
“Baada ya miaka 32 ya kupambana na ugonjwa wa Parkinson, Muhammad
Ali ametutoka akiwa na umri wa miaka 74, msemaji wa familia Bob Gunnell amesema
katika taarifa yake.
“Familia ya Ali ingependa kuwashukuru wote kwa mawazo, dua na
uungaji mkono wenu na inaomba faragha kwa wakati huu”.
Mazishi ya Ali yatafanyika katika mji wake wa Louisville,
Kentucky. 
Mapema kabla ya mauti yake, Gunnell alikuwa amesema kuwa Ali
alikuwa katika hali ya kawaida katika hospitali ambayo haikuwa imewekwa wazi
katika mji wa Phoenix.
Muhammad Ali alizaliwa katika mji wa Louisville mwezi Januari
mwaka 1942 na jina lake la awali ni Cassius. Alianza masumbwi akiwa na umri wa
miaka 12 na kushinda taji la uzito wa juu mwaka 1964. Mwaka huohuo alibadili
dini kuwa Muislamu akabadili jina lake na kuwa Muhammad Ali.
Kabla ya kustaafu masumbwi mwaka 1981 alishinda mataji mengine
mawili ya uzito wa juu.
Muhammad Ali anachukuliwa kama mmoja wa wanamichezo wakubwa
kabisa wa karne ya 20 na mwanamasumbwi wa uzito wa juu wa wakati wote. Anajulikana
kwa mtindo wa upiganaji wake usiokuwa wa kawaida ambao ulijumuisha kasi ya
ajabu, wepesi, nguvu na radiamali endelevu dhidi ya wapinzani wake.
(Mzizima WhatsApp: +255 712 566 595)
(Mzizima WhatsApp: +255 712 566 595)
0 comments:
Post a Comment