Baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vinatoa taarifa
potofu kuhusu mchakato wa Mwenyekiti wa sasa wa CCM Dkt. Jakaya Kikwete
kukabidhi kijiti cha uongozi wa CCM kwa Rais John Pombe Magufuli kama ilivyo
mila na desturi ya Chama Cha Mapinduzi.
Yamekuwepo madai eti Mwenyekiti amekataa au
anachelewesha kukabidhi kijiti.
Habari hiyo sio kweli kabisa na ni kinyume chake, kwani
Dkt. Kikwete amekuwa akisisitiza kukabidhi madaraka mapema iwezekanavyo. Kwa
ajili hiyo kwenye kikao cha Mei 3, 2016 alikataa kusiongezwe agenda nyingine
ambazo zitalazimisha Mkutano Mkuu Maalum kuchelewa kufanyika kwa sababu ya
kukamilisha maandalizi ya agenda hizo. Alisisitiza agenda iwe moja tu.
Dhamira ya kufanyika Mkutano Mkuu maalum mwezi Juni,
2016 iko pale pale. Kilichoelezwa kwenye kikao ni kutaka kukamilisha utaratibu
wa kupata fedha za kugharamia mkutano huo. Taratibu zikikamilika tarehe
itapangwa. Mipango ya kutafuta pesa inaendelea na ikikamilika tarehe
itatangazwa.
Tunawataka wana-CCM wasihamanike wala kubabaishwa na
taarifa za upotoshaji zinazofanywa na watu wenye nia mbaya na CCM. Hawa ni wale
wale ambao wamekuwa wakiiombea mabaya CCM bila ya mafanikio.
Pia tunapenda kukanusha madai ati kuwa Mwenyekiti
Kikwete aliwatahadharisha Wajumbe wa Kamati Kuu kuhusu ukimya wa Ndugu Edward
Lowassa. Hakuna wakati wowote kauli kama hiyo aliitoa. Ni uzushi mtupu. Jina la
Ndugu Lowassa halikutajwa kabisa.
Aidha, tunapenda kukanusha madai ya kufanyika mkutano
baina ya Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Jamhuri ya Muungano, Makamu wa Rais na
Katibu Mkuu wa CCM kuhusu uchaguzi wa Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM.
Hapajawahi kufanyika mkutano wa aina hiyo siku yoyote na mahali popote. Hivyo
madai ya kuwepo kwa tofauti baina ya Viongozi wakuu kuhusu nani achaguliwe kuwa
Katibu wa Wabunge wa CCM hayana msingi wowote.
Kamati Kuu iliteua Wabunge wanne kugombea na kuwaachia
Wabunge wa CCM kuamua. Kuhusisha Viongozi na hasa kuzua kuwepo kutokuelewana ni
jambo la kusikitisha. Ni taarifa ya
uongo yenye nia ovu kwa CCM na Viongozi wake.
Tunapenda kuwatahadharisha waandishi wa habari kuandika
habari za ukweli. Waache kuzua mambo yenye kupandikiza chuki na mgawanyiko
usiostahili kuwepo ndani ya CCM na kuyaeneza kwa watu. Waheshimu maadili ya
kazi zao.
Napenda kuwahakikishia na kusisitiza kuwa hakuna mgogoro
wa kukabidhi kijiti cha uenyekiti katika CCM na wala hautakuwepo.
Imetolewa na;
Ndugu Christopher Ole Sendeka
MSEMAJI WA CCM
MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
05/05/2016
0 comments:
Post a Comment