Na Pendo Fundisha, Mbeya
WACHEZAJI wa klabu ya Mbeya City, wamegoma kufanya
mazoezi kwa siku kadhaa na kuendelea kubaki kambini wakiushinikiza uongozi wa
klabu hiyo kuwalipa mishahara yao.
Imeelezwa kwamba wachezaji hao wamekuwa wakiidai
Halmashauri ya Jiji la Mbeya mishahara ya miezi mitatu jambo linalotajwa kuwa
chanzo cha wachezaji kukosa morali ya kucheza vizuri uwanjani.
Wakizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutoandikwa
majina yao, baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo walisema kuwa klabu hiyo kwa sasa
inakabiliwa na ukata wa fedha kwani mbali na mishahara yao pia upande wa
chakula na malazi nako ni tatizo.
“Sio siri klabu yetu inakabiliwa na ukata, hali ni mbaya
kwani licha ya kula chakula kisichokizuri pia mishahara yetu ni tatizo, hadi
sasa huwezi amini uongozi haujatulipa mishahara kwa zaidi ya miezi mitatu,”
kilisema chanzo cha habari hizi.
Chanzo hicho kilieleza kuwa ukosefu wa mishahara ni moja
ya changamoto zinazoigharimu timu hiyo kufanya vibaya, kwani wachezaji wamekuwa
wakifanya mgomo baridi kwa kutocheza vizuri uwanjani ikiwa na kugoma kwenda
kufanya mazoezi kwa zaidi ya siku tano.
“Viongozi wakifika kuzungumza na wachezaji wamekuwa
wakiwafariji tu kwa macho ila moyoni wachezaji wamejiwekea misimamo yao
wenyewe, hivyo ni vema mwajiri wetu akalifahamu hili na kulifanyia utatuzi,”
alisema.
Akizungumzia hilo, Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, David
Mwashilindi, alikiri kwamba klabu hiyo inakabiliwa na ukata wa fedha na tayari
wamezungumza na wachezaji ili kuona ni jinsi gani mishahara hiyo watalipwa.
“Kweli wachezaji wanadai mishahara yao lakini juzi
tumezungumza nao na kuna kiasi cha fedha wameingiziwa, uongozi unaendelea na
mchakato wa kutafuta fedha zitakazoweza kulimaliza tatizo hilo,” alisema.
Aidha, Meya huyo aliwaomba wachezaji hao kuendelea na
mazoezi ya kujiandaa na mechi ngumu za mbeleni kwani timu hiyo kwa sasa ina
wakati mgumu wa kuhakikisha inasimama katika msimamo wa ligi kuu.
“Timu kwa sasa ipo sehemu mbaya nilichowaomba wachezaji
tushikamane na kufanya vizuri ili tujinasue katika kushuka daraja na uongozi
ujipange kwa msimu ujao wa ligi kuu,” alisema.
CHANZO: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment