· 

Baada ya kimya cha muda
mrefu, Mchungaji mstaafu, Ambilikile Masapila (82) maarufu kama ‘Babu wa
Loliondo’, ameibuka upya na kuwataka Watanzania wajiandae kwa ‘mafuriko’ ya
watu watakaomiminika nyumbani kwake kutoka katika mataifa mbalimbali duniani,
kufuata huduma itokanayo na muujiza mkubwa zaidi kulinganisha na ule wa tiba ya
kikombe uliomtokea mwaka 2009.
Akizungumza juzi katika
mahojiano maalum na Nipashe nyumbani kwake Samunge, Loliondo, Wilaya ya
Ngorongoro mkoani Arusha, Masapila alisema kwa mara nyingine, Watanzania
wajiandae kupokea habari njema kuhusiana na muujiza mkubwa wenye kuleta
suluhisho la matatizo mengi ya binadamu, na hivyo kulitangaza jina la nchi yao
(Tanzania) kote ulimwenguni.
'Babu' alisema ujiuo wa
‘mafuriko’ hayo ya watu utaanza hivi karibuni na ameshaanza maandalizi kabambe
ya kupokea ugeni huo utakaokuwa wa kihistoria.
Hata hivyo, Babu
Masapila hakutaja ni lini hasa ataanza kutoa huduma hiyo itokanayo na muujiza
mpya, bali alisisitiza kuwa “ni hivi karibuni”, hasa atakapokuwa amekamilisha
maandalizi ya mahala pa kupokea wageni.
“Nilipata maono ya jambo
hili mwishoni mwa mwaka uliopita (2015). Ni ndoto inayohusiana na habari njema
kwa binadamu, ni ndoto iliyonilazimu kuanza maandalizi ya kupokea watu wengi
zaidi na ndiyo maana nimeanza maandalizi,” alisema Babu Masapila, anayesisitiza
kuwa yeye hupata nafasi ya kuzungumza na Mungu (wake) mara kwa mara kupitia
ndoto.
Anasema kila
anachokifanya hutokana na maagizo anayoyapata kupitia sauti kutoka kwa Mungu.
Hadi kufikia mwaka 2011,
Babu Masapila alikuwa gumzo nchini na nje ya mipaka kutokana na huduma yake ya
tiba ya kikombe iliyovutia maelfu ya watu.
Dawa hiyo aliyodai
inatibu maradhi mengi yakiwamo ya kisukari, aliitoa kupitia kikombe na kuiuza
kwa Sh. 500 tu.
Iliwateka watu wa kila
namna wakiwamo wanasiasa, viongozi wa kidini, wasanii maarufu, wafanyabiashara
na wakuu wa vikosi mbalimbali vya majeshi.
Inakumbukwa kuwa
miongoni mwa vigogo waliowahi kufika kwa Babu na kupata ‘kikombe’ ni pamoja na
aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Rais John Magufuli,
ambaye baada ya kunywa dawa aliwaambia watu waliojazana eneo hilo kwa maelfu
kuwa serikali itatumia Sh. bilioni 1.05 kutengeneza barabara inayoingia
kijijini hapo ili kurahisishia usafiri kwa watu wanaokwenda kwa Babu Masapila.
Wengine waliowahi kufika
ni pamoja na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi,
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro na Askofu Thomas Laizer ambaye sasa ni
marehemu.
Ingawa watu
waliomiminika kwake mwaka 2011 kwa ajili ya kupata tiba ya ‘kikombe’
walitengeneza msururu mrefu wa magari uliofikia kilometa 15, Babu Masapila
alisema watu watakaokwenda kwake sasa kutokana na muujiza mpya watakuwa wengi
maradufu na ndiyo maana ameanza kujenga nyumba za kutosha ndani ya eneo lenye
ukubwa wa eka 70 ili kuwapokea.
“Kupitia ndoto hiyo
niliagizwa kutafuta eneo kubwa na kujenga nyumba za kutosha kwa ajili ya
kupokea wageni kabla ya kuanza kutoa huduma," alisema Babu Mwasapila
katika mahojiano.
"Nashukuru uongozi
wa kijiji (cha Samunge) umenielewa na kuniunga mkono kwa kunipatia eneo
nililoelekezwa kwa kazi hiyo (kupitia ndoto).”
Akieleza zaidi, Babu Masapila
alisema sauti kupitia ndoto yake ilimuelekeza kujenga nyumba za kupokea wageni
katika eneo la jirani na Mlima wa Makao na hivyo, anaushukuru uongozi wa
serikali ya kijiji kwa kumpatia eka 70 hizo kandoni mwa mlima huo na tayari
ameanza ujenzi wa nyumba hizo.
“Namshukuru sana Mungu.
Ana mpango maalumu na Tanzania kupitia Samunge. Naona Tanzania inakwenda kuwa
maarufu barani Afrika kupitia Samunge.
"Kutafanyika
miujiza mingi na dunia nzima itaijua Tanzania, tena kuliko ule muujiza wa
kikombe.“
Babu Mwasapila ni
mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
Akieleza zaidi
maandalizi hayo ya kupokea ugeni mkubwa zaidi, Babu Masapila alisema tayari
kuna nyumba sita ameshazijenga na ziko katika hatua ya mwisho ya kukamilika.
Alisema kazi hizo
zinarahisishwa na malori mawili aina ya Fuso aliyoyanunua kitambo kwa shughuli
za kubeba mchanga na vifaa vya ujenzi, na pia kubebea kuni za kuchemshia dawa
zake.
Aidha, gari lake la
kutembelea aina ya Toyota Land Cruiser hutumika pia kwa shughuli za kubebea
dawa mbalimbali za uponyaji.
Babu Masapila anasema
hivi sasa amewaajiri watu 13 ambao huwalipa mishahara kuanzia Sh.100,000 kwa
mwezi ili kusaidia maandalizi hayo.
Masapila alisema tangu
alipopata maono kuhusu maandalizi ya kupokea ugeni wa watu wengi zaidi, kila
anapolala huona makundi ya watu waliosongamana pembeni mwa Mlima Makao na ndiyo
chanzo cha kuliomba eneo hilo.
Diwani wa Kata ya
Samunge, Kajulus Steven, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Wilaya ya Ngorongoro, anakiri kijiji kumpatia Babu Masapila eneo la eka 70,
kandoni mwa Mlima Makao ili afanye maandalizi kwa ajili ya kuwapokea wageni.
Alisema walimpa eneo
hilo baada ya Babu Masapila kuwaeleza kuwa kuna muujiza mwingine hivi karibuni.
“Tulishajifunza kutokana
na kile kilichotokea mwaka ule… alituambia anaona watu wakifurika Samunge
lakini sisi hatukujali, tukapuuza maono yake.
Mwishowe watu wakafurika
kweli, tukahangaika sana,” alisema Steven na kuongeza:
“Kwa sababu hiyo, safari
hii tumemsikiliza na kumpatia eneo alilodai kuoteshwa kuwa ndilo linalofaa kwa
huduma.
"Viongozi wa eneo
hili tulikaa na kuingia naye makubaliano kuwa akimaliza kutoa huduma zake hizo
tutalirejesha.”
Steven alisema
wanamchukulia Babu Masapila kama ‘nabii’ kwa sababu mambo mengi aliyowahi
kutabiri kuwa yatatokea, yametokea kweli, ikiwamo kupata umeme ambao hivi sasa
umewafikia kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA), na kufikishwa kwa huduma za
simu za mkononi baada ya kufungwa kwa minara ya kampuni mbili.
HIVI SASA HALI IKOJE?
Akizungumzia hali ya
utoaji huduma za uponyaji hivi sasa kulinganisha na vile ilivyokuwa wakati wa
‘mafuriko’ yaliyotokana na tiba ya kikombe, Babu Masapila alisema ipo tofauti
kubwa.
Alisema wakati huo, watu
aliokuwa akiwapatia kikombe walikuwa wakifika hadi 18,000 kwa siku lakini hivi
sasa idadi hiyo imepungua hadi kuwa chini ya watu 20 kwa siku.
“Hivi sasa nawahudumia
(watu) 10 hadi 20 na kwa sababu kila mmoja hulipia Sh. 500, mwanzoni fedha
zilizopatikana zilifikia hadi Sh. milioni tisa kwa siku… lakini hivi sasa kiasi
kinachopatikana ni kati ya Sh. 5,000 na 10,000,” alisema.
Akieleza sababu za
kupungua huko kwa wateja, Babu Masapila alisema hashangazwei kwa sababu
anaamini kuwa huo ni mpango maalum wa Mungu.
“Sishangazwi. Mungu
mwenyewe amependa kusitisha umaarufu wa huduma hii (tiba ya kikombe) ili nipate
muda wa kufanya maandalizi kwa ajili ya kuwapokea watu wengi zaidi watakaofika
hapa (Samunge) kuliko wale wa awali,” alisema Babu Masapila.
FAMILIA, HISTORIA
Babu Masapila aliiambia
Nipashe kuwa yeye ni baba wa watoto wanne, kati yao watatu ni wa kiume na
kwamba, hivi sasa familia yake bado iko Babati mkoani Manyara.
Alisema kabla ya kufika
Samunge, alikuwa wilayani Rungwe, mkoani Mbeya. Mwaka 1952 aliondoka (Mbeya) na
kwenda Korogwe mkoani Tanga kabla ya kuhamia Babati na kisha kutua Samunge
alikokuwa akifanya kazi ya uchungaji wa KKKT.
Alisema baada ya Mungu
kumpa nguvu ya uponyaji kupitia kikombe, sasa bado anaendelea kutoa huduma hiyo
kwa watu mbalimbali, wengi wanaoendelea kufika kwake wakitokea Dodoma na nchi
za Kenya, Uganda, Sudan Kusini na Eritrea.
HALI KIMAISHA
Baada ya kufika nyumbani
kwa Babu Masapila na kuonyeshwa mahala anapoishi sasa na pale alipokuwa akiishia
awali kabla ya mwaka 2011, mwandishi alibaini kuwa Babu Mwasapila ameimarika
zaidi kiuchumi.
Hali hiyo inatokana na
ukweli kuwa awali alikuwa akiishi katika nyumba ndogo ya udongo lakini sasa
anaishi kwenye nyumba kubwa na ya kisasa huku pia akitembelea Land Cruiser na
kumiliki malori mawili aina ya Fuso, achilia mbali muonekano wake unaoshiria
kuwa ni mtu mwenye afya tele.
Aidha, Babu ana mradi
wake wa ujenzi wa nyumba sita za kisasa na miundombinu mingine kwa maandalizi
ya kupokea maelfu ya wageni kwenye eneo la eka 70.
Mbali na malori yake
kumsaidia katika shughuli za maandalizi ya ujenzi wa nyumba za kupokea wageni,
pia vyombo hivyo huvikodisha kwa shughuli za ujenzi na hivyo kumuongezea kipato
kinachotumika kuboresha huduma zake.
UJIO WA VIONGOZI,
WANASIASA
Kuhusiana na namna
alivyojisikia baada ya kupata ugeni wa viongozi mbalimbali mashuhuri na watu
kutoka nje ya nchi kufuata tiba yake ya kikombe, Babu Masapila alisema hayuko
tayari kuzungumzia hilo kwani siyo vizuri kujadili majina ya wale waliowahi
kupata huduma yake.
Hata hivyo, alisema
anafurahi kuona kuwa wapo wakubwa wengi wanakubali tiba ya kikombe chake na
kuiamini kwani ndiyo msingi wa kupona kwa kila anayepata huduma hiyo.
MTI WA DAWA
Akiuzungumzia mti wa
dawa ya kikombe, Babu Masapila alisema siyo mpya na wengi wanaufahamu kwa
majina taofauti.
“Mti wa dawa ninaotoa
unajulikana kwa majina tofauti kulingana na makabila husika. Wairaqw wanauita
Titiwi, Wakurya wanaita Mkarakara na Wamasai wanauita Ngamriaki," alisema.
"Siyo kwamba mimi
nimeubuni na sikujua kama unatibu, hapana. Mungu aliweka neno na akanionyesha
mimi… mtu akinywa kikombe kimoja tu anapaswa kupona.”
Hata hivyo, aliongeza
kuwa kama mtu hajapona vizuri, hazuiwi kurudia kunywa kikombe, lakini kwa
sharti kwamba siyo kwa siku hiyo bali siku nyingine, hasa baada ya kupita siku
saba zinazopaswa kuwa za uponyaji.
Alisema mhusika anapaswa
kwenda kupimwa kama maradhi yanayomsumbua yameisha ama la ndani ya kipindi cha
miezi mitatu hadi minne.
Alisema wapo baadhi ya
watu humpuuza na kumdharau, lakini hilo halimsumbui ila anawasamehe na
kumuachia Mungu kwani anajua kuwa wengi wa wanaombeza ni waganga wa jadi
wanaohofia kupoteza wateja, na wakuu wa makanisa ya baadhi ya madhehebu ambao
huhofia kupoteza waumini wao wenye nia ya kuombewa ili wapate nafuu ya matatizo
mbalimbali ya kiafya.
TUHUMA ZA KUSABABISHA
VIFO
Babu Masapila alisema
anatambua kuwa baadhi ya watu wanaompinga huvumisha kuwa dawa ya ‘kikombe’
chake ilisababisha vifo.
Akielezea kuhusu hilo,
alisema hakuna ukweli bali wapo baadhi ya wagonjwa walifariki baada ya ndugu
zao kuwatorosha kutoka katika hospitali mbalimbali walikokuwa wamelazwa, na
kuzidiwa wakati wakiwa kwenye foleni ya kupata kikombe cha dawa.
“Wengi kati ya wale
waliobahatika kupata kikombe walipata nafuu na afya zao kuimarika,” alisema.
Hata hivyo,
haitashangaza kusikia kuwa wapo pia watu waliokunywa dawa ya kikombe chake na
bado wakafariki dunia, alisema Babu Masapila, kwani yeye hana dawa ya kuzuia
kifo.
Alisema hata kwenye
hospitali zote duniani wapo watu hupona na wengine hufariki kwa sababu Mungu
ndiye huamua hatma ya maisha ya kila binadamu.
Alisema wakati watu
walipokuwa wakifurika kwake kufuata tiba ya ‘kikombe’, kuna wataalamu
waliojitambulisha kuwa wanatoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali walifika na
kuchukua sampuli ya dawa na kwenda kuifanyia utafiti na hakukuwa na majibu
yaliyodai dawa hiyo ina madhara.
Babu Mwasapila alisema
kuwa wataalamu hao walifika tena na kuchukua mizizi ya mti anaoutumia kwa
maelezo kuwa wanakwenda kuchunguza ili kujua ni baada ya muda gani dawa hiyo
huua virusi na vimelea vingine vya magonjwa mbalimbali baada ya mtu kuinywa.
“Cha kushangaza, watu
hao hawajarudi tena kwangu… kwa hiyo sijui kinachoendelea.”
Kwa mujibu wa Afisa
Mtendaji wa Kata ya Samunge, Simon Dudui, watu 52 walifariki dunia wakati
wakiwa kwenye foleni ndefu kusubiri huduma ya ‘kikombe cha babu’ mwaka 2011.
MATUNDA YA ‘KIKOMBE‘
SAMUNGE
Diwani Steven wa Kata ya
Samunge, alisema huduma ya kikombe cha Babu Masapila ilileta maendeleo makubwa
na ya ghafla kwao, hasa kuhusiana na barabara, upatikanaji wa maji safi na pia
kuinuka kiuchumi kwa baadhi ya wakazi wake.
Alisema kabla ya kikombe
cha babu, Samunge hakukuwa na mahala pa kulala wageni na yeyote anayehitaji
huduma hiyo alilazimika kwenda Loliondo ambako ni mbali, lakini sasa hali ni
tofauti kwani tatizo hilo halipo tena.
Mwenyekiti wa Kitongoji
cha Samunge, Jonath Kilobei, alisema ‘kikombe cha babu’ hawatakisahau kwani
kimewainua kimaisha kutokana na biashara walizokuwa wakifanya wakati watu
walipofurika na kwamba sasa, wanasubiri kwa hamu ujio wa mkubwa zaidi wa wageni
kama Babu Masapila alivyowaahidi.
Afisa Mtendaji Dudui,
alisema mbali na maandalizi binafsi ya Babu Masapila, wao pia wameanza
maandalizi ya kupokea maelfu ya watu kwa kuimarisha huduma za zahanati yao ya
Samunge kwa kuipanua na pia kuongeza madaktari wawili.
“Pia kijiji kimetenga
eneo la ujenzi wa vyoo na stendi kwa ajili ya kuingiza magari mengi kwa wakati
mmoja,” alisema.
Aidha, aliongeza kuwa
tayari kijiji cha Samunge kimeanzisha vikundi vya ulinzi na usalama na pia
kununua matanki kadhaa ya maji yenye ujazo wa lita 1,000 kila moja ili
yasambazwe kwenye maeneo yaliyo karibu na eneo la Babu.
“Hatutaki tena aibu ya
wakati ule wa ujiuo wa watu wengi. Tulikuwa tunafanya kazi kwa zimamoto baada
ya kupuuza maelezo ya Babu. Hivi sasa tupo naye karibu na tumejipanga mapema
kupokea watu wengi zaidi,” alisema Afisa Mtendaji huyo.
Mmoja wa wafanyabiashara
wa Kijiji cha Samunge, Aden Sinodia Gibaseya, alisema yeye ni miongoni mwa watu
walionufaika kibiashara wakati wa muujiza wa ‘kikombe cha babu’ kwa kuuza maji
na vyakula.
Mfanyabiashara mwingine
aitwaye Sam Alen Ndugai, alisema naye ni miongoni mwa watu walionufaika sana
kwa kuuza vyakula na maji na alikuwa akiingiza hadi Sh. milioni 28 kwa siku.
Hata hivyo, anasema
alipata pigo kubwa baadaye wakati shehena ya maji aliyokuwa akiyauza Sh. 4,000
kubaki mikononi mwake kufuatia umati uliokuwa ukifika Samunge kila uchao
kupotea ghafla.
“Babu alisisitiza kwamba
tusiuze bidhaa zetu kwa bei kubwa. Wengi hatukumsikiliza… tukawa tukiuza chupa
moja ya maji kwa Sh. 4,000," alisema Ndugai. "Nilipata fedha nyingi,
lakini nyingi zikapotea pia baada ya kununua bidhaa kibao na kubaki nazo ndani wakati
kasi ya watu kufuata kikombe ikikatika ghafla.
"Safari hii kama
wageni wakija tena kwa wingi nitakuwa makini na kuzingatia ushauri wa Babu.”
Kina mama
waliojitambulisha kwa majina ya Esuvati Loishiye na Anna Laizer, walisema Babu
amesaidia kubadilisha hali ya Samunge kupitia tiba ya kikombe kwa sababu tangu
wakati huo, hivi sasa wameamka na kuchangamkia biashara ya kupika na kuuza
chakula.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment