Watu wasiojulikana wakiwa na silaha wamevamia studio za
kituo cha redio Hits FM kilichopo
Migombani mjini Unguja na kufanikiwa
kukichoma moto kwa kutumia mafuta yanayosadikiwa kuwa ni petroli.
Akizungumza na gazeti hili msemaji wa kituo hicho Juma
Ayoub Amohamed, alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 7:30, usiku wa
kuamkia jana ambapo zaidi ya watu 15 waliweza kuvamia studio hiyo na kufanikiwa
kuchoma moto.
Alisema kuwa hadi sasa bado hawajajua nini chanzo cha
kufanyiwa hivyo huku wakisema kuwa hakuna siku hata moja waliyopewa onyo na
mtu, kundi au taasisi yeyote juu ya uendeshaji vipindi vyao.
“kiukweli hadi sasa tunashangaa hili kundi lilitokea
wapi na nini chanzo chake ila kazi kubwa tumewachia Jeshi la Polisi ambao
wanaendelea na uchunguzi wao wa kisheria”alisema Juma.
Hata hivyo alisema kuwa makadirio ya awali juu ya tukio
hilo ni zaidi ya shilingi milioni 40, ambapo hesabu rasm itajulikana baada ya
kufanyika kwa uhakiki.
Akisimulia mkasa wa tukio hilo Ali Abdallah mfanyakazi
wa zamu ambaye alikuwamo kituoni hapo wakati wa tukio hilo alisema kuwa alikuwa
anaendelea na uendeshaji wa vipindi mara akasikia sauti za watu wakiwa ndani ya
studio hiyo.
Alisema kuwa watu hao wambao walikuwa zaidi ya 15 wakiwa
wamejifunika uso na kumuamuru anyanyuke na kutoka nje ili wafanye
wanachokitaka.
Alisema kuwa mara bada ya taarifa yao hiyo mfanyakazi huyo
alisita kidogo, na mmoja wao akamsogelea na kuanza kumpiga kwa mabapa ya panga
na kumyanyua na kumfunga kitambaa cha uso na kumtoa nje kijeshi.
“Waliponambia nitoke nje nilisita kidogo nao
walinichukua kwa kamandi na kunipiga mabapa ya mapanga mwilini na kunifunga
kitamba cha uso na kunitoa nje huku wakisema tunataka kufanya jambo humu ndani”
alisema Abdallah.
Hata hivyo alisema kuwa kutolewa kwake nje hakukuwa dawa
kwa studio hiyo kwani mara baada ya muda mfupi walishuhudia moshi mkubwa
ukiteketeza vifaa vyao vya studio.
Alisema kuwa huku moto huo ukiteketeza vifaa hivyo kundi
hilo la watu liliweza kutoka nje na kuanza kuondoka, huku yeye na walinzi wa
zamu wa studio wakiwa wamewekewa ulinzi na baadhi ya vijana wa kundi hilo .
“Walipoondoka tu mimi na askari wetu tulijitahidi sana
kutafuta watu wakutusaidi tulienda hadi katika nyumba hadi katika nyumba ya
Rais mstaafu Aboud Jumbe tukawaelezea wale akari waliokuwapo pale jinsi ya
tukio letu nao walipiga simu kituoni kwao bada ya muda mfupi kikosi cha akari
kikaja ila hawakufanikiwa kukuta hao wachomaji walikuwa wameshaondoka na gari
lao”alisema Ali
Ismail Mwinyi ambaye ni mwandishi wa habari kituo hapo
alisema kuwa kwa upande wake alipopata habari hio aliweza kufika kituo kwao hapo
na kushuhudia jinsi ya studio hio inavyoteketea kwa moto.
Alisema kuwa tukio kwa ukweli limewasikitisha sana
kutokana na hasa kosa lao kubwa la kufanyiwa hivyo hadi sasa bado hawalitambui
huku akisisitiza kuwa kituo chao kinaendesha vipindi kwa kufuata taratibu za
kisheria.
Hili ni tukio la pili katika kipindi cha mwaka mmoja
ambapo miezi michache iliyopita watu kama hao waliokuwa na silaha walivamia
kituo cha Coconut Fm na kuwatisha watangazaji.
CHANZO: Zanzibar Yetu
0 comments:
Post a Comment