SERIKALI ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John
Magufuli, imeshusha rungu jipya kwa kutangaza uamuzi mchungu wa kupunguza
wafanyakazi katika taasisi na mashirika ya umma ambayo yameonekana kuwa mzigo
katika utendaji.
Mashirika hayo yameelezwa licha ya kuwa na watumishi
wengi, lakini bado uzalishaji na utendaji wake umekuwa hauna tija kwa taifa.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Msajili
wa Hazina, Laurence Mafuru, katika kikao na wenyeviti wa bodi na
wakurugenzi wa taasisi na mashirika ya umma.
Kikao hicho kilikuwa na lengo la kukumbushana wajibu na
kuhakikisha watendaji hawafanyi kazi kwa mazoea na badala yake kutakiwa
waendane na mabadiliko ya kiuchumi.
Mfuru aliyataja baadhi ya mashirika hayo mzigo
yanayotakiwa kupunguza watumishi wake kuwa ni Shirika la Reli Tanzania (TRL),
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Shirika
la Nyumba la Taifa (NHC), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),
Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa).
Mafuru alisema hayo ni maelekezo ya Rais Magufuli kwa
watumishi hao juu ya utendaji anaoutaka katika Serikali ya awamu ya tano.
“Serikali inatarajia kupunguza wafanyakazi kwani kiwango
cha utendaji kimeshuka na tusipofanya hivyo jamii inatuona. Kwani mfano kwa
sasa Shirika la Reli (TRL), Tanesco, TTCL, NHC, TPA, TPDC wote hawa wanapanga
foleni hazina kutaka mishahara kwani wameshindwa kujiendesha,” alisema Mafuru.
Alisema Serikali inalipa madeni ya taasisi ambazo
zimeshindwa kujiendesha yakiwamo ya pensheni za wastaafu, huku lengo la
kuanzishwa kwake ni kuhakikisha kwamba yanaiingizia Serikali mapato na kukuza
uchumi wa nchi.
“Taasisi zote zinazopokea mtaji kwa Serikali zinatakiwa
kujieleza kwanini zinashindwa kupata faida kwa kuingiza mambo ambayo hayana
msingi,” alisema Mafuru na kutolea mfano vyuo binafsi vinavyojiendesha kwa
kutegemea michango ya shule na machapisho, huku vyuo vya Serikali vikitegemea fedha kutoka hazina.
“Ningewasifu sana kama wangeomba fedha kwa ajili ya
ujenzi wa majengo, lakini fedha zinazoombwa ni karatasi na machapisho wakati
hivi wangenunua wenyewe kwa lengo la kukuza uchumi wetu,” alisema.
Akizungumzia kuhusu nafasi za uteuzi wa rais, alisema
watumishi wengine wanapoteuliwa huchukulia kama wamepewa zawadi wakati
wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo.
“Nafasi za uteuzi wa rais si zawadi bali ni kazi, hivyo
mtu anatakiwa kufanya kazi kwa weledi, na kama anaona hatoweza kazi hiyo, ni
bora aikatae ili apewe mwingine anayeweza kufanya kazi,” alisema.
Akizungumzia kuhusu majukumu ya mawaziri, alisema ni
lazima watambue mipaka katika sehemu zao za kazi ili kuepuka kuingiliana
masuala ya utawala kwani kinachoangusha mashirika ya umma ni watu kutofuata
utawala bora.
Alisema taasisi za Serikali zinatakiwa kufanya kazi kwa
pamoja kwa kuhakikisha zinavunja kuta za kisheria na kiutendaji na
kushughulikia kero za wananchi ikiwamo maji, elimu, afya na umeme.
“Ni vyema taasisi zipunguze matumizi hata ya wanasheria
kwani zipo taasisi wanasema mwanasheria wao analipwa shilingi milioni tano hadi
20, sasa ina maana mwingine ana kesi nyingi zaidi au inakuwaje?” alisema na
kuhoji Mafuru.
Alisema miradi yote yenye uwezo wa kujiendesha haitakiwi
kujazana hazina badala yake watumie vyanzo vya mapato walivyo navyo.
Mafuru alisema Serikali itachukua hatua za kuhakikisha
kwamba inafufua mashirika hayo ambayo ni mizigo ili kuweza kujiinua na kufikia
kiwango stahiki kwani yakisimama vizuri yatasaidia katika kukuza uchumi wa nchi
kwa kiwango kikubwa.
“Serikali tunapitia madeni yetu tunayodaiwa na mashirika
ya umma na tutayalipa, na lazima muhakikishe matumizi yanabanwa kwenye
uendeshaji wa mashirika na kufanya manunuzi yenye tija,” alisema.
Aidha aliyataka mashirika ya umma yahakikishe
yanakamilisha madeni wanayodaiana wao kwa wao ili kusaidia mashirika ambayo
yanadai fedha nyingi kuweza kupata fedha za kuwekeza.
Akitolea mfano wa Tanesco, Mafuru alisema fedha ambazo
shirika hilo linadai katika mashirika na
taasisi nyingine zina uwezo wa kutekeleza mradi kama wa Kinyerezi I.
“Unaweza kuona kama madeni yote ya Tanesco yangelipwa,
ingekuwa imekamilisha mradi wa Kinyerezi II,” alisema.
VIKAO VINNE VYA BOSI KWA MWAKA
Akizungumzia kuhusu posho za vikao vya bodi, alisema kwa
sasa hivi kutakuwa na vikao vinne tu kwa mwaka tofauti na ilivyozoeleka ambapo
ikifika Januari kunakuwa na utitiri wa vikao.
Katika kuhakikisha Serikali inapata mapato ya kutosha,
aliyataka mashirika ya umma kupendelea kutumia benki za Serikali kuliko benki
binafsi.
POSHO ZA WABUNGE MARUFUKU
Kuhusu wabunge kulipwa posho kutoka hazina pindi
wanapokuwa katika vikao vya bodi mbalimbali, alisema kuwa zimepigwa marufuku
kwani posho zao wanalipwa na Bunge.
“Mtu mwingine anakuwa kwenye bodi zaidi ya moja kwa
sababu anajua kuwa kuna posho, hii haikubaliki, watakuwa wanalipwa posho za
Bunge tu,” alisema Mafuru.
MKURUGENZI TANESCO
Akizungumza baada ya kikao hicho, Mkurugenzi wa Tanesco,
Felchesmi Mramba, alisema kuwa wamejipanga katika kutekeleza agizo hilo la Rais
Magufuli kwa kushirikiana na Serikali ili waweze kufikia malengo.
MKURUGENZI BODI YA KOROSHO
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, Anna Abdallah,
alisema kuwa wao walishaanza kasi hiyo ya Dk. Magufuli miaka iliyopita na watu
waliwacheka, lakini walivumilia kwani walikuwa na lengo la kuiingizia Serikali
mapato.
ANNE MAKINDA
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Chai, Anne
Makinda ambaye ni Spika mstaafu wa Bunge, alisema Serikali imefanya vizuri
kuwakumbusha wajibu wao wa kuwatumikia wananchi kwa sababu mashirika hayo ni
yao.
“Haya mashirika ni ya wananchi na sisi lazima tutambue
kazi tunayofanya ni yao, hivyo lazima tutumie vizuri fedha zao na tuwe na
uchungu nazo,” alisema Makinda.
Alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu mabadiliko ya
malipo ya posho za wabunge, Makinda alisema: “Kama kuna kasoro zimeonekana
zirekebishwe, lakini mimi siwezi kukosoa muhimili ambao mimi niliuongoza,
hairuhusiwi kimaadili.”
BIL 4/- ZA UHURU KUJENGA BARABARA
Wakati hayo yakiendelea, Rais Magufuli, ameamuru Sh
bilioni nne zilizopaswa kutumika mwaka huu kugharamia shamrashamra za Siku ya Uhuru
inayofanyika Desemba 9 kila mwaka, zitumike kwa ajili ya upanuzi wa barabara
jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na
Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilieleza kwamba fedha hizo zitafanya kazi ya
upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco yenye urefu wa kilometa 4.3.
Upanuzi huo utaongeza njia mbili za barabara ya lami
katika eneo hilo na kuifanya kuwa na njia tano.
“Tayari fedha hizo kiasi cha shilingi bilioni nne
zimepelekwa kwa Wakala wa Barabara (Tanroads) kwa ajili ya utekelezaji wa agizo
hilo linalopaswa kuanza mara moja,” ilisema taarifa hiyo.
Rais Magufuli amemtaka Mtendaji Mkuu wa Tanroads,
Mhandisi Patrick Mfugale, kuanza ujenzi huo haraka ili kukabiliana na adha ya
msongamano wa magari katika barabara
hiyo.
MAGUFULI NA
LIPUMBA
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli jana alikutana na
kufanya mazungumzo na Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa
Ibrahim Lipumba.
Chanzo cha kuaminika kiliiambia MTANZANIA jana kuwa
pamoja na Profesa Lipumba kumpongeza Magufuli kwa ushindi na kutoa hotuba nzuri
katika uzinduzi wa Bunge, viongozi hao walizungumzia hali ya uchumi wa nchi.
Katika mazungumzo hayo, Profesa Lipumba alipewa kazi ya
kuandaa andiko la hali ya uchumi wa nchi na namna ya ukuzaji wa uchumi.
Pamoja na hali hiyo, Dk. Magufuli, alimpongeza Profesa
Lipumba kwa msimamo wake thabiti wa kupinga ufisadi na amemtakia heri katika
shughuli zake.
CHANZO: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment