![]() |
| Rais Dkt John Magufuli |
Kuna taarifa kuwa moto wa Serikali ya Rais Dk. John
Magufuli, katika kudhibiti ukwepaji kodi kwenye Bandari ya Da es Salaam, umezua
taharuki ya aina yake kwa wafanyabiashara walioshiriki kuingiza kinyemela
kontena 349 na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 80.
Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana
zilieleza kuwa kufuatia uamuzi wa serikali kumsimamisha Kamishna wa TRA na
kisha kumshikilia polisi na pamoja na vigogo wengine kadhaa wa mamlaka hiyo
huku pia kukitolewa amri kwa wafanyabiashara wote walioingiza makontena hayo
kulipa kodi mara moja kumeibuia hofu kubwa na tayari baadhi yao wameanza
kujisalimisha kwa nia ya kumuangukia Rais Magufuli.
Chanzo kimedai kuwa hadi sasa, tayari baadhi yao
wamekuwa wakihaha kwa kuwatumia watu mbalimbali wanaoamini kuwa wana ushawishi
ili wawasaidie kumuonea Rais Magufuli kwa matumaini kuwa watapewa nafasi ya
kulipa kodi waliyoikwepa na kisha kuachiwa ili waendelee na shughuli zao kama
kawaida.
“Kuna wafanyabiashara wakubwa walizoea kukwepa kodi na
kujipatia utajiri wa kutisha. Sasa mambo yameharibika… baadhi wanahangaika
kupata miadi ya kuonana na Rais Magufuli ili serikali iwasamehe kama
ilivyofanya wakati wa sakata la Epa. Ila wengi hawaelekei kufanikiwa kwa sababu
Rais Magufuli haingiliki kirahisi linapokuja suala la utekelezaji wa sheria za
nchi,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe jana, kikikumbushia ahadi ya Rais wa
Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, kwa watu waliochota fedha za Akaunti ya Malipo ya
Madeni ya Nje (EPA), pale alipowapa siku za kurejesha fedha walizokwapua ili
awasamehe.
Hata hivyo, akizungumza na Nipashe jana kuhusiana na
madai ya kuwapo kwa wafanyabiashara wanaohaha kuonana na Rais Magufuli, Katibu
Mkuu Kiongozi wa Ikulu, Ombeni Sefue, alisema (yeye) hana taarifa hizo, lakini
muhimu kwa kila aliyehusika na hujuma hiyo dhidi ya mapato ya serikali
kuhakikisha kuwa analipa mara moja kabla ya kutaka kujua ni hatua gani
zitakazofuata.
“ Sina habari kabisa kama (wafanyabiashara) wanafanya
jitihada kutaka kuonana na Rais au wanawatumia watu wa karibu na Rais kutaka
kuonana naye ili kuyamaliza mamabo hayo,” alisema Sefue
Alisema suala la wafanyabiashara kutakiwa kulipa kodi
halimhusu Rais Magufuli bali ni wahusika wenyewe ambao hawana namna nyingine
isipokuwa ni kulipa tu fedha hizo.
Sefue alisema kuwa katika suala hilo, hakuna majadiliano
wala msamaha bali kulipa kodi kama sheria inavyoelekeza.
Uingizaji wa makontena bila kulipiwa kodi ulishtukiwa na
serikali baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kufanya ziara ya kustukiza na
kubaini kuwapo kwa makontena 349 yasiyoonekana kwenye kumbukumbu za TRA licha
ya kuwamo katika takwimu za Mamlaka ya Bandari (TPA).
Chanzo kimoja kimeiambia Nipashe kuwa hivi sasa, ikiwa
ni siku tatu baada ya Rais Magufuli kumsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka
ya Kodi (TRA), Rished Bade na pia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwasimamisha
kazi vigogo wengine watano wa mamlaka hiyo kutokana na kashfa ya kutoonekana
kodi ya makontena 349 yaliyoingizwa nchini katika kipindi cha mwaka mmoja
uliopita, tayari kuna wafanyabiashara kadhaa wameanza kutapatapa kwa nia ya
kujinusuru.
Kadhalika, inaelezwa zaidi kuwa baadhi ya
wafanyabiashara waliohusika katika mchezo huo wamekuwa wakitafuta watu wa
kuwaunganisha kwa Rais Magufuli au Waziri Mkuu (Majaliwa) ili wawaangukie kwa
nia ya kuwapa nafasi ya kulipa kodi hiyo na kisha wasamehewe.
“Hili tishio la kukamatwa kwa wahusika baada ya
uchunguzi kukamilika linazidi kuongeza hofu kwa wafanyabiashara walioshirikiana
na maafisa wa TRA kuingiza makontena bila kuyalipia kodi,” chanzo kiliiambia
zaidi Nipashe.
Taarifa zaidi zilisambaa kwenye mitandao mbalimbali ya
kijamii jana kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakitafuta namna ya
kuondoka nchini kwa kujua kuwa wanaweza kukamatwa wakati wowote kutokana na
uchunguzi mkali unaoendelea kuhusiana na tuhuma za ukwepaji wa kodi.
Nipashe ilithibitishiwa kuwa miongoni mwa wale
wanaotajwa kuwamo katika orodha ya wafanyabiashara walioshirikiana na maafisa
wa TRA kuingiza makontena hayo bila kuyalipia kodi ni wafanyabiashara wakubwa,
tena baadhi yao wakiwa maarufu.
Inaelezwa kuwa matumaini ya baadhi ya wafanyabiashara
walioshiriki kuliingizia taifa hasara ya takriban Sh. bilioni 80 kutokana na
ukwepaji wa kodi katika kuingiza makontena ni pamoja na wale wanaomiliki
kampuni maarufu za bidhaa na huduma.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:
Post a Comment