TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(UKAWA), Freeman Mbowe amesema kuwa hawatashiriki shughuli ya kuapishwa kwa Dk.
John Pombe Magufuli inayotarajiwa kufanyika Alhamis, Novemba 5, 2015.
Kauli hiyo ya Mwenyekiti Mbowe aliyoitoa leo, imekuja
wakati kukiwa bado kuna sintofahamu kubwa miongoni mwa Watanzania kuhusu
mchakato wa uchaguzi hususan upigaji kura, ukusanyaji na ujumlishaji wa matokeo
ulivyofanyika hasa katika nafasi ya urais.
"Hatutahudhuria shughuli hiyo ya kumwapisha
Magufuli. Tumekubaliana wote kwenye UKAWA, ndani ya CHADEMA, viongozi wetu,
wabunge wetu wote hawatahudhuria uapishwaji wala sherehe.
"Tumetoa wito kwa wananchi wote, Watanzania wote,
wapenda mabadiliko na wapenda haki wote kwa ujumla kutohudhuria shughuli
hiyo," amesema Mwenyekiti Mbowe.
Mwenyekiti Mbowe amesisitiza kuwa UKAWA, wapenda
mabadiliko wote na Watanzania wapenda haki hawakubaliani na wanapinga mchakato
wa uchaguzi hususan matokeo ya urais ambayo, kwa mujibu wa Katiba ya Nchi
aliyosema ni mbovu, yakishatangazwa hakuna haki ya kuyapinga katika mahakama
yoyote ile.
"Tunataka nchi na dunia nzima ijue wazi kuwa
hatukubaliani na mchakato wa uchaguzi hasa matokeo ya urais ambayo kwa mujibu
wa Katiba yetu mbovu, Mwenyekiti wa Tume akishatangaza hakuna mahali pa
kuyapinga."
"Matokeo ya ubunge au udiwani yanaweza kupingwa
mahakamani, lakini kwa matokeo ya urais Katiba yetu mbovu inawafunga mikono na
miguu Watanzania wote ambao wangependa waone haki imetendeka katika nafasi
hiyo," amesema Mwenyekiti Mbowe.
"Watawala wamechezea haki ya Watanzania kupiga
kura. Kura zimehesabiwa kama karatasi za kawaida tu. Hujuma dhidi ya matokeo ya
wagombea wetu imehujumiwa waziwazi. Safari hii hujuma hazikuwa kificho tena.
Kila mtu amejionea matokeo yaliyokuwa na Jaji Lubuva si yale ambaye yalikuwa
yamebandikwa vituoni. Hayakuwa na uhalisia na matokeo yaliyokusanywa na
mawakala. Uchaguzi umefanywa kama ni jambo lisilokuwa na maana yoyote. Hiyo ni
hatari sana kwa taifa lolote linalotaka kukuza demokrasia kama mojawapo ya
nguzo za maendeleo. Hatuwezi kukubali kufika huko," amesema Mbowe.
Aidha, Mwenyekiti Mbowe ameongeza kusema kuwa vyama
vinavyounda UKAWA vimeitisha kikao cha Wabunge wateule wote wa vyama hivyo
ambao watakutana Alhamis, saa 4 asubuhi, jijini Dar es Salaam.
Imetolewa leo Jumatano Novemba 4, 2015 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
0 comments:
Post a Comment