TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kitendo
kilichofanywa na mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa cha kuomba kura kwa
kuwataka waumini wa madhehebu ya Kilutheri kumchagua yeye, kamwe hakikubaliki.
Imesisitiza kuwa kitendo hicho, kinawagawa Watanzania na
kuwapa mwelekeo wa kuchagua viongozi kwa misingi ya udini na ni ukiukwaji wa
Kifungu cha 2.2 (i) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani 2015,
kinachosema “Vyama vya Siasa au Wagombea hawaruhusiwi kuomba kupigiwa kura kwa
misingi ya Udini, Ukabila, jinsia au rangi.” Onyo hilo la NEC lilitolewa jana
na Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Damian Lubuva ikiwa ni muda mfupi tangu CCM
ilipoitisha mkutano wa waandishi wa habari, kuzungumzia suala hilo, huku
ikiitaka NEC kuchukua hatua dhidi ya ukiukwaji wa kanuni wa mgombea huyo wa
Chadema.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, NEC
imewakumbusha wagombea na vyama kuzingatia Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge
na Madiwani ambayo walikubali kuyafuata kwa kutia saini Julai 27, mwaka huu.
Ilisema inasikitisha kuona kiongozi au mgombea anatumia madhabahu kufanya
kampeni na mbaya zaidi kuomba kura kwa misingi ya kidini.
“Kitendo kilichofanywa na mgombea wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Edward Lowassa kuomba kura kwa kuwataka
waumini wa madhehebu ya Kilutheri kumchagua yeye hakikubaliki,” ilieleza sehemu
ya taarifa hiyo. Alisema Tume inavikumbusha Vyama vya Siasa kuzingatia Kifungu
cha 2.1 (k) cha Maadili kinachoelekeza vyama au wagombea kutotumia majengo ya
Ibada kufanya kampeni, na pia vyama au wagombea kutowatumia viongozi wa dini
kupiga kampeni kwa ajili ya vyama vya siasa au wagombea wao.
“Tunatumia fursa hii tena kuwaasa viongozi wa madhehebu
yote ya dini kutoruhusu vyama au wagombea au wanachama wa vyama vya siasa
kutumia nyumba za Ibada kufanya kampeni za uchaguzi wa rais, wabunge na
madiwani.” Jaji Lubuva alisema mbali ya hilo, Lowassa na viongozi wengine wa
Chadema wamekuwa na kauli za kuwaogofya wananchi kuwa ‘kura zitaibiwa’ na
kwamba Tume itasababisha machafuko, bila kutoa ufafanuzi jambo ambalo ni
hatari.
“Kauli hizo zinashangaza na kustaajabisha na ni kauli za
hatari sana kipindi kama hiki, kwa sababu maelekezo kwa vyama vya siasa na
wagombea, ambayo wagombea wote na vyama vya siasa walipewa, yana maelekezo
kuhusu utaratibu mzima wa kupiga na kuhesabu kura katika ngazi ya kituo,
kujumlisha kura katika ngazi ya kata, jimbo na taifa.
Akifafanua utaratibu ulivyo, Jaji Lubuva alisema
taratibu zote hizo hushuhudiwa na Mawakala wa Vyama vya Siasa na Wagombea,
ambapo kura zikihesabiwa ngazi ya Kituo, mawakala hupewa nakala ya matokeo
katika fomu Na. 21A Kura za Urais, 21B Kura za Mbunge na 21C Kura za Udiwani.
Alisema katika ngazi ya Jimbo, hesabu ya kura za kila kituo zilizopo pia katika
nakala la Fomu 21A za Urais na 21B za Mbunge hujumlishwa na matokeo kujazwa
katika fomu 24A kwa Rais na 24B Mbunge na Nakala ya matokeo wanapewa mawakala
wa vyama na wagombea waliopo katika kituo cha kujumlishia kura ngazi ya jimbo.
Kwa upande wa ngazi ya Taifa, alisema Tume hujumlisha
matokeo ya kura za Rais mbele ya wagombea na mawakala wa vyama na kutangaza
matokeo. Aliongeza kuwa katika hatua hizo, Chadema wanapaswa kueleza wizi
unafanyika wapi? “Jana Freeman Mbowe (Mwenyekiti Chadema Taifa) naye amesema
kuwa Tume inaegemea Chama Tawala, hivyo itasababisha uvunjifu wa amani. Hili
nalo ni tamshi lisilo la ukweli kabisa.
“Wakati wote Tume haiegemei wala kupendelea chama
chochote katika kazi zake. Mbowe anajua hivyo, chaguzi zote Tume imefanya kwa kutegemea
kura halali zote na ndiyo maana hata wabunge wa vyama vingine walitangazwa.
Alisema viongozi wote hasa wakuu wanaogombea Urais, yafaa wawe waangalifu
katika matamshi yao, vinginevyo matamshi ya aina hiyo yanaweza kujenga msingi
wa vurugu baadaye.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi inakumbusha vyama vya siasa
vijielekeze kwenye kutumia muda mwingi kuelezea Sera za vyama vyao ili ziweze
kupimwa na wapiga kura, badala ya kuchochea uhasama kati yao na Serikali na
Tume ya Uchaguzi. Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, NEC haitasita kukifikisha chama au
mgombea mbele ya Kamati ya Maadili ili aweze kuthibitisha kauli yake ;na
anaposhindwa Kamati itaweza kutoa adhabu kali kwa chama au mgombea husika,
ikiwa ni pamoja na kukatazwa kampeni kwa mhusika.
CHANZO: Habari Leo
0 comments:
Post a Comment