
Maelfu ya waandamanaji barani Ulaya walimiminika
barabarani jana Jumamosi kuwaunga mkono wakimbizi wanaelekea barani humo baada
ya kuzikimbia nchi zao zilizokumbwa na ghasia za vita.
Polisi wamesema kuwa kwa uchache watu 30,000 walishiriki
katika maandamano mjini Copenhagen, Denmark, yaliyoratibiwa na kundi
lijulikanalo kama "Refugees Welcome" (Karibuni Wakimbizi) na Venligboerne
(“Marafiki wa Mji”) kwenye mitandao ya kijamii.
Michala Clante Bendixen kutoka kundi la “Refugees
Welcome” amesema kuwa wananchi wamefanya vya kutosha kuwasaidia wakimbizi,
tofauti na serikali.
Polisi ya nchi hiyo imesema kuwa takriban watu 34,000 walikusanyika
katika mitaa ya Denmark kwa ajili ya maandamano kadhaa yaliyoratibiwa kwenye
mitandao ya kijamii.
Wakati huo huo maandamano mengine ya kuwaunga mkono
wakimbizi yalifanyika katika mji wa Budapest, nchini Hungary. Mamia ya watu
walikusanyika nje ya kituo kimoja mashariki mwa mji huo, ambapo wanaharakati
waliitaka serikali kutowarudisha wakimbizi nchini Serbia, mahali wanapopita
kuingilia Hungary.
Waandamanaji walikuwa wamebeba mabango yaliyokuwa na
ujumbe mbalimbali kama vile “Yesu alikuwa mkimbizi pia” na “Wakimbizi Karibuni”,
na kadhalika.
Mnamo Juni 17 Hungary iliamua kujenga uzio wenye urefu
wa mita tatu kwenda juu na unaotandaa umbali wa kilometa 175 kwenye mpaka wake
na Serbia ili kuwazuia wakimbizi wasiingie.
Wakati huo huo, watu wengine 5,000 walifanya maandamano
mjini Vienna, Austria kuwaunga mkono wakimbizi.
Waandamanaji hao waliokusanyika katika medani ya Christian-Broda-Platz
waliitaka serikali kufungua milango kwa ajili ya wakimbizi wengine na kuboresha
hali za maisha katika kambi za wakimbizi zilizopo.
Walibeba mabango yaliyosomeka, “Hakuna mwanadamu haramu”,
“Waislamu na wakimbizi karibuni”, na “Ondoeni mipaka”.
Awali maelfu ya watu walijaa katika Medani ya Bunge
katikati mwa mji wa London hapo jana mchana wakiitaka serikali ya Uingereza na
viongozi wa Ulaya kuongeza juhudi kushughulikia mateso ya wakimbizi. “Semeni
kwa sauti, semeni kwa uwazi! Wakimbizi wakaribishwe hapa!” ni miongoni mwa nara
zilizosikika kwenye maandamano hayo yaliyowashirikisha maelfu ya watu.
Maelfu kwa maelfu ya wakimbizi wanasafiri kuelekea
Ulaya, ambayo inakabiliwa na kile kinachoitwa kama mgogoro mbaya zaidi wa
wakimbizi barani humo tangu Vita ya Pili ya Dunia.
Hivi karibuni Muungano wa Ulaya uliamua kuwapokea
wakimbizi 140,000, huku utawala wa Obama ukisema kuwa utawaruhusu wakimbizi 10,000
wa Syria kuingia nchini Marekani kwa mwaka 2016.
Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi hivi
karibuni lilisema kwa uchache watu 850,000 wanatarajiwa kuvuka Bahari ya
Mediterania mwaka huu na mwaka 2016; na kwamba zaidi ya nusu ya wakimbizi
waliofika Ulaya mwaka huu wanatokea Syria.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu 250,000 wamepoteza
maisha tangu vita ilipolipuka nchini Syria na wengine milioni 10 ni wakimbizi –
milioni 6 ni wakiwa wakimbizi wa ndani.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kuna wakimbizi milioni 1.9
wa Syria walioandikishwa nchini Uturuki pekee mpaka kufikia Agosti 25.
0 comments:
Post a Comment