![]() |
| Mama Anna Mghwira katika harakati za kisiasa |
MAMA ANNA ELISHA MGHWIRA.
Mgombea Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania 2015
kwa tiketi ya ACT WAZALENDO.
Chama cha ACT Wazalendo kimemteua na kumpitisha Mama
Anna Mghwira kuwa mgombea Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika
uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, 2015. Pia kimemteua na kumpitisha Ndugu
Hamad Mussa Yusuf kuwa mgombea mwenza wake.
Mama Anna Mghwira ambaye ni Mwenyekiti Taifa wa chama
cha ACT Wazalendo, anakuwa mwanamke wa pili kuwania nafasi ya Urais katika
historia ya siasa za Tanzania.
NI NANI HUYU Anna Elisha Mghwira?
Mama Anna Mghwira alizaliwa Januari 23, 1959 katika
hospitali ya Mkoa wa Singida, kata ya Mungumaji, kitongoji cha Irao, Manispaa
ya Singida Mjini.
Baba mzazi wa Anna alikuwa Diwani na kiongozi wa TANU
kabla ya CCM hadi mwaka 1985, mama yake alijishughulisha na kilimo na ufugaji
na wazazi hawa kwa ujumla walipata watoto tisa akiwemo Anna.
Alianza safari ya kielimu katika shule ya Msingi Nyerere
Road mwaka 1968 - 1974 akaendelea na Sekondari kwenye shule ya Ufundi Ihanja
kati ya mwaka 1975 - 1978 kabla ya kuhitimisha masomo ya juu ya Sekondari
(kidato cha Tano na Sita) Lutheran Junior Seminary mwaka 1979 - 1981.
Mwaka 1982 alijiunga na Chuo Kikuu cha Theolojia cha
Tumaini na kuhitimu Shahada ya Theolojia mwaka 1986.
Mwaka huohuo 1986 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM) ambako alisoma na kuhitimu Shahada ya Sheria (LLB).
Aliendelea na shughuli za ujenzi wa Taifa akifanya kazi
ndani na nje ya Tanzania na kupata uzoefu mkubwa.
Mwaka 1999 alijiunga na Chuo Kikuu cha Essex, nchini
Uingereza na akatunukiwa Shahada ya Uzamili ya Sheria (LLM) mwaka 2000.
Licha ya kuwa mwanatheolojia na mwanasheria aliyebobea
pia amefanya kazi za maendeleo kwa muda mrefu na ana uzoefu katika uendeshaji
wa Serikali za Mitaa, Utumishi katika Mashirika ya Kitaifa, Kimataifa,
mashirika ya dini ambamo amejihusisha na Masuala ya Wanawake, Watoto,
Wakimbizi, Utawala Bora na Haki za Binaadamu.
Mama Anna Mghwira ana historia ya kupenda siasa, masuala
ya jamii na michakato ya maendeleo kama inavyojidhihirisha katika maandiko yake
mbalimbali katika safu za magazeti na majarida ndani na nje ya Tanzania. Jambo
hili linampambanua Anna na wagombea wengine ambao hawaandiki chochote na hata
hotuba zao huandikiwa.
Alianza siasa Tangu wakati wa TANU akiwa mwanachama wa
Umoja wa Vijana wa TANU (TANU YOUTH LEAGUE) na aliwahi kushinda tuzo mbalimbali
kutokana na ushiriki wake wa juu katika TANU lakini baadae ilipoanzishwa CCM
alipunguza ushiriki wake ili ajipe muda zaidi katika masomo na baadae Ndoa na
Malezi ya watoto.

Aliolewa na Shedrack Mghwira tangu mwaka 1982 na
walibahatika kupata watoto watatu wa kiume Fadhil, Peter na Elisha. Hata hivyo
kwa bahati mbaya, mumewe kwa hivi sasa ni marehemu.
Kwa muda mrefu hakuwa akijihusisha na siasa mpaka mwaka
2009 ambako alijiunga na chadema na kushika nyadhifa za Mwenyekiti wa Baraza la
Wanawake ngazi ya Wilaya na Katibu wa Baraza la Wanawake ngazi ya Mkoa.
Machi 2015 alijiunga na chama kipya cha ACT Wazalendo na
Machi 28, 2015 Mama Anna Mghwira aliingia kwenye historia ya siasa za mageuzi
Tanzania baada ya Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Chama Cha ACT Wazalendo kumchagua kwa
kura nyingi kuwa Mwenyekiti Taifa wa Kwanza wa chama hicho na pia Mwanamke wa
Kwanza katika historia ya siasa za Tanzania kuwa Mwenyekiti Taifa wa chama cha
Siasa.
Agosti 20, 2015 Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia wa Chama
cha ACT Wazalendo ulimteua na kumpitisha kuwa mgombea wa nafasi ya Urais
akipeperusha bendera ya chama hicho.
Agosti 21, 2015 amechukua fomu na kukamilisha taratibu
zote za kisheria na kuteuliwa Rasmi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (National
Electoral Commission) kumthibitisha kama mgombea Urais rasmi wa Chama cha ACT
Wazalendo.
Mama Anna Mghwira hana madoadoa ya ufisadi na wala
hahitaji dodoki la kumsafisha. Ni mtu mwenye uwezo na sifa za kuwa Rais wa
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa kazi za Rais ambazo ni kufikiri, kuwa
mlinzi Mkuu wa Umoja, Amani na Tunu za Taifa na kuwa mfano bora wa ubinaadamu
anazimudu.
Akizungumzia uteuzi wake kwa nafasi hiyo Mama Anna
anasema: "Taifa linahitaji kiongozi mwenye moyo wa nyama, mwenye upendo,
maono, uadilifu, uzalendo na mwenye uwezo wa kuwaunganisha watu wote bila
upendeleo na huyo sio mwingine bali ni Ndugu Anna Elisha Mghwira".

0 comments:
Post a Comment