![]() |
| Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki |
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Mecky Sadiki amepiga
marufuku biashara ya kuuza vyakula maeneo hatarishi ili kukabiliana na ugonjwa
wa kipindupindu. Aidha amepiga marufuku maji ya viroba maarufu kama maji ya
Kandoro, matunda yaliyomenywa na juisi zilizotengenezwa kienyeji.
Alitoa maagizo hayo jana wakati akizungumzia hali ya
kipindupindu jijini Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa huyo akifafanua kuhusu marufuku
hiyo alisema wapo watu wanaouza vyakula katika maeneo yaliyo karibu na mitaro
ya maji machafu, kwenye vizimba vya kukusanyia taka, karibu na vyoo hali ambayo
ni hatari kwa afya.
Sadik aliongeza kuwa hadi kufikia jana kulikuwa na
wagonjwa 56 ambao walibainika kuwa na dalili za ugonjwa huo wakitoka katika
maeneo ya Makumbusho, Kijitonyama, Kimara, Sangara, Manzese, Kigogo, Tandale na
Mwananyamala.
Mkuu huyo alisema wagonjwa waliopo katika kambi hadi
kufikia jana walikuwa wagonjwa 36 na waliopata matibabu na kuruhusiwa ni
wagonjwa 17 na kusema idadi ya vifo vya ugonjwa huo ni watu watatu. Aidha
alisema ni marufuku kufanya shughuli za mazishi na kuweka matanga kwa familia
zilizopoteza ndugu zao kwa ugonjwa huo.
“Nawataka viongozi wa serikali za mitaa na viongozi wa
kata kupiga marufuku familia zilizokumbwa na ugonjwa huo kufanya shughuli za
mazishi kwa ndugu zao na hata kuweka matanga,” alisema Sadiki.
Mkuu huyo alisema kutokana na wagonjwa wa kipindupindu
kuongezeka wameanzisha kambi mpya kwa wagonjwa wapya wa ugonjwa wa kipindupindu
Mbagala jijini Dar es Salaam ili kuepusha mlundikano wa wagonjwa katika kambi
moja. Hadi sasa kuna kambi tatu zinazohudumia wagonjwa ikiwemo ya Mwananyamala
Mburahati na Mbagala.

0 comments:
Post a Comment