
Ndugu waandishi wa habari na ndugu Watanzania wenzangu.
Yamepita majuma mawili tangu mchakato wa kuchagua mgombea urais wa Tanzania
kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) ukamilike. Nimetumia muda huu kutafakari kwa
kina yaliyotokea Dodoma na hatima yangu katika siasa nchini. Ninajua marafiki
wengi na wananchi wenzangu wanaoniunga mkono wamekuwa wakisubiri kwa hamu nitoe
kauli.
Nilipokuwa natangaza nia ya kugombea urais kule Arusha,
nilieleza nia yangu ya kuanza mchakamchaka wa maendeleo ya nchi yetu na
kuondokana na umaskini. Pamoja na yaliyotokea Dodoma, azma hii bado iko
palepale.
Lakini nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa
Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetupa sisi pumzi ya kuendelea kuwa wazima
wa afya njema hadi hivi sasa. Nawashukuru pia mke wangu Regina, wanangu,
wanafamilia na marafiki wote kwa mapenzi, msaada na uvumilivu wao wakati wa
kipindi hiki kigumu tunachopitia. Nawashukuru sana pia maelfu ya wanachama wa
CCM walionidhamini na mamilioni zaidi walioniunga mkono.
Katika safari zangu za mikoani wakati wa kuomba
udhamini, nilitiwa hamasa na umati mkubwa wa watu waliojitokeza kuniunga mkono.
Aidha, ninawashukuru sana wana kamati wangu, makundi mbalimbali na mamilioni ya
vijana wakiwamo; “For You Movement”, “Friends of Lowassa” “Team Lowassa”, Umoja
wa Bodaboda na wengine wengi ambao walijitolea kwa hali na mali katika Safari
yetu ya Matumaini.
Nitakuwa sijahitimisha orodha ya shukrani iwapo nitaacha
kuwashukuru viongozi wa dini zote nchini ambao waliungana na waumini wao wengi
katika maombi na kwa kuniunga mkono. Najua sote tumevunjika moyo kwa
yaliyotokea Dodoma na mazingira yaliyopelekea matokeo yale.
Kama ilivyokwishaelezwa, mchakato wa kuteua wagombea
uligubikwa na mizengwe, ukiukwaji wa maadili, uvunjaji wa Katiba na taratibu za
uchaguzi za CCM.
Zaidi ya hayo uchaguzi ulisimamiwa kwa upendeleo dhahiri
na chuki iliyokithiri dhidi yangu. Kikatiba, Kamati ya Maadili si chombo rasmi
na haina madaraka ya kuchuja na kupendekeza majina miongoni mwa wale wanaoomba
kugombea Urais kupitia CCM.
Kilichotokea Dodoma ni kupora madaraka ya Kamati Kuu na
kukiuka katiba ya CCM. Aidha, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu viliitishwa na
kuburuzwa ili vitekeleze azma ya watu binafsi pasipo kujali demokrasia, katiba,
kanuni na taratibu za uchaguzi ndani ya CCM. Niliwekewa mizengwe na kuzushiwa
majungu na uongo mwingi, kuhakikisha kuwa jina langu halifikishwi mbele ya
Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kujadiliwa licha ya ukweli usiopingika kuwa
nilikuwa mgombea anayeungwa mkono na wananchi na wanachama wengi wa CCM kuliko
wenzangu wote. Kibaya zaidi ni kile kitendo cha kuwanyima wagombea wote 38 haki
ya kujieleza mbele ya Kamati Kuu.
Ni dhahiri kwamba njama dhidi yangu ndani ya CCM si
jambo jipya. Kumekuwa na mkakati wa siku nyingi wa kulichafua jina langu kwa
uzushi na uongo usio na kifani. Aidha, mmeshuhudia jinsi vijana kadhaa
walivyotumika kunikashifu na kunitukana na bila aibu na uongozi wa CCM na
Serikali kuwazawadia madaraka makubwa.
Kwa namna ya kipekee napenda kuwapongeza na kuwashukuru
wazee wetu akiwamo Mzee Kingunge Ngombale Mwiru na baadhi ya wajumbe wa Kamati
Kuu ikiwa ni pamoja na waheshimiwa Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Alhaj Adam
Kimbisa kwa uadilifu na ushujaa wao mkubwa wa kuisimamia katiba ya CCM na
misingi ya haki na kukataa maamuzi batili ya Kamati ya Maadili na Kamati Kuu
kuhusu uteuzi wa wagombea.
Cha msingi kuzingatia ni kuwa ili kuhitimisha njama za
kunipora mimi na wagombea wengine haki zetu za msingi za kusikilizwa, viongozi
wachache walikuwa tayari kupanda mbegu ya chuki na mfarakano ambao ni mfano
mbaya kwa CCM na hata Taifa letu. Watanzania walitarajia chama kinachoongoza
nchi kiwe ni mfano wa utawala wa sheria na kinara katika kutetea misingi ya
haki na demokrasia na siyo kuihujumu. Yaliyotokea Dodoma yameitia dosari nchi
yetu.
Kwa kifupi, ninaamini sikutendewa haki katika mchakato
mzima wa kupendekeza majina na kuteua mgombea wa urais kupitia CCM. Nilinyimwa
haki yangu ya msingi ya kusikilizwa na kuchaguliwa.
Kwa mantiki hii nitakuwa mnafiki kama nitaendelea
kujidanganya mimi mwenyewe na umma wa Watanzania kwa kusema kuwa bado nina
imani na CCM au kuwa CCM ni chama kitakachowaletea ukombozi wa kweli wa
kiuchumi, kisiasa na kijamii. CCM niliyoiona Dodoma siyo tena kile chama
nilichokulia na kilichonipa malezi na maadili ya siasa yaliyojengwa kwenye
misingi ya haki, usawa na uadilifu.
Ni dhahiri kwamba CCM imepotoka na kupoteza mwelekeo na
sifa ya kuendelea kuiongoza Tanzania yetu. Mimi kama Mtanzania aliye na uchungu
na nchi yake nasema imetosha na SASA BASI!
Kama Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
alivyosema, CCM siyo baba yangu wala mama yangu na kwamba kama Watanzania
hawapati mabadiliko ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM. Sasa tuyatafute
mabadiliko nje ya CCM.
Hivyo basi, baada ya kutafakari kwa kina nimeamua kuwa
kuanzia leo ninaondoka CCM na kuitikia wito wa Ukawa kupitia Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuungana nao katika kuleta mabadiliko ya
kweli ya nchi yetu. Navishukuru vyama vyote vya siasa chini ya Ukawa, yaani
Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD kwa mwaliko wao na imani yao na kuthamini
mchango ninaoweza kutoa kufanikisha azma ya kuleta mabadiliko na maendeleo ya
kweli ya Taifa letu. Waheshimiwa Freeman Mbowe, Profesa Ibrahim Lipumba,
Mheshimiwa James Mbatia na Emmanuel Makaidi asanteni sana.
Ndugu zangu, sikuufanya uamuzi huu kwa pupa, lakini
unafika wakati wa kuchukua maamuzi hata kama ni magumu kwa kuamini fika kuwa ni
kwa masilahi ya Taifa letu.
Nimejiridhisha kuwa ndani ya Ukawa Taifa letu linayo
fursa ya pekee na ya kihistoria kushinda Uchaguzi Mkuu ujao na ya kuleta
mabadiliko ya msingi katika nchi yetu. Kwa uamuzi na ushiriki wangu huu,
ninaamini kwa dhati kuwa tutaondoa uhodhi wa madaraka wa chama kimoja na
kujenga demokrasia yenye ushindani wa kweli kisiasa.
Namalizia kwa kutoa wito kwa Watanzania wenye nia njema
na nchi yetu na wanaotaka kujenga demokrasia na kuleta mageuzi na maendeleo ya
kweli, kujiunga nasi katika safari hii mpya ya kuinusuru nchi yetu.
Safari ya Matumaini inaendelea kupitia Ukawa lakini
haitafanikiwa iwapo sote hatutajiandisha kupiga kura. Natoa wito kwa wakazi wa
Dar es salaam, kutumia fursa iliyopo kujiandikisha kwa wingi.
Aidha, nawakumbusha Watanzania kote nchini
waliojiandikisha kutunza shahada zao na kukumbushana kupiga kura ili ifikapo
Oktoba mwaka huu tupate ushindi wa kishindo.
Ndugu zangu Watanzania, tuungane pamoja kuuondoa
umaskini na kuleta mabadiliko ya kweli.
NARUDIA CCM SIYO MAMA YANGU
0 comments:
Post a Comment